Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Thomas Maganga Kampala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. THOMAS M. KAMPALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mosi nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu wa mbinguni kwa kuniwezesha leo siha njema kusimama mbele yako na kuchangia hotuba ya Waziri wa Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwa moyo wa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha kwa vitendo. Leo wakati ninakuja kuchangia hapa nimemwona mama huyu akigawa majiko kuonyesha ni namna gani alivyo serious na mambo ya mazingira, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Waziri wa Mazingira na Muungano, ndugu yangu Hamad Yussuf Masauni kwa wasilisho zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunakubaliana mazingira ndiyo kila kitu. Uhai wetu sisi unahitaji mazingira, kilimo kinahitaji mazingira, afya zinahitaji mazingira, viwanda vinahitaji mazingira, kila kitu kinahitaji mazingira. Ukisikiliza wasilisho la Waziri ameongea, kwa mwaka Tanzania inapoteza hekta 469,420 za misitu. Kwa miaka mitano tunapoteza hekta 250,000. Hizi hekta 250,000 ni sawa square kilometer 23,500. Square kilometer 23,500, Mkoa wa Mwanza una square kilometer 25,233. Kwa hiyo, kwa miaka mitano tunapoteza misitu yenye ukubwa wa Mkoa wa Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumepitisha hapa mpango. Kwa kasi hii ya upotevu wa misitu ni kubwa ya kiwango hiki baada ya miaka 10 huu mpango hautakuja kutekelezeka. Nini ushauri wangu? Tumeongea sana hapa. Imefikia wakati sasa Serikali ifanye maamuzi. NEMC wamepewa jukumu kubwa sana, lakini NEMC amepewa jukumu ni sawa na nyoka wa kwenye ngoma. NEMC amepewa jukumu halafu hana meno lazima tukubaliane, umefika wakati sasa wa NEMC kuwa mamlaka kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye miji yetu mikubwa, ukienda vijijini kwenye kila eneo, tatizo kubwa ni uharibifu wa mazingira. Leo hii tunayoongea NEMC hana uwezo wowote wa kwenda sehemu akafika akakuta kuna eneo ambalo lina uharibifu mkubwa wa mazingira. Kwa mfano, kila siku huwa ninatolea mfano ukienda kwenye Mkoa wa Mwanza kila mwaka mvua zinaponyesha kuna disaster za mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kuangalia mafuriko mengi yanayotokea kwenye mikoa ya Mwanza na majiji makubwa changamoto kubwa ni shughuli za kibinadamu. Kwa mfano Mto wa Mkuyuni pale ukienda Mto wa Mkuyuni juzi tu kulikuwa kwenye mafuriko makubwa sana. Chanzo cha mafuriko yale ya Mto wa Mkuyuni vimetolewa vibali vya ujenzi, ule mto pembeni yake kumejengwa viwanda vikubwa, mbele ya daraja ukienda pale Mkuyuni utakuta kuna ghorofa limejengwa NEMC hana mandate ya kumwambia yule bwana avunje. Matokeo yake sasa NEMC kazi yake ni kutoa ushauri tu. Akifika anatoa ushauri na vifaini vidogo vidogo. Kama tunataka Taifa hili lipige hatua lazima tukubaliane NEMC sasa iwe mamlaka kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya kaboni; halmashauri zetu nyingi zimejipanga kuingia kwenye biashara ya carbon na hili jambo, Waziri Mkuu yuko hapa ni vizuri akasikiliza vizuri na akalichukulia hatua tatizo la halmashauri nyingi kuingia kwenye biashara ya carbon ni TFS. TFS wamekuja kwenye halmashauri zetu, wamechukua misitu kila kwenye kijiji wameweka GN. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye halmashauri zetu sisi tunaotoka vijijini kila sehemu ukizunguka GN za TFS na TAWA zimekuwa kama kombati ya jeshi. Sasa tukijipanga kuingia kwenye biashara ya carbon credit huku unakuta kuna zuio la NEMC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikubaliki na hawa TFS sio kwamba wanakataa sisi tusiingie kwenye biashara ya carbon credit wana faida na hii misitu. Hapana, ukienda pale sasa hivi kwenye halmashauri zetu kuna kuna contradiction kati ya TAWA na TFS. TAWA wanahifadhi misitu, TFS wanakata misitu. Leo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anapiga magoti kupanda miti halafu huku kuna taasisi la Serikali kazi yake kukata miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane TFS na TAWA wanafanya kazi moja ni sawa na Dula na Abdalla. Kuna sababu gani ya kuwa na taasisi nyingi? Hakuna sababu ya kufunga mpaka asiyekula panya. Lazima tukubaliane hapa hizi taasisi kila mmoja kama kuna majukumu ya TFS ni bora yakapelekwa TAWA kwa sababu sasa kule kijijini ni shida, TFS ni disaster kubwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nije kwenye kuchangia Muungano; ni muumini mkubwa sana wa muungano. Kwangu mimi Muungano ni Imani; mtu akiugusa Muungano mbele yangu ni sawa na kunishika bega wakati wa tafaruku ile. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akigusa Muungano kwangu atakutana na matatizo makubwa kweli kweli. Muungano unazo faida nyingi sana ambazo kwa akili ya kawaida tu unaweza usizione, lakini napenda kueleza ni mmoja ya watu ambao wako tayari kulinda Muungano kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri aje na majibu lini NEMC itakuwa mamlaka kamili na Mheshimiwa Waziri asipokuja na haya majibu shemeji yangu alikuwa pale juu, shemeji ninaondoka na mshahara wa mzee. Bila majibu ya lini NEMC itakuwa mamlaka ninapita na mshahara bila kujali matatizo yatakayotokea nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)