Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Christina Solomon Mndeme

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kupata nafasi ya kuchangia siku ya leo mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii nami kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri aliyowasilisha leo hapa Bungeni. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais. Pamoja na hilo nitumie na fursa hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeye akiwa mwana mazingira namba moja; yeye akiwa kinara wa nishati safi ya kupikia. Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uongozi wake thabiti Mheshimiwa Rais, ameonyesha maono yake na nia yake. Ameweka mikakati thabiti ya kusimamia suala la mazingira nchini. Katika hili tumemwona Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuliweka suala la mazingira kulipa kipaumbele ameliweka katika dira yetu ya maendeleo ya mwaka 2020 - 2050. Ili sasa suala la kuhifadhi, kulinda na kutunza mazingira lipewe kipaumbele kwa sababu ndiyo suala muhimu linotufikisha katika maendeleo na mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua suala la mazingira ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa letu amefanya mambo mbalimbali katika nchi yetu na anaendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameiwezesha NEMC kupata maabara tembezi yaani mobile laboratories haijawahi kutokea katika nchi hii. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ameipatia NEMC maabara hii ili kuweza kuiongezea uwezo NEMC kufanya udhibiti wa kina, uchambuzi wa mazingira, kusimamia suala la uchafuzi wa mazingira kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Hii ni historia katika nchi yetu na ndiyo maana Wabunge wengine wamesema nami ninaungana nao tunahitaji sasa mabadiliko ya kisheria. NEMC sasa ibadilike kutoka kuwa baraza na kuwa mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunayasema haya? Kwa uchache zipo sababu kadhaa; sababu ya kwanza, NEMC itakapobadilika kwenda kuwa mamlaka itaongezewa nguvu ya kisheria; pili, ufanisi wa kazi zake utaongezeka bila kuingiliwa na taasisi zingine; tatu usimamizi wa masuala ya mazingira utaongezeka; nne, uwajibikaji utaongezeka katika kusimamia sheria za mazingira bila kuwepo na mgongano na taasisi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, utoaji wa vyeti vya tathmini ya mazingira utafanyika kwa uharaka bila kucheleweshwa; sita, hawategemei Mamlaka za Serikali za Mitaa au Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yao katika suala zima la udhibiti wa mazingira na kusimamia sheria; saba, kutaondoa migongano ya majukumu na wadau wengine kwa kutambua kuwa NEMC sasa ni mamlaka na hivyo itaongeza ushirikiano na taasisi zingine; nane, kutakuwepo na ulinzi wa mazingira kwani udhibiti wa uchafuzi na utupaji wa taka hovyo utafanywa kwa kiwango cha juu na mamlaka hii mpya ambayo utaundwa sio baraza mamlaka ya mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tisa, hilo baraza litakapoundwa litapatiwa mamlaka kamili na hivyo NEMC itapata nguvu ya kuongeza mapato, itakuwa na mwonekano mpya, lakini na wawekezaji watakuwa na imani na baraza hili jipya ambalo litaundwa na mamlaka hii mpya ambayo itaundwa. Ulinzi wa rasilimali za mazingira utakuwepo na utasimamiwa kwa uaminifu mkubwa na uwajibikaji mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchelewa kuleta mabadiliko haya ya sheria katika Bunge lako hili Tukufu kunasababisha athari mbalimbali ikiwemo NEMC kuchelewa kutoa maamuzi ikiwemo kutoa vyeti na vibali mbalimbali kwa sababu ya mwingiliano na mlolongo mrefu sana. NEMC ikibadilika ikiwa mamlaka kutakuwa kuna direct enforcement ya sheria. Kwa kuchelewa kuleta mabadiliko haya ya kisheria, mwajibikaji hafahamiki ipasavyo, je, ni NEMC? Je, ni Mamlaka za Serikali za Mitaa? Je, ni polisi? Tunataka sasa NEMC iwe na nguvu na iwe na meno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchelewa kuleta mabadiliko haya taswira ya NEMC inaendelea kudhohofika kwa wawekezaji. Vilevile kunakuwa kuna ongezeko la malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali. Sasa NEMC huyu ni eyes on, hands off hana nguvu. Tumwongezee nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayasema haya ili dira yetu ya mwaka 2020 - 2050 ili iweze kufikiwa kikamilifu na malengo yake yatekelezwe kamilifu, tunahitaji mabadiliko ya sheria hii iletwe Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ambaye ndiye kinara wa nishati safi ya kupikia, tunampongeza sana kwa kuleta hii ajenda ya nishati safi kwa Watanzania. Mafanikio makubwa yameonekana, leo hii takribani taasisi 3,350 zimehama kutoka kutumia nishati isiyo salama, sasa hivi inatumika nishati iliyo salama. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini na matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mpaka 23%, haijawahi kutokea!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa uchumi wa bluu. Usimamizi mzuri na uendelezaji wa uchumi wa bluu nchini tunauona. Rasilimali maji zinatumika kwa sababu ya mazingira mazuri aliyoyaweka Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali sasa iweke mfumo mzuri ili sasa rasilimali maji hii iweze kutumika vizuri. Ushauri mwingine kwa sababu ya muda; tunaona jitihada za upandaji miti zinafanyika nchini, lakini sasa tunashauri uwekwe mfumo mzuri wa kufuatilia ile miti inayopandwa je inakua? Sustainability ya ile miti inayopandwa iwepo lakini vilevile, biashara ya kaboni. Tunaipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Kituo hiki cha Kitaifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda umekwisha ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)