Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Hija Hassan Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na leo kwa mara ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake uliotukuka na ambao unatuletea masilahi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda ninaomba niwashukuru sana viongozi wangu wa Chama Cha Mapinduzi kwa ujasiri wao na uamuzi wao sahihi wa kuamua sasa kuwa mwana-CCM na kuwa Mbunge wa Jimbo la Kiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kiwani kwa uamuzi wao wa kutupatia kura wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi na kuwa washindi ndani ya Jimbo la Kiwani na hatimaye kuwa viongozi wa nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa mchango wangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo ametoa hotuba yake iliyoeleweka na ambayo ina kiwango. Ninamwelewa Mheshimiwa Masauni kwamba jambo hili halikuwa gumu kwake kwa sababu tumeuelewa uwezo wake wa kufanya kazi kwa mujibu na kwa maslahi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Dira ya Wizara hii eneo la Muungano sina shida nalo, liko sawa na tunaunga mkono kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza. Kwa msingi huo na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kiwani ninaomba tudumishe Muungano na tuutetee kwa nguvu zote kama alivyosema wenzetu hii ndiyo silaha pekee ambayo itafanya Tanzania kuishi katika amani na ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mazingira ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Wizara yake kwa kutujengea tuta ambalo limejengwa eneo la Sepwese mpakani mwa Jimbo la Kiwani ambalo limenusuru sana athari ya kimazingira katika mashamba ya wakulima na leo hii wananchi wa Jimbo la Kiwani na Jimbo la Mtambile wamekuwa na unafuu mkubwa kwenye eneo hili la mazingira baada ya kujengwa tuto la Mheshimiwa Waziri chini ya Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba, kama kuna eneo ambalo limeathirika Pemba, basi ni Jimbo la Kiwani na ni kutokana na ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayoendelea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kujenga barabara Pemba bila kuzungumza Kiwani. Huwezi kujenga miundombinu ya gati bila kuzungumza Jimbo la Kiwani hususan kwenye Wadi ya Muwambe. Nimwombe Mheshimiwa Waziri afanye ziara makusudi kuja kuangalia mazingira haya ili kufanya busara kwa ajili ya kuokoa wananchi wa Jimbo la Kiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kwa sababu ya muda kwenye suala la biashara ya carbon. Nimejaribu kufanya utafiti tangu asubuhi na kuona kwamba yale ambayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akitueleza kwa kweli yako makubwa zaidi ambayo Mheshimiwa Waziri hajatupatia maslahi ya elimu ya wananchi wa Tanzania. Mara nyingi Mheshimiwa Waziri amekuwa akizungumzia biashara ya carbon kwa eneo la misitu ya ardhini. Mheshimiwa mwenzangu Mbunge hapa wa Mkoa wa Tanga amezungumzia juu ya suala la blue carbon.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti mdogo hapa, nimeona kwamba biashara ya carbon inayotokana na misitu ya ardhini bei yake ni dola tano mpaka dola 25 kwa tani moja ya carbon dioxide ya biashara hii, lakini biashara ya blue carbon kwa tani hiyo hiyo kwa kipimo hicho hicho bei yake ni dola 45 mpaka 70. Maana yake nini? Kumbe biashara hii kwenye bahari kuu ina thamani kubwa zaidi kuliko ili biashara hii kwenye misitu yetu ya ardhini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo Mheshimiwa Waziri ana kazi kubwa ya kufanya, lazima apambane na atuelekeze kwenye kufanya biashara hii mbele ya misitu ya ardhini na katika eneo la bahari. Watanzania wanahitaji kufanya biashara hii ili wajikwamua na umaskini wao na wajenge nchi yao, nchi yenye kipato cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie, Tanzania ina misitu hekta 160,000 na kwa mujibu wa utafiti huu kama misitu hiyo itawekezwa kwenye biashara hii maana yake Tanzania ina uwezo wa kupata dola milioni 320 kwa mwaka. Sasa kama hilo ni jambo sahihi, ni kwa nini Mheshimiwa Waziri asifanye juhudi na kuwekeza kwenye eneo hili kwa ajili ya kulinda uchumi wetu na kuongeza mapato ya Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri na ninaomba Wabunge wenzangu tupitishe bajeti hii ili tumpe nguvu Mheshimiwa Waziri apambane kutafuta fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye biashara ya carbon kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Hija Hassan Hija. Waheshimiwa Wabunge, sasa tunaenda kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo.