Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kushiriki kwenye sehemu ya majumuisho ya mjadala wetu huu wa Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunifanya kuja kumsaidia Mheshimiwa Waziri wetu wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Vivyo hivyo, ninamshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa maelekezo na mwongozo wakati wote ambao wamekuwa wakitupatia ndani ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amekuwa kiongozi wa shughuli zetu za Serikali za kila siku. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo amekuwa mlezi mzuri kwa siku chache hizi ambazo nimekuwa Wizarani, lakini na kwa namna ambavyo ametupa uelekeo mpya wa Wizara yetu na kwa kupitia bajeti hii ambayo leo Waheshimiwa Wabunge tumesimama hapa kuwaomba waipitishe ili tuweze kuyatekeleza yale yote ambayo wameyachangia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara yetu hii tumepata michango ya Kamati zetu zote mbili pamoja na michango ya Wabunge takriban 20. Maoni yote ambayo yametolewa na Wabunge, ushauri wote ambao Waheshimiwa Wabunge wameutoa na kwa kweli maelekezo yote ambayo Bunge hili litayaridhia, chini ya uongozi wa Waziri wetu Mheshimiwa Engineer Masauni, tuwahakikishie kwamba tutakwenda kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuja Mheshimiwa Waziri kufanya majumuisho ya jumla kwenye maeneo mengi, lakini kwa fursa hii ninaomba niseme machache sana na kwa muda mfupi sana. Imezungumzwa hapa kwamba kwenye Dira yetu ya 2050 mazingira yamewekwa kama sehemu ya nguzo zile tatu. Ni bahati mbaya sana kwamba kwa sababu zile nguzo mbili zinaeleweka hazikuzungumzwa hapa. Sasa ili tuilete maana kamili ya nguzo ya tatu ni vyema tukajua zile nguzo mbili zimezungumza nini kwenye Dira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya kwanza ili kufikia malengo ya Dira yetu 2050 inazungumzia uchumi imara, jumuishi na shindani. Nguzo ya kwanza ambayo inazingatia uchumi unaokuwa kwa kasi, lakini uchumi unaobebwa na sekta binafsi. Nguzo ya pili, inazungumzia uwezo wa watu, uwezo wa Watanzania na maendeleo ya jamii ya Kitanzania. Jamii ambayo ina uwezo wa kupata afya bora, elimu bora na ujuzi kwa ajili ya kuendana na soko la ajira la dunia ya sasa na dunia hii tunayoizungumzia kwa miaka 25 ijayo sisi kama Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya tatu ndiyo hii ambayo tumezungumza sana Waheshimiwa Wabunge; uendelevu wa mazingira na ustahimilivu. Kwa nini nguzo hii imewekwa na waandishi wa Dira na tukakubaliana kama Taifa iwe sehemu ya nguzo tatu za Dira hii 2050? Imewekwa ili kusimamia rasilimali za Taifa kuhakikisha kwamba tunapotumia rasilimali zetu za Taifa tuzingatie kuzuia mabadiliko ya tabianchi. Sababu ya pili nguzo hii ya uendelevu wa mazingira na ustahimilivu imewekwa ili kuhakikisha matumizi endelevu ya mazingira na maendeleo ya sasa yasiathiri vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na niwasihi sana watupitishie bajeti hii ili tukayasimamie mazingira. Mheshimiwa Waziri wetu, Engineer Masauni tumeshakaa pamoja ndani ya Wizara na wataalam wote na tumekubaliana kwa dhamana hii tuliyopewa ya kitaifa ya kusimamia mazingira na Taifa letu kwa ajili ya vizazi vijavyo tutakwenda kuifanya kazi hii kuliko wakati mwingine wowote ambao umewahi kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni champion wa uhifadhi na uendelevu wa mazingira ndani ya Tanzania, Afrika Mashariki na duniani, amesaini Kitabu hiki cha Dira yetu ya 2050 mpaka tukafikia kuongelea habari ya zile nguzo tatu. Anataka nguzo hizi tatu zituelekeze kwenye uchumi wa dola trilioni moja, la kwanza; pia, zituelekeze kwenye kuwahudumia Watanzania ambao mwaka 2050 inakadiriwa tutakuwa tumefikia milioni 118. Siyo hivyo tu, anataka wakati huo ukifika tuwe uchumi wa juu wa pato la kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa, wakati akiuzungumzia Muungano na nitamnukuu. Amesema, “amani na umoja wa Taifa letu tunaouona kifungashio chake ni muungano.” Sasa, dira yetu hii na mambo yote yatakayoenda kufanyika, mipango yote ya maendeleo ambayo tutaipitisha kwa miaka 25 kutokea sasa, kifungashio chake ni mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii tutakwenda kuifanya kwa weledi na wivu mkubwa na kwa kweli, ninawahakikishia zitakuwepo kelele za hapa na pale. Kusimamia urithi, kwa ajili ya kizazi kijacho haitakuwa kazi ya kupigiana makofi. Tuko tayari kuzibeba lawama, lakini tutatanguliza kutoa elimu kwa Watanzania wote watuelewe na baada ya kutoa elimu tutakwenda kusimamia misingi ya sheria na taratibu ambazo tumejiwekea, kama Taifa, katika kuyasimamia mazingira ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda katika kipindi ambacho mazingira hayatakuwa a by the way thing, itakuwa ni jambo la kwanza kabla ya mtu kuwaza jambo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)