Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ametujalia kukutana leo hapa kwa mara nyingine tena tukiwa wazima wenye afya. Ninaomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, pamoja na Uongozi mzima wa Bunge letu kwa kuendesha mjadala wetu wa leo wa Bajeti hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa weledi mkubwa toka asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua fursa hii kuwapongeza sana na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Wapo waliobahatika kusema, lakini kwa sababu ya muda, nina hakika wameyawakilisha vyema mawazo ya wengi na wale ambao pia, walichangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja kuhusiana na Muungano. Ninajua hoja nyingi zimezungumzwa, ziko ambazo tunaweza tukazitolea ufafanuzi sasa hivi na ziko ambazo tutazichukua, kama maelekezo na kwenda kuzifanyia kazi. Ninawaahidi Waheshimiwa Wabunge, zile ambazo hatutaweza kuzitolea ufafanuzi leo, tutazitolea ufafanuzi kwa maandishi. Vilevile, maoni yao yote mazuri na muhimu sana tutayafanyia kazi na tunayachukulia kwa uzito mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Muungano, ninaomba nianze na hoja moja ya msingi sana ambayo baadhi ya wachangiaji, ninadhani mchangiaji mmoja, alizungumza. Kuna wachangiaji wengi walizungumza, lakini ninaanzia pale ambapo mchangiaji mmoja alizungumza kuhusiana na zilizokuwa zinaitwa Kero za Muungano, ambapo sasa sisi tunaziita Hoja za Muungano. Akaeleza kwamba kutokufanyiwa kazi kwa kero hizo ni moja ya sababu ya kuudhoofisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikubaliane naye kwamba, moja kati ya mambo ambayo yamevunja miungano ya baadhi ya nchi duniani, ikiwemo katika Bara la Afrika ambapo nchi nyingi sana zilijaribu kuungana, lakini hazikufanikiwa na hazikufika tulipofika, sisi leo tunaadhimisha miaka 62. Miongoni mwa sababu, moja, ilikuwa ni hiyo, zipo sababu nyingi, kwa mfano; kuna nchi ziliungana hazina mahusiano yoyote ya kihistoria, tofauti na sisi. Sisi historia ya pande hizi mbili za Muungano haikuanzia leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya pande mbili za Muungano wa watu wa nchi hii ya Tanzania wanaotokea upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara inaanzia hata kabla ya wageni hawajaja katika nchi hizi. Vilevile, historia yao inaendelea wakati wa ukoloni, lakini historia hiyo imeendelea vilevile kipindi cha mapambano dhidi ya ukoloni na hata wakati wa utumwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa hiyo utakumbuka kwamba, pande hizi za Muungano wakati zinapambania ukombozi wa nchi hii, Waafrika ambao walikuwa wakinyanyaswa katika nchi hizi waliunganisha nguvu na kuunda vyama vya siasa. Mnamo Mwaka 1929 Chama cha African Association cha iliyokuwa Tanganyika kiliundwa na hicho ndicho kilichosababisha mwaka 1954 kuundwa kwa TANU, chama kilichosimamia na kuongoza mapambano ya ukombozi wa iliyokuwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar, mnamo mwaka 1934 Chama cha African Association kimeundwa na ndicho kilichosababisha kuundwa kwa Chama cha Afro Shiraz Party mwaka 1957. Chama hicho ndicho kilichosimamia ukombozi wa nchi hii kwa hiyo, ushirikiano wa vyama hivi vya Waafrika unathibitisha mahusiano yaliyopo kipindi cha wakati wa ukombozi wa nchi hizi na hata pale ambapo vuguvugu la ukombozi, kupitia PAFMECA, mwaka 1958 ambapo Mzee Karume na Mwalimu Nyerere waliongoza mapambano hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu suala la kihistoria hata suala la kijiografia; ninapongeza sana, kuna wachangiaji waliozungumza kwamba, Muungano huu ni urasimishaji uliofanywa na Mwalimu Nyerere wa kuwarudisha pamoja watu wa nchi hizi mbili ambao walikuwa pamoja toka karne na karne na kukataa mipaka ya mabeberu iliyowekwa na kuwagawa Waafrika kwa mipaka, pale Berlin, katika Karne ya 19. Kwa hiyo, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume waligoma mipaka ya wakoloni wakaamua kutengeneza na kusimamia mipaka yetu wenyewe Waafrika, ambayo mpaka leo inadumu. Hata Mwaka 1886 wakati ambapo mamlaka ya Sultan ilirasimishiwa mipaka mipya ambayo leo hii tunaiona ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sababu zipo nyingi. Hata sababu ya matarajio, iko miungano iliyovunjika kwa sababu, matarajio ya wananchi hayakutimizwa; sisi matarajio hapa yametimia. Moja katika matarajio makubwa, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliozungumzia kuhusu umuhimu wa amani, utulivu na umoja wa nchi yetu, kama ndiyo msingi mkubwa wa Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio ya wananchi wa nchi hii ni kuendelea kuishi katika amani, umoja, mshikamano na maendeleo, lakini vilevile hata matarajio ya ugawanaji wa madaraka. Hii inadhihirishwa na Baraza la Kwanza la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mara baada ya kuungana. Wako watu wanasema kwamba, nchi hii mbali na kuungana leo wanataka kutugawa tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alithibitisha hilo hata katika uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri la kwanza. Kulikuwa kuna Wizara tano ambazo Mawaziri wake walikuwa ni kutoka Zanzibar na Wizara hizo wala hazikuwa za Muungano. Kwa mfano; Wizara ya Viwanda, Madini na Nishati, Waziri wake alikuwa Kassim Hanga; Wizara ya Sheria na Katiba, Mzee Hassan Nassor Moyo; Wizara ya Habari na Utalii alikuwa Idris Abdul Wakil; Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi; Wizara ya Biashara na Uchumi, Abdulrahman Babu. Kati ya Mawaziri 23 aliamua kwa makusudi kuonyesha kwamba, nchi hii ni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kitendo cha Zanzibar kuondoa sovereignty yake na kusainiwa Mkataba wa Muungano Taifa hili limeendelea kubaki kuwa moja na leo hii tunashuhudia Muungano wetu ukiendelea kudumu. Ukiachilia mbali masuala ya utamaduni ambao utamaduni wetu wananchi wa pande hizi mbili unafanana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikirudi katika hoja ya msingi, nimeona niyagusie hayo, lakini hoja ya msingi ambayo ninataka niigusie ni kuhusiana na zilizoitwa kero. Ninaomba nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, Wahenga wanasema; mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Ninaona watu wengi wanatofautiana sasa hivi juu ya msemo huo wa wahenga, wanasema mnyonge asinyongwe na ni kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameweza kuondoa kero 11 katika kipindi chake. Leo hii tunavyozungumza kati ya kero 25 tumebakiwa na hoja tatu peke yake. Leo ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walio wengi, wamelitambua na kulithamini hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii kuwaeleza ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wananisikia kwamba, haya siyo mafanikio madogo, ni mafanikio makubwa sana, ni mafanikio ambayo tunahitaji tujivunie na ni mafanikio ambayo yamewezesha kufanya Muungano wetu uwe imara zaidi. Waheshimiwa Wabunge, katika kero tatu zilizobaki, kero mbili tunatarajia kuzimaliza muda siyo mrefu na moja iko chini ya mamlaka yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili hili panapo majaaliwa tunataka tuwasilishe mabadiliko madogo ya sheria kuimaliza kero moja kati ya hizo zilizobaki. Kero hii ni ambayo inahusu usajili wa vyombo vya moto; tunatarajia, Waheshimiwa Wabunge wakiridhia na nina uhakika wataridhia kwa sababu wao watu ambao wanaamini kabisa juu ya dhamira ya dhati ya kuondoa hoja hizi, ili tuweze kuimarisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hoja nyingine moja na yenyewe tunatarajia katika kikao kijacho kitakachofanyika siku ya Tarehe 25, cha Kamati ya Pamoja ya Fedha, kwenda kuimaliza. Hivyo, kwa kipindi hiki tutakuwa tumemaliza kero 24 kati ya kero 25. Hayo siyo mafanikio madogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero moja ambayo imezungumzwa inahusu masuala ya kifedha, ikiwemo masuala ya mgao wa hisa za iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambayo kuna madai kwamba, Zanzibar ilichangia hisa kwenye Benki ya Tanzania wakati wa uanzishwaji wake. Hivyo hoja iliyopo ni kwamba, mgao huo uzingatie hisa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii pamoja na Mfuko wa Pamoja wa Fedha, hoja hizi za kifedha zinahitaji umakini na utulivu wa hali ya juu. Hata hivyo, Waheshimiwa Wabunge, ikiwa Mama Samia ameweza kupunguza hoja 11 na hizi mbili tunatarajia kuzimaliza kwa kipindi cha miaka mitano ni imani yangu na hii moja itamalizika. Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana leo hii tumezungumza kwamba, sasa tunakwenda kufanya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Kamati kuwa, sasa siyo Wizara tena ya kuzungumzia hoja za Muungano, ni Wizara ya kuzungumzia fursa za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wetu wa kuelekea kwenye fursa, ambazo ziko nyingi, bahati mbaya sana fursa hizi ambazo wananchi wa pande mbili wameendelea kufaidika nazo zimekuwa hazizungumzwi sana. Wakati umefika sasa wa kufanya kila linalowezekana, ili elimu hii iweze kufika kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo tumekuja na mpango kabambe wa elimu kwa umma kuhusu Muungano. Ninaomba tushukuru Bunge lako Tukufu kwa kuridhia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuweza kuja kutoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge tunawashukuru sana, maoni yao mazuri waliyotoa pamoja na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, tutayazingatia. Tunaamini semina hii imeleta utofauti hata miongoni mwa Wabunge na kuongeza uelewa juu ya masuala mbalimbali ya Muungano, ikiwemo fursa zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, mkakati huu unalenga katika mambo mengi. Tunajua kuna changamoto kubwa ya uelewa, hususan kwa vijana, kuhusu masuala ya Muungano. Hivyo, moja katika mkakati wetu huu kabambe utagusa maeneo ambayo yanawagusa vijana ili vijana hawa tuweze kuwarithisha Muungano wetu, waweze kuulinda Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo yanagusa vijana moja ni eneo la elimu. Ndiyo maana leo hii ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kutoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kuingiza masomo ya Muungano katika mitaala. Ninataka niwajulishe katika hilo tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaeleza baadaye eneo la mitaala, lakini ninaomba nigusie kwenye mkakati huu kabambe. Moja ni suala la midahalo, semina, makongamano na mashindano mbalimbali yakiwemo ya insha, kupitia kwenye shule zetu, vyuo vyetu na kadhalika kupitia mitandao ya kijamii. Maeneo ambayo vijana wanayatumia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, kuingia katika mitandao ya kijamii ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais. Huko wataweza kujionea shughuli mbalimbali na kupata taarifa kuhusu Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika bajeti hii ni tumetenga fedha, kwa ajili ya kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, ambayo ameitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa kuanzisha makavazi. Hivi tunavyozungumza tumekamilisha ujenzi wa jengo letu lililopo Mtumba, ambapo tutakuwa tuna makavazi ya muda, lakini katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha, kwa ajili ya kujenga makavazi hapa Dodoma pamoja na Zanzibar. Tunaamini kwamba, makavazi hizi zitakapokamilika zitasaidia sana kuhifadhi nyaraka mbalimbali zitakazosaidia vijana wetu kupata taaluma mbalimbali kuhusiana na Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba, elimu hii kwa umma inafika kupitia mkakati wetu huu, vilevile kuna matamasha mbalimbali tunafanya. Kwa mfano, ninaomba kuchukua fursa hii kuwajulisha na kuwaalika Waheshimiwa Wabunge, siku ya tarehe 26 tutakuwa tuna tamasha la aina yake la Mtanzania, pale Dar es Salaam. Leo hii tunapozungumza, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, tunazindua Ligi ya Muungano ambayo inafanyika pale Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, siku ya tarehe 3 tunatarajia kuzindua Msafara wa Muungano (Muungano Caravan) ambao utapita katika Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania kufikisha elimu kwa wananchi wetu, hasa vijana kwa utaratibu ambao utakuwa ni kivutio kwa watu kuhamasika na kuwa na hamu ya kusikiliza. Waheshimiwa Wabunge siku ya tarehe 3 tutazindua mpango huo wa Muungano Caravan Dar es Salaam na itakuwa ni siku ya Jumapili; tunaomba sana ushiriki wa Wabunge, wao ni watu muhimu sana katika kudumisha Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda sitagusia maeneo mengine ambayo yanagusa watu wa aina nyingine, mikakati kwenye eneo la viongozi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa baada ya maelezo hayo kuhusu Muungano niende kwenye eneo la mazingira. Ninataka nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge juu ya changamoto ambazo wamezieleza kwamba, bado zinasumbua katika nchi yetu kuhusiana na mazingira. Kwa mfano, bado kumekuwa na ukataji miti hovyo, tunakiri juu ya hilo. Tunakiri bado majiji yetu siyo masafi, lazima tukiri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakiri bado kuna uharibifu kwenye vyanzo vyetu vya maji, bado kuna viumbe vamizi, lakini bado kuna kelele zitokanazo na shughuli mbalimbali kwenye makazi ya watu na mambo mengine mengi, sisemi kwamba hakuna kazi iliyofanyika, nimeeleza kwenye hotuba yangu mafanikio ya hatua ambazo zimechukuliwa, lakini kama kweli tunataka tufikie Dira ya Miaka 50 ambayo imeweka suala la uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa tabianchi kama moja kati ya nguzo muhimu pamoja na maelekezo yaliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ni lazima tufanye mabadiliko makubwa katika eneo zima la usimamizi wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Mheshimiwa Naibu Waziri, kuwahakikishia Wabunge kwamba tunatarajia bajeti hii itakapokuwa imepita na yale yote ambayo tumedhamiria kuyafanya mengine nimeyaeleza hapa, tunakwenda kukabiliana na changamoto hizi na uwezo wa kudhibiti na kuzimaliza changamoto hizi tunao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza na la muhimu sana ambalo ninaomba Waheshimiwa Wabunge walifahamu, kwamba tumeamua kuja na mpango mkakati, kabambe wa mageuzi ya kimkakati ya mazingira endelevu na tumeitengea bajeti tayari katika bajeti ya mwaka huu kwa kuanzia ni shilingi bilioni 3.5 na mpango huu tunatarajia tuuzindue siku ya mazingira Tarehe 5 Juni ambapo utahusisha maeneo kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika maeneo ambayo mpango huu unakwenda ku-address ni suala la kuhakikisha kwamba tunaikijanisha nchi yetu, kwamba tunakwenda kuhakikisha kwamba tunapanda miti na siyo kuipanda miti tu, lakini hata kuilinda na kuitunza. Mpango huu unakwenda kutoa majawabu juu ya baadhi ya kero zilizopo kwa Waheshimiwa Wabunge kwenye Majimbo yenu kuhusu viumbe vamizi. Mpango huu unakwenda kutoa majawabu katika masuala ya usafi na urejezwaji wa taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taka zinazozolewa hizi ni bidhaa, wakati umefika tuwe na mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba taka hizi tunazitumia vizuri kuzalisha products zenye tija kwa ustawi wa wananchi wetu. Mkakati huu unakwenda vilevile ku-address suala la urejeshaji wa ardhi pamoja na ardhi oevu bila kusahau biashara ya kaboni. Ili hayo yafanyike ni lazima tuwe na nyenzo, nyenzo zetu kuu ni taasisi zetu mbili, Taasisi ya Baraza la Hifadhi na Mazingira Tanzania (NEMC), pamoja na Kituo chetu cha Kuratibu Biashara ya Kaboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kukuhakikishia kwamba maoni ya Wabunge ni ya msingi kuhusu namna ambavyo tutafanya kuisaidia NEMC iweze kutimiza majukumu yake vizuri, ndiyo maana tunaamua kufanya, kuliangalia suala la NEMC kwa mapana zaidi si katika eneo moja la sheria peke yake tunataka NEMC iwe ni chombo ambacho kinaweza kufanya kazi ya enforcement kwa wale wote ambao wanakiuka sheria za nchi yetu na ziwe na nguvu, uwezo, meno na makucha ya kusimamia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusingependelea kufanya kazi zetu kwa kuzima moto kwamba leo Waziri kaenda kafanya ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda kimoja, mpango huu unakwenda kutupatia ufumbuzi wa kudumu. Kwa hiyo ni Mpango ambao unataka tuifanye NEMC iwe ya kisayansi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ninakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kwamba wakati umefika sasa NEMC kuwa Mamlaka, jambo hilo haliepukiki. Waheshimiwa Wabunge katika Bunge hili Tukufu niliwahi kutoa ahadi hiyo na bahati nzuri Dkt. Samia Suluhu Hassan amenirudisha katika Wizara hii, ninataka kuwahakikishia, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na Mwanasheria Mkuu ananisikiliza, Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa, Chief Whip yupo hapa, tunatarajia katika Bunge lijalo Mungu akipenda tuweze kuleta hapa sheria ya kuifanya NEMC iweze kuwa mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zote muhimu za kiserikali tumeshazifika, kwa hiyo kiu ya Waheshimiwa Wabunge ya kuifanya NEMC kuwa Mamlaka sasa inaenda kupata ufumbuzi muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuifanya NEMC kuwa Mamlaka haitoshi, lazima tuiangalie NEMC juu ya mambo mengi mbalimbali. Kwa mfano, NEMC inahitaji kuwa na vitendeakazi vya kisasa ili iweze kutekeleza majukumu yake vizuri, tumejitahidi kwenye bajeti hii kuiwezesha NEMC kupata magari, tumejitahidi katika bajeti hii kuhakikisha kwamba mbali ya mipango mingine ya upatikanaji wa fedha kupitia kwenye miradi mbalimbali ambayo tunaisimamia, kuweza kuwa na mifumo na mitambo ya kisasa ambayo inaweza kuifanya NEMC ipate taarifa in real time, kwamba mahali popote ambapo kuna uchafuzi wa mazingira na ukiukwaji wa sheria, NEMC aweze kupata taarifa hapohapo na siyo kukimbizana, mifumo hii tayari ipo katika hatua za mwisho kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii tunatarajia kuanza, tunayo mahitaji ya drone karibu 13, tunaanza na drones mbili, pia malengo yetu, NEMC tunataka kuipatia helicopter, tuipatie na boti, tuwapatie wafanyakazi na watendaji wenye uwezo wa kutosha kusimamia shughuli za mazingira, tukiyatimiza hayo hakuna sababu katika nchi hii kuona kuna mtu yeyote anakiuka Sheria za Mazingira, hakuna sababu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Majiji yetu yatakuwa masafi kama yalivyo majiji mengine nchi zilizoendelea, hakuna mtu atapigiwa kelele katika mitaa, hakuna uharibifu wa vyanzo vya maji, hakuna changamoto yoyote inaweza itajitokeza. Kwa hiyo, ninataka kuwahakikishia, hayo mambo wanaweza wakaona ni magumu, lakini ni mambo ambayo yanawezekana na yanatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la watumishi tumeanza katika bajeti hii, tumepata vibali vya watumishi zaidi ya 103, si hatua ndogo. Ninajua bado mahitaji ni makubwa lakini si haba! Hata majengo ya ofisi, juzi nilikwenda kutembelea Jengo la NEMC – Geita, si ofisi tu ya NEMC, ni kituo cha umahiri. Tunataka Ofisi za Kanda zote 13 za NEMC ziwe vituo vya kimahiri, kama ilivyo Kituo cha Geita ambayo changamoto iliyopo katika Kituo cha Geita kuhusiana na uchafuzi wa mazingira ya wachimbaji madini wanaotumia zebaki, tunaweka kituo ambacho kitafanya research na kutafuta njia mbadala kwa wachimbaji wetu wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa pia ni sehemu ya kuweza kutoa elimu ya madhara ya matumizi ya kemikali hizo zenye athari na afya na mazingira. Kwa hiyo, lengo letu ni kwamba vituo kama kilichokuwepo Geita ambacho tunatarajia kukizindua hivi karibuni, viwe katika Kanda zote. Tukifanikiwa kuifanya NEMC ikaweza kusimama kisheria, kitaasisi, tutaweza kuwa na chombo imara kabisa ambacho kitatusaidia sana kabisa, kukabiliana na changamoto ya mazingira ambayo Wabunge mmeipigia kelele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyenzo yetu nyingine ni Kituo cha kuratibu biashara ya kaboni. Wabunge wamezungumza kwa uchungu na ninakubaliana na wao kwamba, eneo la fursa ya biashara ya kaboni bado hatujalitumia ipasavyo. Bahati nzuri Taifa letu lina fursa nyingi sana ambazo hazijatumika na bahati mbaya ni kwamba fursa hizi hazisimami, kadri ya dunia inavyokwenda mbele, inawezekana, kwa mfano, kama sasa hivi kuna teknolojia za kufyonza hewa ukaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea wakati teknolojia hizi zikisambaa, hakutakuwa na mtu anahitaji misitu yako iliyokaa haina kazi yoyote, kwa hiyo ni lazima tuchukue hatua sasa hivi. Nami ninataka kuwapongeza Wabunge, kwenye Bunge la Mwezi Machi mwaka jana, tulipitisha Sheria ya kukitambua rasmi kituo hiki, tunashukuru sana na jambo hilo limesaidia sana. Hata katika bajeti hii, tutafanya kazi kubwa sana ya kukiimarisha kituo chetu na tunataka bishara ya kaboni iwe ni katika vyanzo vitatu vikubwa vya mapato vya nchi, hayo ndiyo malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kituo chetu cha NCMC Tanzania kiwe kituo cha mfano Afrika. Hayo ndiyo malengo na dhamira yetu tunataka kituo hiki kitengeneze Dola bilioni mbili kwa mwaka. Hayo ndiyo malengo, Wabunge wanaweza wakaona ni malengo ambayo ni very ambitious, malengo ambayo ni ya kufikirika, lakini ni malengo ambayo yanawezekana kwa sababu fursa hizo zipo nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike ili tuweze kutimiza malengo hayo. Jambo la kwanza nimeeleza kwamba sasa tuna kituo na hata watu wa nchi nyingine wanakuja kujifunza hapa kwa mfumo ambao tumeuanzisha sisi. Jambo la pili ambalo baadhi yao wamezungumza ni kuhakikisha kwamba tunazitumia fursa zote, iwe kwenye misitu, kilimo, taka, madini, miundombinu, usafirishaji na kwenye sekta zote tutumie fursa zilizopo kwenye biashara ya kaboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ziko baadhi ya Wilaya wameshaanza kufanya biashara ya kaboni, lakini haturidhiki juu ya utaratibu uliopo sasa. Tunaamini kabisa kwamba tutaweza kupata fedha nyingi zaidi ikiwa tutaimarisha mifumo yetu ya Registry na MRV kwa ajili ya kuhakikisha biashara hii inakuwa ya uwazi na kwamba bei ya kaboni popote duniani, ndiyo bei hiyo hiyo mwananchi wa kwenye halmashauri yoyote anaipata moja kwa moja. Ndiyo maana tumepata shilingi bilioni tano katika bajeti hii kwa ajili ya kuimarisha mifumo hii. Kwa hiyo sasa, dhuluma kwa wananchi wa nchi hii inakwenda kukoma muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kama nilivyoeleza kwenye NEMC, NCMC inahitaji wataalam, inahitaji training, hayo ni miongoni mwa mambo tumeyapa kipaumbele katika bajeti yetu ya mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, ninaomba uridhie nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wameziuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika hoja ambazo ziliwasilishwa ambayo ninaona ni vizuri nikaitolea ufafanuzi, ni kuhusu sekta ya uchumi wa buluu. Kuna hoja kwamba tumeanzisha Kitengo cha Uchumi wa Buluu mwaka jana kuweza kuratibu na kuwezesha wananchi wanaohitaji kujishughulisha na uchumi wa buluu, wanufaike na uanzishwaji wa kitengo hicho. Hii ilikuwa ni hoja ya Kamati ya kwamba, Kamati inaona kuna haja ya kutuwezesha kituo hicho kifedha na kirasilimali ili kiweze kuwasaidia wananchi wa pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri huu umepokelewa. Aidha, Serikali zote mbili zimeendelea kushirikiana katika masuala ya uchumi wa buluu na tayari maeneo ya ushirikiano yameainishwa ikiwemo kuandaa miradi ya pamoja na kuandaa Marine Special Plan, mpango wa matumizi endelevu ya rasilimali ya maji, elimu kwa umma na mikataba ya kimataifa ambayo itanufaisha wananchi wa pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ninaomba kuwashukuru sana Mawaziri ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Wizara zenye mnasaba na uchumi wa buluu. Hivi karibuni mpango huu sasa unakwenda kupanga mifumo yetu kwa kuanzia ya bahari vyema ili kuepusha mgongano uliopo kati ya sekta moja na sekta nyingine, kwamba tuwe na maeneo tunajua kabisa, haya ni maeneo kwa ajili ya burudani na utalii, haya ni maeneo kwa ajili ya uvuvi, haya ni maeneo kwa ajili ya uchimbaji gesi na mafuta na kadhalika na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo tumeutengea bajeti mwaka huu kwa mara ya kwanza na tunakwenda kuanza utekelezaji wake, ni hatua moja kubwa sana na ni hatua ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kuhusiana na suala lile ambalo nilisema nitalizungumza baadaye kuhusiana na kushirikiana na Wizara za Elimu kuweka suala la Muungano kwenye mitaala ya elimu na kuweka mashuleni elimu ya Muungano ili udumu vizazi na vizazi. Ushauri huu umepokelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, majadiliano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu masuala ya Muungano kuingizwa kwenye mtaala wa elimu nchini, yanaendelea kufanyika na kwa kuanzisha kitabu cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ‘Chimbuko, Misingi na Maendeleo’, kitabu chenyewe hiki hapa, tutafanya jitihada Waheshimiwa Wabunge wakipate hiki kitabu ni kizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu hiki kimepata ithibati na kitatumika kama kitabu cha ziada katika shule za sekondari Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo, wataalam wanaendelea na utaratibu wa kurudufu kitabu hicho kwa ajili ya kukisambaza pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ninaomba kuitolea ufafanuzi, ni kuhusiana na ujenzi wa Ofisi za Muungano Zanzibar. Ushauri huu umepokelewa, aidha, taasisi 21 kati ya 33 zilizo na ofisi Zanzibar, zina majengo yenye hadhi na ni ya kudumu hivyo Serikali itaendelea kuzihimiza taasisi zilizopanga ofisi kujenga ofisi zao Zanzibar. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, malizia kuhitimisha hoja yako.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ufafanuzi mwingine tuweze kuwasilisha kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)