Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kunipa fursa ili na mimi niweze kuweka mchango wangu katika kuunga mkono pongezi nyingi za dhati na za upendo sana kwa vijana wetu na watoto wetu wa timu ya Serengeti Boys. Timu ya watoto chini ya miaka 17 ambao kwa kweli wameitangaza Tanzania. Dunia nzima jana imeijua Tanzania. Tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo haya yametokana na juhudi na jitihada na utayari wa Serikali katika kuwekeza katika sekta ya michezo. Ametangulia kusema hapa mzungumzaji aliyetangulia kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluh Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa na utayari wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanja, vilevile amewekeza katika ujenzi wa akademia za michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa tunaona watu wanapiga kelele kwa nini tusilee vipaji vya watoto tangu wakiwa wadogo. Ndani ya miaka mitano ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefunguliwa akademia ya michezo pale Kigamboni, imefunguliwa akademia ya michezo pale Tanga, na zinafunguliwa akademia za michezo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Zinalea vipaji vya watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Samia Suluh Hassan ameweka miundombinu ya kulea vipaji vya watoto hadi shuleni. Watoto wa miaka 17 ni watoto walioko shuleni, lakini sasa kwa miundombinu na kwa nyenzo ambazo ameziweka Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari wameshajua kwamba wanalo soko la ajira la wazi kabisa katika mpira wa miguu. Tunaipongeza sana Serikali na tunawapongeza sana viongozi wote wa Wizara wakiongozwa na ndugu yangu Paul Makonda kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameifanya katika kuhakikisha kuwa jambo hili linatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza wenzangu, vijana hawa baada ya hapa sisi kama Taifa tunakwenda kuwatunuku nini kwa jambo kubwa walilofanya la kuitangaza nchi yetu? Hii timu inaitwa Serengeti Boys. Imeitwa Serengeti kwa lengo la kuitangaza mbuga yetu ya Serengeti. Je, Wizara ya Maliasili na Utalii na Serengeti National Park yenyewe wanajua kwamba vijana hao wameitangaza Serengeti? Na je, wamejiandaa vipi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba angalau wanawapa nyenzo ya kuendelea kuwatia moyo na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuitangaza nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai, pamoja na pongezi nyingi tunazotoa, lakini kama Taifa lazima tukubali kwamba vijana hawa wametuwakilisha vizuri. Wapewe zawadi kwa kuitangaza nchi yetu, na katika michuano mingine tuone kuwa kwenye jezi zao zinaendana na jina la Serengeti.
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: ... jezi zao ziwekwe nembo ya Serengeti.
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: ... Serengeti wawajibike kusaidia vijana hawa na waendelee kufanya vizuri na kuendelea kuitangaza nchi yetu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa...
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ninawatakia heri sana. Soko lao la ajira limeonekana. Tumeona ma-agent wengi wa michezo wanawasifia. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Sekiboko.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna imani watapata ajira kimataifa na sisi tuwe tayari kuwasaidia. Ninashukuru sana. (Makofi)