Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuweka mchango wangu katika azimio hili ambalo liko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kujua Taifa waangalie vijana wake leo. Leo vijana wetu hawa Serengeti Boys under 17 wamethibitisha kwamba vijana ndiyo wanaotoa dira ya Taifa. Katika sekta ya michezo tunakwenda kuona michezo inaenda kufunguka kupitia vijana hawa. Kupitia vijana hawa, vijana wa shuleni na vijana wa mtaani wameona kumbe inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo unasema ukiona mtoto yuko juu jua kuna mkono chini umembeba. Ushindi huu haujaja kwa bahati mbaya. Ushindi huu umekuja kwa sababu tuna kiongozi mwenye maono, tuna kiongozi shupavu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi wote ni mashahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais tangu ameingia madarakani tumeona mchango wake mkubwa katika sekta ya michezo. Kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais ameenda kuheshimisha sekta ya michezo, kuwaheshimisha wanamichezo na pia kutoa thamani katika wanamichezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mara nyingi tumemuona Mheshimiwa Rais hata akitoa ndege kuwafuata wachezaji na tunaona hamasa kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais. Yote haya yameleta leo tunaona manufaa kwa vijana wetu hawa. Sisi Watanzania tujivunie sana kitu ambacho kimefanywa na vijana wetu hawa. Wameongea wazungumzaji Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli Tanzania imeenda kwenye ramani ya dunia hata kwenye sekta ya michezo na sisi Tanzania tunasomeka tunafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutumie nafasi hii kupitia vijana wetu hawa ambao wameenda kuitangaza Tanzania, kupitia vijana wetu hawa ambao wamefuzu kushiriki fainali za AFCON na fainali hizi tunaamini kupitia maombi ya Watanzania na hapa niwaombe Watanzania tuungane kwa pamoja kuwaombea dua vijana wetu hawa. Tuwaombee sala vijana wetu hawa ili ushindi uwe kwetu na ushindi utakapokuja kwetu Tanzania ikatangazwe kimataifa zaidi na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo tumeliona hapa. Tumeona uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali na hapa Mheshimiwa Waziri siwezi kuacha kukupongeza, hakika kazi imepata mtu. Tunaona hekaheka zako kwenye sekta hii ya michezo, kazi unaiweza, unaifanya vizuri. Tunaamini vijana hao watakaporudi Mheshimiwa Waziri utafanya jambo kubwa kwa ajili yao. Hatuna mashaka na wewe. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia pongezi hizi ni za kwetu Watanzania wote, lakini zikiongozwa na Mheshimiwa Rais, mwanamichezo namba moja. Tunawapongeza sana vijana wetu under 17. Mungu awabariki sana kwa kuitangaza Tanzania kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)