Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kunipa nafasi hii na mimi nitumie kuwapongeza sana timu yetu ya Serengeti Boys kwa kufuzu mashindano ya AFCON na kuweza kushiriki katika Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 wa kiume. Tuna maneno tunasema kila kinachong'ara na kupendeza kimegharimiwa. Kwa hiyo, Serikali ninaipongeza sana kupitia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugharimia kuwekeza katika sekta hizi za michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu utatoa chachu kwa vijana wengine kushiriki katika michezo kwa sababu hapa timu yetu hii imeifanya sasa Tanzania kuendelea kutangazika zaidi duniani, pia inaonesha sasa namna Serikali na viongozi wake wanavyothamini michezo na wanavyothamini vijana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia ushindi huu wa AFCON vijana wengi watahamasika kuingia kwenye michezo kwa sababu sasa wanaona michezo inazidi kuwa ni ajira, michezo inazidi kuwa ni kipato kwao. Hapa tayari tuna mtaji wa timu zetu za Taifa, vilabu vyetu vikubwa kupata wachezaji bora ambao wataweza kushiriki hata kwenye vilabu vingine vya kimataifa. Kwa hiyo, hapa zitapatikana ajira za ndani, lakini na ajira za nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea sana kuwapongeza vijana wetu. Katika kuongezea, pongezi ziende kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake. Mheshimiwa Waziri na timu yako unafanya kazi kubwa sana kumsaidia Mheshimiwa Rais katika sekta hii ya michezo. Tunaomba taasisi zote zinazoshughulika na michezo ziendelee kuongeza juhudi zaidi katika kuwekeza zaidi kwenye michezo kwa ajili ya kuliinua Taifa kuwasaidia vijana wasiingie kwenye vitendo viovu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninashauri katika hili kuwe na namna fulani ambayo itaweza kusaidia Watanzania kwenda kushiriki kuwashangilia hao vijana wetu watakapocheza hizo fainali za Kombe la Dunia. Tuone namna ya unafuu wa kuwashirikisha wananchi na vijana wengine kwenda kuwa-support vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa kutumia fursa hii adhimu niweze pia kuwapongeza Tanzanite Queens, jamani timu yetu hii ya chini ya miaka 20 imefanya vizuri na wao wanaingia sasa kwenye Kombe la Dunia. Hapa tunaona uwekezaji mkubwa kwenye sekta hii ya michezo kwa vijana wa kike na kwa vijana wa kiume. Tunakwenda sambamba kuwawezesha na kuitangaza nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninatumia fursa hii kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)