Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mimi nimesimama kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuweza kuleta Azimio hili la kuipongeza Timu yetu ya Serengeti Boys. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwapongeza vijana wetu wa Serengeti Boys kwa kuweza kwa kweli kuingia fainali ya mashindano ya AFCON Under 17 lakini zaidi kuweza kushinda kwenda kushiriki kwenye World Cup. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuipongeza pia Menejimenti ya Wizara nzima ikiongozwa na Waziri na timu nzima ambayo imeenda kule kwa maana ya benchi na watu wote ambao wameshiriki kuhakikisha kwamba Serengeti Boys inafika pale ilipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na ushindi wa Serengeti Boys, lakini pia kwa kipindi hiki cha Awamu ya Sita tumeshuhudia michezo ikishika kasi kwa kasi kubwa sana ambapo timu zetu za football za wanawake; Tanzanite Queens wamesema hapa imeshinda kwenda Under 20 Women World Cup, pia tunayo Twiga inaenda kwenye WAFCON. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hapo tu, tumeona michezo ikikua kwenye riadha, netball na basketball. Tumeshuhudia timu yetu ya Dar City kwa mara ya kwanza kuweza kuingia kwenye robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Afrika imeandika historia. Haya yote kwa kweli yanatokana na maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ameamua kuwekeza kwa vitendo. (Makofi)
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Asha Baraka.
TAARIFA
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa taarifa kwa mchangiaji kwamba Tanzanite Queens inacheza World Cup mwezi Septemba mwaka huu na hapo hapo Twiga Stars itashiriki AFCON Julai mwaka huu, Morocco. Ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Esther Matiko, taarifa unaipokea?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu ulindwe nilikuwa nimeanza. Ninakushukuru dada yangu Mheshimiwa Asha. Nimesema hayo yote, nimewatambua Tanzanite Queens wanashiriki World Cup na Twiga wanashiriki WAFCON. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ni utashi mkubwa wa kisiasa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeshuhudia na hii ni dhahiri katika kipindi cha Awamu ya Sita kumekuwepo na maboresho kwenye miundombinu ya kimichezo kwenye viwanja mbalimbali ikiwepo ile ya Benjamin, tunaona tunajenga kule Arusha na hapa Dodoma, lakini pia maendeleo ya vijana kuweza kuibua vipaji mbalimbali na ndiyo maana leo tuko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni katika kuhakikisha kwamba Tanzania inafunguka kimataifa kupitia diplomasia ya kimichezo, ndiyo maana leo katika utashi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Taifa limekubali kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON ambapo tunawekeza mabilioni ya fedha kuweza kujenga miundombinu ya AFCON. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (MHE. JAMES K. MILLYA): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa James Millya.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (MHE. JAMES K. MILLYA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sana mzungumzaji anayeongea akaelewa pia kwamba michezo ni diplomasia na kwamba nchi yetu pamoja na kwamba vijana hawa wanacheza vizuri, lakini pia wanapeperusha bendera ya nchi yetu. Hivyo basi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tunatoa wito kwa balozi zetu zote duniani kwamba popote ambapo vijana hawa wanacheza Under 17, kwanza tunawapongeza, lakini wapokelewe na waandaliwe mazingira mazuri kwa sababu wanaandaa mazingira ya kupeperusha bendera yetu ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, pamoja na maneno mazuri ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaongea akumbuke kwamba jambo hili pia ni suala la diplomasia na kwamba Serikali inawaunga mkono sana vijana hawa na tuko tayari kuwapa msaada wa aina yoyote. Ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa James. Mheshimiwa Esther Matiko, Taarifa unaipokea?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu ulindwe. Ninaipokea na nimetaja hapa diplomasia ya kimichezo, Tanzania imefunguka kimataifa. Ninashukuru sana wanaonipa taarifa, lakini muda wangu ulindwe, dakika tatu ni ndogo sana. Kwa hiyo, naomba nianze maana yake hata sijamaliza wanani-interrupt sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther, taarifa ni sehemu ya mchango wako.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumesimama hapa kuwapongeza vijana wetu wa Serengeti Boys kwa kushinda penalty nne dhidi ya Egypt. Hii ni tafsiri kwamba ushindi wao siyo tu kwamba ni ushindi wa hayo magoli bali ni uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa vijana ambayo inaonesha dhahiri kwamba inaweza kugeuka kuwa heshima ya Taifa, kuwa uchumi wa michezo, ajira, lakini zaidi kuweza kuipa nguvu Tanzania ya soft power duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ni maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba anaunganisha michezo, utalii na uchumi wa Taifa. Sasa hivi ndugu zangu watu wengi kwenye utalii hawawekezi kwa wanyamapori tu. Mataifa makubwa yamejielekeza kwenye utalii wa kimichezo ambapo yanaamini kabisa kwamba yataleta watalii, wawekezaji, ajira na uchumi utaenda kukua sanjari kama tulivyosema hapa kuweza kuitangaza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serengeti Boys wanaitangaza Tanzania duniani, yaani watu duniani wanavutiwa kuangalia nchi yetu, wanatamani kuja Tanzania kupitia Serengeti Boys. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tunapotambua ushindi wa Serengeti Boys kuandika historia katika Taifa letu, tuweze kumpa kongole Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kwa utashi wake wa kisiasa kwa mambo mbalimbali, lakini ametamalaki kwenye michezo. Leo hata ligi zetu za Tanzania zinafahamika duniani, leo wachezaji mbalimbali ukiwaambia kuja kushiriki kwenye ligi ya mipira Tanzania wanakuja. Hii yote ni kwa sababu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo ameamini kupitia michezo anaenda kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Esther, hujaunga mkono hoja bado, unga mkono hoja.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo ninaunga mkono Azimio hili ambalo limeletwa hapa kuwapongeza vijana wetu wa Serengeti Boys na kwa kweli tuweze kuwapa zawadi. Tuwatafutie zawadi kama motisha ambayo itaweza kutoa morali kwa vijana wengi kuweza kushiriki kwenye sekta ya michezo. Ahsante sana. (Makofi)