Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) kwa Kufuzu Fainali za AFCON 2026 na Kukata Tiketi ya Kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri ya Miaka 17, Mwaka 2026

Hon. Paul Christian Makonda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) kwa Kufuzu Fainali za AFCON 2026 na Kukata Tiketi ya Kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri ya Miaka 17, Mwaka 2026

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa na mimi ninaungana na Bunge lako Tukufu kuunga mkono hoja nzito iliyotolewa na Mheshimiwa Ester Bulaya ikiwa ni kuwapongeza vijana wetu under 17 kwa historia waliyoiandika usiku wa jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada zake binafsi na mapenzi yake ya dhati kwa watoto wa Kitanzania na vipaji tulivyonavyo na kuamua kuichukua Tanzania na kuiweka kwenye ramani ya dunia katika michezo hii tunayoshuhudia leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika uwekezaji uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia katika michezo, morali aliyoiweka katika michezo inatutoa kimasomaso Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wote kwa pongezi walizompa na kwa kweli anastahili kwa kazi nzuri na njema aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirudi kwenye historia utakuja kuona namna ambavyo kipindi ambacho Taifa hili lilipigana vita na Uganda. Baada ya vita ya Uganda Wizara ya Michezo ilinyimwa hata shilingi 100 na kutokea pale Wizara hii ikaonekana ni ya michezo michezo tu. Rais pekee aliyeamua kuwekeza kwenye michezo hapana mwingine bila haya ninaweza kutaja ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi na utashi wake alioweza kuweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, uniruhusu pia niwapongeze sana sana kwa moyo wangu wa dhati TFF. TFF wanaosimamiwa na Baraza letu la Michezo (BMT) wanafanya kazi kubwa, kazi nzuri ya kuendelea kutambua na kukuza vipaji tulivyonavyo katika Taifa letu. Leo tunaposema Serengeti Boys watu wanafikiri labda ni vijana waliotoka kwenye mataifa tofauti na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu, vijana hawa Serengeti Boys ni matokeo ya UMISSETA. Ni matokeo ya watoto wa Tanzania, ni watoto wetu, ni vijana wetu waliopatikana kwa njia ya UMISSETA na wapo kwenye vituo vyetu ambavyo Serikali imewekeza kupitia TFF. Ukienda pale Tanga, ukienda pale Kigamboni na ukienda kwenye sports academy nyingi ambazo zimetengenezwa ndani ya nchi yetu zaidi ya 91. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu pia nimpongeze kocha. Kocha huyu ni mtoto wa Kitanzania aliyeibeba timu yetu ya Taifa na kuipa heshima ya kuingia kwenye fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu pia ninaomba uniruhusu nimpongeze kepteni, kijana mdogo aliyesimamia kijana wangu Kassim kuhakikisha kwamba timu inakwenda vizuri. (Makofi)

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninaomba uniruhusu nimpongeze golikipa wetu kijana mahiri, aliyefanya kazi nzuri. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Makonda, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro.

TAARIFA

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Waziri, Paul Christian Makonda kwamba hivi punde kocha wa Taifa Stars, Gamondi, amewachagua wachezaji wawili kati ya hawa ambao tunawasifia sasa kuingia kwenye Taifa Stars. Wachezaji hao waliochaguliwa ni Lukman Mbalasalu pamoja na Kassim Juma. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Makonda, Taarifa unaipokea?

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii ninaipokea kwa unyenyekevu mkubwa na kwa sababu kaka yangu alivyosikia tu jina huku limetajwa la kepteni akajua tayari mambo yameitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninampongeza sana golikipa wetu, kijana huyu Haji Ali amefanya kazi kubwa na kwa ujasiri mkubwa. Hakuogopa wala hakushangazwa na aina ya uwanja waliokuwa nao, lakini aliamua kusimama kuhakikisha kwamba analinda goli la Tanzania na kuhakikisha hakuna mtu anayefunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba uniruhusu nimalizie mambo mawili tu ya mwisho; la kwanza, Waheshimiwa Wabunge wametaka kujua baada ya hapa Serikali ina mpango gani? Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametupa maelekezo baada ya jana tu kuona matokeo. Matokeo haya ya mechi hii Mheshimiwa Rais mwenyewe ameifuatilia mwanzo-mwisho kwa sababu ni mapenzi yake kuona Taifa lake linapiga hatua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo yake amesema, vijana hawa wote walioonesha uwezo mkubwa na kuhakikisha kwamba wanaibeba bendera ya Taifa kwa kuitoa Egypt na kwenda Jumanne kucheza na timu ya Senegal watakapomaliza AFCON ya mwaka 2027, anataka vijana hawa wote wawekwe kambi kwa ajili ya maandalizi ya Tanzania kushiriki World Cup mwaka 2030. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matumaini yake ni kwamba vijana hawa ambao wameonesha uwezo na kwa kweli tunamuomba mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake juu ya Taifa letu kuhakikisha kwamba siku ya Jumanne tunabeba kombe na kuja hapa tukiwa washindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa kumalizia tu tunafahamu ya kwamba Bunge hili limeunga mkono Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia, nami ninaomba kutumia nafasi hii kuwaomba Wakuu wa Mikoa, siku ya Jumanne vijana hawa wa Serengeti Boys watakuwa wanacheza na timu ya Senegal. Basi kila mkoa kwa kuwaunga mkono tuweke screen kubwa kuangalia heshima inayojengwa na vijana wetu wa Kitanzania ikiwa ni sehemu ya kuweka hamasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja na kwa kweli tumepata…; Mheshimiwa Sanga amesema kuna wale mameneja uchwara, vijana hawa hawatakwenda kwa mameneja uchwara, vijana hawa wanaenda kwenye sport academy za kimataifa ikiwa katika mkakati wa kujenga heshima ya Taifa letu, maandalizi yetu ya kuingia World Cup 2030. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)