Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) kwa Kufuzu Fainali za AFCON 2026 na Kukata Tiketi ya Kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri ya Miaka 17, Mwaka 2026

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) kwa Kufuzu Fainali za AFCON 2026 na Kukata Tiketi ya Kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri ya Miaka 17, Mwaka 2026

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijahitimisha hoja yangu, ninaanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi kusimama mbele ya Bunge Tukufu kwa ajili ya kutoa hoja hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninamshukuru Mheshimiwa Spika wetu pamoja na Katibu wa Bunge na staff wote baada ya kuipokea hoja hii usiku na kunipa fursa mbali ya kwamba kuna shughuli inaendelea leo ya Wizara ya Ardhi, lakini kwa uzito, kwa heshima na kwa malengo ya Taifa letu katika diplomasia ya michezo, wameona wanipe nafasi hii niwasilishe Azimio hili ili tuweze kuipongeza timu yetu ya vijana under 17. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao hoja hii imechangiwa na takribani Waheshimiwa Wabunge saba, Mheshimiwa Festo Sanga, Mheshimiwa Sylivia Sigula, Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mheshimiwa Khadija Aboud, Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mheshimiwa Jafari Wambura Chege na Mheshimiwa Paul Christian Makonda. Ninawashukuru sana kwa michango yenu, ninashukuru sana kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea kwa ujumla, hoja hii ambayo nimeitoa; mosi, wengi wametambua mchango wa mwanamichezo namba moja Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya kwenye sekta ya michezo na imesababisha vijana wengi kuona kwamba michezo siyo suala la afya, siyo suala la kujifurahisha, lakini michezo ni ajira ambayo inawafanya vijana kujiajiri kupitia sekta ya michezo na kupata kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kupitia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ku-invest kwenye michezo, ni Mheshimiwa Mbunge wa term ya nne, tulikuwa tukizungumza masuala ya academy kwenye Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo iko Tanga, leo ipo Kigamboni. Tulikuwa tunazungumzia uwekezaji kwenye timu za vijana, leo vilabu vyetu wana timu za vijana. Tulizungumzia kurudisha michezo shuleni, leo michezo imerudi shuleni na matokeo yake hawa ni watoto wa kawaida kutoka kwenye mikoa mbalimbali, kutoka kwenye familia maskini kabisa ambaye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita imeamua ku-invest kwenye michezo. Mosi, wakijua zaidi ya 70% ya Taifa hili ni vijana ambao wameamua kushiriki kwenye michezo ili ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahitaji kuwatoa kina Cristian Ronaldo wengine kutoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anawataka kuwatoa akina Messi kutoka Tanzania, ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuwatoa kina Leo, kina Drogba kutoka Tanzania. Hii isingewezekana bila uwekezaji ambao umefanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ndugu zangu, michezo huunganisha Taifa, michezo huweka watu pamoja. Nami ninakushukuru Mheshimiwa Waziri, jana umetoka kumteua kaka yangu Haji Manara nami ninampongeza kuwa Msemaji wa Timu zetu za Taifa, ninaamini huko aliko ameanza kazi kuwaunganisha Watanzania, kuwaomba Watanzania wote tuungane, tui-support timu yetu ya Serengeti Boys ili Jumanne tuweze kuchukua kombe na tukawapokee kwa bashasha kubwa airport wakilileta heshima ya kombe hili nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kazi kubwa anayoifanya. Wizara yako ni Wizara ya hekaheka, upele umepata mkunaji, Mheshimiwa Dkt. Samia amejua kumpanga mchezaji kwenye Wizara ya Michezo ambaye anaifanya kazi kubwa na sisi tutakupa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, uwekezaji huu wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambao umesababisha si tu Serengeti Boys kuingia fainali na kufuzu michuano ya dunia mwaka huu, hivi tunavyozungumza Tanzanite Queens ya under 20 imefuzu kwenda kushiriki michuano ya dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza timu yetu ya wanawake ya Twiga Stars mwaka huu itashiriki michuano ya WAFCON. Huu ni uwekezaji na ushuhuda tosha ya kwamba vijana wameona kwenye michezo kuna ajira. Ninawaomba Watanzania, michezo ni heshima ya nchi, michezo inalitangaza Taifa letu si tu kwenye diplomasia ya michezo, lakini vilevile kwenye diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Wenger anaizungumza Tanzania, aki-post kwenye page yake tu watu wengi wataiona Serengeti Boys, lakini watajua kuna mbuga namba moja duniani iliyopewa tuzo inaitwa Serengeti. Tutaongeza watalii kupitia michezo, tutaongeza wawekezaji kupitia michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Watanzania, tuungane, tuipe support timu yetu vijana wetu waweze kufanya vizuri kwenye fainali, lakini vilevile waweze kufanya vizuri kwenye michuano inayokuja ya Kombe la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninachukua fursa kuipongeza Serikali, nimemsikia Mheshimiwa Waziri, wamesema wataandaa kambi mapema kwa ajili ya kuwaweka vijana hawa kuelekea kwenye michuano ya World Cup. Nami, kwa kumalizia, ninaamini Wizara ya Maliasili itakuwa imesikia, Serengeti itakuwa imesikia, vijana wameitangaza nchi, wametangaza utalii, wameitangaza Mbuga ya Serengeti, waseme jambo kwa vijana hawa ambao wameletea heshima kubwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi na baada ya kusema hayo, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliochangia. Ninaomba kutoa hoja. (Makofi)