Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Yahaya Esmail Nawanda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali yote ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, lakini pia ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ameyafanya katika Wizara hii ya Ardhi, ni kumteua kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Akwilapo pamoja na kaka yangu Mheshimiwa Mmuya kuongoza hii Wizara na kwa hakika wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika mchango wangu; Mkoa wa Mtwara na Lindi katika upimaji wa ardhi tuna jumla ya wakulima kwa Mkoa wa Mtwara peke yake wakulima 333,543 ambayo jumla ya korosho zote zinazolimwa, hawa ni wakulima wa korosho wana ekari 2,336,830. Hata hivyo, kwa Mkoa wa Lindi ambako anatoka Mheshimiwa Naibu Waziri pia kuna jumla ya wakulima wa korosho, pia wakulima kutoka Wilaya ya Ruangwa 127,260 hawa wote wana jumla ya ekari 1,221,922.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa hesabu inayofanyika leo hii, Mkoa wa Mtwara na Lindi mashamba yaliyopimwa ni 0.01% ya mashamba yote na kaka yangu Mheshimiwa Akwilapo, ukitaka kuacha legacy katika Wizara hii, twende tukapime mashamba ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara, Lindi na wananchi wa mikoa yote ambayo wanalima korosho, wanaolima pamba, wanaolima tumbaku, tuanze na kwenye korosho kama pilot study. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa korosho, ekari moja inaweza kupimwa kwa shilingi 80,000 na hii shilingi 80,000 kwa ekari hizo 2,336,000 tunaweza kupata jumla ya fedha shilingi bilioni 186. Serikali isitoe hata shilingi kwenye upimaji huu, sisi wenyewe wakulima wa korosho tutachangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunachotaka kitu kimoja tu hapa Mheshimiwa Waziri, tuanze na wilaya moja na mfano mzuri tuanze na Wilaya ya Newala, tuanze na Jimbo la Newala Vijijini. Sisi wananchi wa Newala Vijijini jumla ya ekari ambazo tunazo ni ekari 496,170. Tukizidisha mara shilingi 80,000, maana yake tutahitaji shilingi bilioni 39 kupima mashamba yetu yote, hizo fedha sisi tunazo. Hata hivyo, wewe umebarikiwa, una Kamishna Mkuu mzuri sana kaka yangu Mathew, anaweza kuifanya hii kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wenyewe wananchi tutachangia na tukiweza kuchangia kupima mashamba yetu yote, maana yake tunaenda kumsaidia mwananchi wa Mkoa wa Lindi, Mtwara na mikoa yote inayolima korosho. Kwanza watakuwa na ulinzi wa kisheria wa maeneo yao na urahisi wa kupata mikopo, pia thamani ya mashamba yao yanaenda kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, la mwisho uhamisho salama wa miliki zao, na hapa wewe ndiyo unaenda kutengeneza historia, tukianza kupima mashamba yote ya mikorosho, tutawasaidia wananchi kwanza kupata mortgage, lakini ile falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia ya Dira 2050 ya kila mwananchi ikifika ya mwaka 2050 apate dola za Marekani 7,000, sisi wananchi tunaolima mazao ya korosho, ninataka nikuambie tukipima mashamba yetu, tunahitaji miaka mitano tu kufikia this target. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninakuomba kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Akwilapo, unapokuja kuleta hitimisho, tuanze sasa kupima mashamba ya mikorosho ili tuwasaidie hawa wananchi, wamekaa na yale mashamba, lakini hayapimwi. Hata hivyo, na wewe una nguvu, kazi nzuri sana, una timu mzuri sana, na Mathew ambaye ni Kamishna Mkuu anaweza kuifanya hii kazi in a proper way na wala msianzie Masasi usije ukapata shida, twende tukaanzie Newala Vijijini. Nami nitahamasisha wananchi wangu wote na wameshakubali kila shamba ekari moja ikipimwa shilingi 80,000, kwa hakika tutapima ekari zote 400,000 tulizonazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, faida ya kupima haya mashamba ikoje, sisi tukishapima kuna kitu kinaitwa Certificate of Customary of Occupancy ambayo hizi ni hati zinazotolewa katika vijiji. Tukisema tu kila kijiji kimoja tuweze kutoa shilingi 5,000 tunaweza kupata shilingi bilioni 11 kwa mkoa mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake tunaweza kutengeneza matundu ya vyoo 6,400 bila kutegemea hela za Serikali, lakini kwa Newala Vijijini tunaweza kutengeneza matundu ya vyoo 1,378 bila kutegemea hela za Serikali sisi wenyewe na tunaweza kutengeneza madarasa 100 ambayo kwa miaka mitano naweza kujenga shule zote za msingi katika Jimbo langu la Newala Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri akija atuambie na atuletee mkakati mzuri wa kuhakikisha haya maeneo yanapimwa ili tuongeze thamani na tuwasaidie hawa wananchi wa korosho, wakiwemo wananchi kutoka Masasi na ikifanikiwa hivyo basi tutaenda kwenye mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ambalo ningependa kuchangia sasa ni muda muafaka wa kupima makao makuu ya halmashauri zetu especially hizi halmashauri kuu mpya. Sisi katika halmashauri yetu ya Newala Vijijini sasa Mji wa Kitangari na maeneo mengine yote tuletee mpango tukaanze kupima ili wananchi wale wasikae kiholela na faida za kupima yale maeneo zinajulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutatengeneza thamani ya miji yetu, lakini accessibility itakuwa nzuri, lakini kuwepo kwa huduma za kijamii. Sasa naomba unapokuja kuleta hitimisho basi utuletee mkakati wa kupima makao makuu za halmashauri mpya ili sasa hii miji ikatengenezwe vizuri, lakini ukianza na Newala Vijijini na Jimbo letu Newala Vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala pale Kitangari itafurahisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, Mheshimiwa Waziri mimi ningechangia kwenye concept moja ni nzuri sana ya Affordable Housing Act, tuanzishe huu mpango wa Affordable Housing Act itatusaidia sana NHC kupata fedha za kutosha kuanza kujenga nyumba katika halmashauri zote, kwa sababu tutaweka sheria, Serikali itatoa fedha, itatafuta vyanzo vya fedha na mwisho wa siku tutakuwa tumewasaidia wananchi na wafanyakazi especially vijana Gen Z. Tutakuja na mpango mzuri na mwisho wa siku tutawasaidia sana wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nikupongeze wewe binafsi kwa kazi nzuri na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)