Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Tarehe 01 Julai, 2026 Bunge hili ndiyo litakuwa Bunge la kwanza kushuhudia Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa ikianza kazi rasmi. Katika Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa kumeainishwa nguzo tisa ambazo zitaifanya Dira yetu itekelezeke na moja ya nguzo hizo ni sekta ya ujenzi pamoja na mali zisizohamishika ikimaanisha kwamba ni makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Dira yetu imeeleza kwamba kuna upungufu wa nyumba milioni 3.8 kwa mwaka huu na zinaendelea, upungufu huu unaendelea kukua kwa kila mwaka mpaka hapo tutakapofikia mwaka 2050.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka hapa tunapoongea sasa kwa bahati mbaya sana nchi yetu haina Sera ya Nyumba. Tuna Sera ya Ardhi lakini vilevile, kuna Sera ya Makazi ambazo zinatumika kama Sera ya Nyumba hapa na pale. Kwa bahati mbaya sana sasa ili Dira yetu iweze kutekelezeka kiufasaha na kwa umakini zaidi tunahitaji kuwa na Sera ya Nyumba ambayo hatuna mpaka sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere mwaka 1962 baada ya kupata uhuru alianzisha Shirika la Nyumba la Taifa kwa madhumuni ya kuchangia katika kuleta makazi ya bei rahisi kwa Watanzania, kwa sababu ndiyo tulikuwa tunatoka katika kupata uhuru, kwa hiyo watu wengi walikuwa hawana makazi mazuri na makazi rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kutumika kama ndiyo shirika linaloweza kutoa makazi haya. Baada ya muda kwenda mwaka 2005 Shirika la Nyumba la Taifa lililetewa sheria ambayo iliruhusu kujiendesha kibiashara. Kwa hiyo, tunavyoongea sasa hivi tuna gap, kuna gap au vacuum ya taasisi au upatikanaji wa nyumba hizi za bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu jukumu hili linaweza likachukuliwa, linachukuliwa na Shirika la Nyumba la Taifa peke yake lakini nchi nzima tuna uhaba wa nyumba milioni 3.8 mpaka sasa. Uhaba huu unaendelea kukua. Kwa hiyo, jukumu hili ni kubwa sana kuchukuliwa na Shirika moja la Nyumba la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapokuwa na Sera ya Nyumba itawezesha na mashirika mengine au taasisi binafsi, wajenzi wengine kuingia katika kuchangia, ku-provide au kuleta suluhisho la kuwa nyumba nyingi. Kwa hiyo, hii itatusaidia zaidi katika kuongeza idadi ya nyumba ambazo tunazihitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuna tatizo kwamba miji yetu inakua kwa haraka na kwa nchi yetu hili siyo tatizo, ni neema tunaweza tukasema kwamba nchi yetu inakua kwa haraka na Watanzania tunaongezeka kwa wingi, lakini sasa jinsi population inavyokua na hili tatizo la uhaba wa nyumba nalo ndiyo tunazidi kwenda nalo. Tumetokanalo tangu enzi za uhuru mpaka sasa na litazidi kuongezeka tusipochukua hatua za haraka za kulifanyia kazi. Bunge hili, ndiyo Bunge litakaloshuhudia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka yake mitano ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilikuwa nina ombi; tunaomba Wizara yetu ya Ardhi ituletee...; Mheshimiwa Waziri anapokuja kwenye kuhitimisha atuletee ahadi au kusema kwamba hii Sera ya Nyumba siyo Sera ya Ardhi. Kuna tofauti katika Sera ya Nyumba na Sera ya Ardhi. Atuletee ahadi kwamba ni lini sasa Wizara yake itakuwa tayari imeandaa hii Sera ya Ardhi ili Bunge hili liweze kupitisha sheria ya nyumba ambayo itarahisisha utekelezaji wa Dira yetu na vilevile itakuza upatikanaji wa makazi ya bei rahisi au bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mariam ahsante sana.
MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)