Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hii hoja ya Wizara ya Ardhi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uzima. Nimesimama hapa na mimi nikiwa mwenye afya tele kuweza kuchangia na kushauri mambo mbalimbali katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya na hususan kwenye Wizara hii ambayo imekuwa na changamoto nyingi sana. Amepambana kuhakikisha kwamba angalau changamoto hizi zinapungua na kuweza kuwapa Watanzania na wananchi wetu tabasamu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba sana nimpongeze Kamishna Mathew, Kamishna huyu amekuwa akifanya kazi kubwa na nzuri sana, amekuwa akipambana hadi huko field, kazi yoyote ama changamoto yoyote utakayomweleza Kamishna Mathew amekuwa akiifuatilia na kuifanyia kazi kwa karibu hata mwenyewe kufikia hatua ya kufika site ili kuweza kujionea hali halisi. Mimi ninampongeza kwa moyo wa dhati na ninajua kazi yake anayoifanya, lakini tuendelee kumtia moyo kwa sababu kazi ni ngumu huko chini, changamoto bado ziko kedekede.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze DG wa National Housing kwa kazi kubwa anayofanya. Leo hapa ninapozungumza pale kwangu Tabora kuna eneo lilikuwa linaitwa changamoto limekwenda kuwa eneo ambalo kwa kweli limeleta mabadaliko makubwa katika Mji wa Tabora na sasa hivi pale panajengwa jengo kubwa la National Housing ambalo litakuwa ni jengo la kitega uchumi kwa ajili ya frame pamoja na nyumba za kuishi watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimpongeze sana DG wa National Housing kwa kazi kubwa. Niseme endeleeni tu jamani, jengo lile liishe angalau mpaka by mwezi wa ngapi mambo yaweze kuwa mazuri na watu waweze kutumia jengo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nishauri mambo kadhaa na hususani nijielekeze zaidi kwenye Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi. Bahati nzuri sana mimi nimekuwa Mjumbe kwenye Kamati ya Ardhi, na Maliasili, jambo hili siyo jambo geni sana watu wanalizungumza, wanalisema lakini tumeshauri sana kwenye Bunge hili. Laiti kama Wizara ingekuwa inatekeleza maelekezo ama mawazo ya Wabunge leo hapa tungekuwa hatuzungumzi suala la Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Hapa tunapozungumza ni katika vijiji 12,000 plus ni vijiji 2,000 plus tu ndivyo ambavyo vimepangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda ama tunapiga mark time pale tulipo. Tumeshauri, tumesisitiza lakini na leo naomba nishauri na Serikali iko hapa, niombe sana hii Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi iondoeni huku ipelekeni kwa Mheshimiwa Kitila kule ndiko kwenye mipango, pengine kule mipango hii ya kuhakikisha kwamba watu wanapangiwa na kutengenezewa matumizi bora ya ardhi yanaweza yakafanyika vizuri kwa sababu ndiko kwenye mipango yenyewe, huku yawezekana kabisa fedha ndiyo tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe utakuwa shahidi umekuwepo Bunge la Kumi na Mbili, tunapanga bajeti, tunapitisha hapa shilingi bilioni 1.5 labda inakwenda kupelekwa shilingi milioni 400, shilingi milioni 500 unapima vijiji vingapi? Unapanga vijiji vingapi? Kwa hiyo, bado tunaendelea kupiga mark time hapo hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kushauri hapa tutapiga kelele kila siku kuhusu tume hii, kama hatutafanya mageuzi makubwa kwenye tume hii basi itakua ni historia vijiji kwenda kupimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili jambo linaitwa Kliniki ya Ardhi, hakuna eneo ambalo linaleta migogoro kwa wananchi kama eneo hili la Kliniki ya Ardhi. Kliniki ya Ardhi tunajua ni darasa, darasa ambalo litakwenda kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala mazima ya migogoro ya ardhi na mambo mengine yanayohusiana na ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hili Mheshimiwa Waziri naomba ulijue pale wanapofika kwenye hizi kliniki ndiyo kumekuwa kunaleta migogoro ya hali ya juu. Unakwenda kwenye kliniki unaenda kutoa hati kweli? Kwangu mimi Tabora nimefanya mkutano mmoja tu na wananchi kero za ardhi zaidi ya 15 na sasa hivi ninavyozungumza na wewe kero nyingine mbichi ziko pale ofisini kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anauziwa ardhi anaambiwa na mtu mwingine hii ardhi ni ya kwangu, hii ardhi ni hivi, changamoto ni nyingi kuliko tunavyofikiria, hii Kliniki ya Ardhi kuna mtu alisema hapa kwamba kesho mtaita sasa badala ya Kliniki ya Ardhi mtaomba Hospitali ya Ardhi, ndiyo tunakoelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama kliniki inashindakana, inaenda kuleta matatizo makubwa zaidi, tutakweda kuomba hospitali ili matatizo haya yaweze kutatuliwa. Mimi nimekuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa vipindi viwili, hakuna kipindi ambacho nakutana na changamoto za ardhi zinazotia aibu kama kipindi nimekuwa Mbunge wa Jimbo na ni palepale kwangu Tabora Mjini.
Mheshimiwa Waziri twende site ukaone huko watu wanavyolia, twende site ukatusaidie, twende site utuondolee miiba kwenye njia zetu tuweze kupita salama ili na wewe uweze kuendelea kuwa salama, kwa sababu hali ni mbaya ya ardhi kuliko tunavyotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo mifumo, kuna mfumo lakini huu mfumo uko Dar es Salaam, uko Dodoma, uko na Arusha; kati ya mikoa 26 ni mikoa mitatu peke yake ndiyo huu mfumo upo, huku kwingine kunatumika nini? Bado Wizara imeendelea kuleta mifumo mingine tofati tofauti inazidi kuwachanganya wananchi wetu, inafanya wananchi wasielewe upi ni mfumo sahihi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alishasema kwamba jamani mfumo uwe mmoja, mifumo ikiwa mingi inapoteza hata hao wananchi. Hii mifumo ndiyo inaleta rushwa, ndiyo inaleta watu kudhulumiwa ardhi zao, ndiyo inaleta kila aina ya changamoto katika Taifa letu na nchi yetu kwa ujumla kwenye Wizara hiiā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Kicheko)