Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza na mimi niipongeze Wizara ya Ardhi kwa hotuba nzuri ya bajeti, lakini ninayo tu mambo machache ya kuweza kushauri. Wizara ya Ardhi, Kitengo chetu cha Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, hapa bado tunahitaji kuweka jitihada ya makusudi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo letu la Msalala lenye square kilometer 3,400 ni square kilometer 1.5 peke yake ndiyo imepimwa, lakini eneo hili linafaa kwa matumizi ya kilimo, linafaa kwa matumizi ya mifugo, linafaa kwa uchimbaji kwa asilimia kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto tunayoipitia sisi sasa hivi Wizara ya Ardhi haina mawasiliano na Wizara ya Madini. Sehemu ambayo ina leseni ya uchimbaji kuna viwanja vya makazi. Kwa hiyo, unaona kabisa changamoto ambayo tunapitia pale sehemu ambayo inafaa kwa ajili ya mifugo hapajatengwa kwa ajili ya mifugo, sehemu ambayo inafaa kwa ajili ya mabonde ya kilimo hapajaainishwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazingira haya tunawachelewesha Watanzania wenzetu kutajirika kwa kutokupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo yetu. Tunakosa mashamba makubwa ya kilimo chenye tija kwa sababu ya ardhi kutokupangwa. Tunakosa migodi mikubwa ambayo wawekezaji wangeweza kufika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uchimbaji na mipango kwa ajili ya uchimbaji na kusiwe na migogoro yoyote kwa maana hakuna makazi maeneo hayo yametengwa maalumu kwa ajili ya shughuli za uchimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashindwa kuvutia wawekezaji, wawekezaji wanaona kuwekeza kwenye maeneo hayo ni gharama kwa sababu tunakwenda kulipa fidia watu wengi ambao wangeweza kupangwa kwenye maeneo mengine na maeneo hayo yakaachwa wazi kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inakusanya kodi ya ardhi, tungeweza kusema kodi ya ardhi ya mwaka mmoja tu irudi ikaweze kupanga miji yetu, tutapiga hatua kubwa mno. Halmashauri ya Msalala peke yake mpaka sasa tumekusanya shilingi milioni 290 kwenye kodi ya ardhi na ukumbuke halmashauri hii bado ni vijijini; je, halmashauri za mjini zimekusanya shilingi ngapi?
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mabula, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Emmanuel Cherehani.
TAARIFA
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji tatizo lililoko Halmashauri ya Msalala ni tatizo pia lililopo katika Halmashauri ya Ushetu, maeneo makubwa hayajapimwa, lakini bado kuna mgogoro kati ya Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Usumbwa Forests Reserve, mpaka wake pia ni mgogoro ambao tulishaufikisha Wizara ya Ardhi, lakini bado hatujapatiwa majibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mabula Johnson Magangila, unaipokea hiyo Taarifa?
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea Taarifa ya kaka yangu Mheshimiwa Cherehani, ninaomba niendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili linaitia gharama hata Serikali kwa ujumla, maeneo ambayo hatukupaswa tupeleke barabara za lami, hatukupaswa tukajenge madaraja kama ni maeneo ya kilimo tunalazimika kupeleka miundombinu hiyo kwa sababu wananchi wameenda kuishi wanavyochagua wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo nguzo za umeme zinafuata kaya tano kwa sababu wananchi hatujapanga matumizi bora ya ardhi. Kuna maeneo tunalazimika leo hii, ni kwa sababu gani miji yetu hata hapa Dodoma tu, miji yetu imejengwa kutazama highway ni kwa sababu gani leo hii mtoto anagongwa na gari akienda shuleni? Anavuka barabara ya highway, kwa sababu gani, unaendesha gari kwenye highway unagonga ng’ombe? Hii yote ni matumizi ya mipango mibovu ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miji yetu ingeweza kutizama upande mwingine, highway kusingekuwa na matuta, kusingekuwa na alama za zebra, lakini kwa sababu tunajichanganya wenyewe, tunajenga shule huku, watoto wavuke upande huu, waende wakasome huku, kwa hiyo, watoto wanagongwa na magari. Matumizi bora ya ardhi yatatuokoa na tunawategemea sana Wizara ya Ardhi waweze kutukomboa kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye migogoro ambayo inawezekana kwa asilimia kubwa imesababisha mpaka Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kunyang'anywa mihuri. Sisi kwetu kwenye majimbo, tunaotoka vijijini Usukumani, Mwenyekiti wa Kitongoji ana kazi nyingi zaidi ya kuuza ardhi. Mwenyekiti wa Kitongoji ndiye anayebaini, ndiye anayemtambua raia wa kitongoji hicho, muhuri wake unatumika kumwandikia barua mtu aende akapate NIDA, muhuri wake unatumika, kwa ajili ya kutoa kibali cha kwenda kuuza ng'ombe. Leo hii kule kwetu, tunapozungumza hatujui mtu anayeswaga ng'ombe amewaiba au ni wa kwake au ni mfanyabiashara, hatujui! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kitengo cha utambuzi kimeondolewa kwa sababu ya migogoro ya ardhi, ninaomba ikiwezekana litoke tamko, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji wasihusike kuuza ardhi, ila waendelee na zoezi lao la utambuzi, tutatoa NIDA kwa wakimbizi! Watendaji wa Vijiji hawakai kwenye maeneo yao wanayofanyia kazi, hawajui mipaka ya maeneo yetu, hawamjui nani ana ng'ombe, nani ni mfanyabiashara, nani si mfanyabiashara wa ng'ombe! Watatoa vibali vya kuswaga ng'ombe kwa wezi. (Makofi)
(Hapa kengele Ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Hitimisha.
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)