Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Ardhi. Naanza kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninampongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote kwa kazi mnayoendelea kuifanya. Ni ukweli kwamba ardhi tuliyonayo hapa nchini haiongezeki, lakini watu kwa maana ya Watanzania wanaongezeka na matumizi na mahitaji ya ardhi yanaendelea kuongezeka. Hata hivyo, ardhi hii tuliyonayo tukiitumia vizuri kwa kuipangilia ni chanzo muhimu na cha uhakika cha mapato ya Serikali na pia pato la mtu mmoja mmoja kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya, kama utangulizi, mchango wangu utajikita katika suala zima la Mabaraza ya Ardhi na Nyumba. Naanza kwa kueleza kidogo chimbuko la Mabaraza haya ya Ardhi na Nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1991 Serikali iliunda tume ambayo iliongozwa na Profesa Issa Shivji. Pamoja na mambo mengine, tume hii ilikuja na mapendekezo ya namna ya kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi tuliyokuwanayo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tume hiyo ikapendekeza kwamba migogoro hii itoke kwenye mfumo rasmi wa kimahakama na ishughulikiwe na mabaraza, lakini pamoja na hayo, mapendekezo haya yalijikita katika nguzo kubwa tatu; moja, kuanzishwa kwa mabaraza kuanzia ngazi za kijiji, kata na wilaya, lakini pia kutenganishwa kwa hizo shughuli kutoka kwenye mfumo rasmi wa kimahakama kwenda kwenye mfumo wa mabaraza.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi au nguzo nyingine ulijikita zaidi katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi. Pamoja na haya yaliyotajwa, ndiyo ulikuwa msingi wa kuanzishwa kwa Sheria ya Ardhi, Namba 04 na Namba 05 ya mwaka 1999 ya masuala yote ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya kuanzisha mabaraza haya, kwanza ni kupunguza urasimu uliokuwepo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi au upatikanaji wa haki kwa watu ambao walikuwa na migogoro. Pia ilikuwa ni kutumia mfumo rahisi na shirikishi wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuwa umiliki wa ardhi wa nchi hii ulikuwa unaendeshwa au kusimamiwa na mila na desturi za makabila mbalimbali hapa nchini. Pia kipindi hicho tulikuwa tuna uchache wa mahakama za mwanzo hivyo, kulikuwa kuna mlundikano na ucheleshwaji mkubwa wa haki pale ambapo wananchi walikuwa wana migogoro na ikawa ni kero kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kulikuwa kuna gharama kubwa ya uendeshaji wa kesi katika mahakama za kawaida, lakini pia iliwagharimu wananchi kuzitafuta au kuzifuata huduma katika Mahakama za Hakimu Mkazi, kwa maana ya Mahakama za Mikoa. Kwa hiyo, kwa uchache haya ndiyo malengo na makusudi ya kwa nini tulianzisha mabaraza haya kwa wananchi kipindi hicho cha mwaka 1991, chini ya Tume ya Profesa Issa Shivji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabaraza yalianzishwa, lakini hali ikoje kwa sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa katika wilaya 139 tunayo mabaraza 118, bado wilaya 21 mpaka leo toka mwaka 1999 hazina Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Tafsiri yake ni kwamba bado kuna wilaya changamoto ya utatuzi wa migogoro ya ardhi imekuwa ni kero kwa sababu hakuna mabaraza haya. Hata hivyo, pamoja na kwamba kuna baadhi ya wilaya zina Mabaraza na Wenyeviti, lakini huduma zinazotolewa zimekuwa ni changamoto na kero kubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, wenyeviti ambao wanaendesha mabaraza hayo wako wachache na watumishi kwa ujumla. Mwenyekiti mmoja anaweza akahudumia wilaya mbili mpaka tatu jambo ambalo linafanya ucheleweshwaji mkubwa.

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Paresso, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sigrada.
TAARIFA

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaomba nimpe Taarifa mchangiaji kwamba miongoni mwa mikoa ambayo haina hayo Mabaraza ni Mkoa wa Njombe wenye wilaya tano, lakini na Mwenyekiti wa Baraza ni mmoja na anazunguka mkoa mzima mpaka sasa. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Paresso, Taarifa unaipokea?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashindwa kuipokea, siipokei mpaka nifanye utafiti kujiridhisha haya anayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba mfano Wilaya yangu ya Karatu ninayotoka, pale tuna Mwenyekiti, lakini yule Mwenyekiti anaishi Arusha. Huduma anazitoa mara chache sana kwa wiki au kwa mwezi jambo ambalo ni kero. Mwenyekiti huyo huyo anaenda kuhudumia wilaya nyingine za jirani jambo ambalo limekuwa ni changamoto na ni kero kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko makubwa ya utoaji wa rushwa ili uweze kupata haki. Rushwa imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi. Tafsiri ni kwamba kwenye mabaraza haya mtu hataweza kupata haki yake mpaka atoe chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, nini kifanyike au ushauri wangu kwa Serikali. Kwanza, ifanyike tathmini ya kina kuona kama malengo ya uanzishaji wa mabaraza haya yamefikiwa. Kwa maoni yangu hayajafikiwa. La pili, wakati tunaanzisha kipindi hicho, kulikuwa kuna makusudio; je, hali halisi ya sasa ikoje? Tunahitaji bado kuendelea nayo au sivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ushauri; kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Mahakama ndiyo chombo cha utoaji wa haki. Pale ambapo panatokea migogoro, maana yake ni kuna haki inatafutwa hivyo, masuala haya yarudishwe kwenye utaratibu wa kawaida wa kimahakama ya utafutaji wa haki, tuondokane na mfumo wa utumiaji wa mabaraza haya katika migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.