Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Wizara ambazo niliomba kuchangia zinaisha, lakini kila nikikaribia kuchangia ninaambiwa dakika tano, dakika sita, nimejiandaa kwa dakika 10, ninaambiwa dakika tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninadhani siyo sawa, hata kama Kiti hakipingwi. Nilikuwa nimejiandaa kuchangia Wizara zote, kila nikisimama tu, jana, Bunge limeisha hapa muda wake... (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa changia, unapoteza muda.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya ahsante, lakini ujumbe umefika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara ni Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, lakini kule Tarime inaitwa Wizara ya migogoro ya ardhi na makazi holela, kule Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ardhi imetuchonganisha sana na wananchi na imejenga chuki na Serikali, imejenga chuki na chama, wananchi wanalalamika sana. Mheshimiwa Waziri mimi ni mwalimu wangu wa chemistry pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umepewa mfupa mgumu na nitachangia hapa bila kumuangalia mtu usoni ili ujumbe ufike. Mheshimiwa Waziri, Wizara hii sio ya kuvaa suti na tai, hii Wizara ni ngumu, siyo Wizara ya kukaa humu ndani kwenye kiyoyozi my brother. Ni Wizara ya kwenda site.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu jana nimesikiliza Wabunge wanasema umeahidi kwenda, haujaenda. Utamtuma Naibu Waziri, hajaenda. Nimekuandikia barua tarehe 20 Aprili Mheshimiwa Waziri, file hili hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo wananchi wamekaa, pale Kata ya Bumera, Kijiji cha Kwisarara, Kitongoji cha Bunyama; wamekaa tangu mwaka 1974, ni umri wangu hapa, mimi nimezaliwa mwaka 1974, lakini nimeenda site kwa gharama zangu. Waziri na Naibu Waziri wana magari ya Serikali, posho wanalipwa, mafuta hawaweki kwenda tu site kule. Watu wanauwana, huendi Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetoka hapa na gari langu private, nimeenda jimboni, nikafanya mkutano, nikakupa clip ya malalamiko. Mwenyekiti wa Kijiji aliyekuwepo kwa miaka hiyo anasema hakuitisha mkutano mkuu kutoa eneo ekari 351, kuna kaya 75 katika eneo hilo. Wameenda wananchi wamekaa, Serikali ya Kijiji imeandika barua, mpaka sasa hivi hata majibu hawajapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimetangaza kule kwamba kwa kuwa kuna mtu anaenda kwenye Baraza la Ardhi anawaambia kwamba atawakamata wamevamia eneo. Tangu mwaka 1974 hati imetolewa mwezi wa Februari mwaka huu, wameongea huyu mtu anasema mwekezaji uchwara ameongea na Afisa Ardhi wa Wilaya, ameenda pale Musoma, akaja makao makuu, anayo hati kwenye begi anatembea nayo, sasa wananchi wote pale ni mateka. Nimewaambia hapa kila mtu ajilinde, mtu asiingie kwenye eneo lile mpaka Waziri aende, haki itendeke, atuambie yeye alipataje eneo?
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Tarime Vijijini wamesikia na hiyo ndio kero kwa sababu, Waziri hajanisikiliza Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro mwingine pale ni watu wameuana kwa muda mrefu. Wanagombana, hawajengi, uhasama kwenda kuangalia mipaka tu. Mgogoro kati ya Tarime na Rorya watu wameshikiana mishale. Nimelalamika, nimeandika, hawasikilizwi. Mgogoro wa vijiji saba, Kata ya Kwihancha, Kata ya Girong’a, Nyanungu, wameenda watu wa ardhi wanaweka beacon wenyewe bila wananchi kushirikishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara ni miongoni mwa Wizara ambazo Wabunge wangekuwa na akili kama ya kwangu na wangekuwa kama mimi, hii Wizara tungeiweka kando kwanza hii bajeti yake tujadili habari ya migogoro na Waziri atuoneshe kama kweli uwezo huo wa kwenda kutatua changamoto upo?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mnazungumza hapo, hivi inawezekanaje kwenye Baraza la Ardhi lile wanaenda, kwanza lazima watu wale wawili uwachangie gharama. Anayemdhulumu mwananchi wa kawaida maskini ni tajiri, huyu maskini hana pesa. Kigezo kimojawapo ni lazima kwanza mtoke muende site. Sasa yule mwenye nacho anatoa gharama, maskini hatoi. Hivyo, wakienda site unafikiri nani atapewa haki? Katika hiyo scenario nani atapewa haki pale? Maana yake ni watu wenye pesa. Mheshimiwa Waziri, ingekuwa mimi nimekalia hicho kiti, kwa muda ambao umekaa hapa, ningejaza magereza watu wa Ardhi, wengi sana pale kwa sababu hivi anatoaje hati mbili-mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, hati zipo kwenye mfumo, mimi nina hati yangu, ninalipia ardhi, unakuta kuna mtu amejenga eneo hilo na vibali anavyo. Yaani mimi nina file la ardhi hiyo hiyo na mwenzako ana file la ardhi hiyo hiyo! Sasa inaonekana nani amem-time mwenzake?
Mheshimiwa Naibu Spika, huu sio mpango. Hii Wizara, Waheshimiwa Wabunge, tutachangia mwaka huu, mwaka ujao wakija na majibu na maelezo kama haya, tuwe na mtindo mwingine kwa sababu haiwezekani. Hivi ninyi mnaona furaha kukaa kwenye majumba, kwenye Bunge ambalo wananchi wanalalamika, wanalia. Maliasili kuna matatizo, Ardhi kuna matatizo, Mifugo kuna matatizo, Maji kuna matatizo, Madini kuna matatizo, TAMISEMI kuna matatizo! Hivi hamuoni kama kuna shida hapo Waheshimiwa Wabunge? Hamuoni kwamba kuna shida?
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania waliopo nje wanataka tutoe suluhu, kwa hiyo, Waziri inabidi ajipange kweli kweli. Mbunge analalamika eti Waziri asiende site? Ni kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri wamepewa kazi na Mheshimiwa Rais, Rais hawezi kuelekeza cha kufanya. Wana miongozo, waende site watatue matatizo. Tujadili hoja bila kuangalia sura ya mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitashika shilingi, kama inakimbizwa-kimbizwa nitashika shilingi. Kwa kweli, sitaunga mkono hoja hizi mpaka nijue namna ambavyo suluhu inapatikana kwenye migogoro. Kata zote watu wanalalamika, sasa mimi ninaungaje mkono?