Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, na mimi ninapenda kumshukuru Mungu aliyenipa afya na pumzi siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi anayoendelea kuifanya kututumikia kwenye nchi yetu. Mimi leo nina jambo moja tu ambalo linaweza kuniumiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninawapongeza sana Wizara ya Ardhi toka tulikotoka mpaka kufikia hapa. Sisi Mkoa wa Ruvuma hati tulikuwa tunachukulia Mbeya mara ya kwanza, baadaye tukachukulia Mtwara, lakini muda ulivyoenda tumefikia sehemu tunachukulia mkoani kwetu. Tumeletewa Kamishna pale na Msajili. Ninawapongeza kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika, lakini kwenye mazuri hayakosi mabaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tunatambua hati ndiyo maisha, hati ndiyo afya ya mtu, hati ndiyo investment. Mtu akiwa na hati anaweza kupata mtaji, lakini kwa sisi Mkoa wa Ruvuma tunapata taabu sana, wananchi wanapata taabu kupata hati. Tunatamani huu mfumo ambao wameuongelea Wabunge wengine ungeenda na kwetu Mkoa wa Ruvuma, lakini pale tumepewa kama demo, Mbinga DC pamoja na Songea DC wameanza kufanya huo mfumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo ungetusaidia sana kuepusha huu urasimu ambao hauna sababu kwa sababu kwa kutumia analogue inatusumbua sana kwenye suala la ardhi kupata hati. Unakuta watumishi ni wachache sana, lakini bado hawa wateule ni wachache, Tunduru unakuta mmoja, ukienda Songea Manispaa ni mmoja, ukienda Mbinga mmoja, kwingine hakuna, Madaba hakuna, lakini inatakiwa huyo huyo ndiyo aidhinishe kila kitu kwenye halmashauri. Kwa hiyo, akiumwa na ofisi imesimama, hati hazitoki. Ikitokea amelazwa hati haitoki, akiwa na tabia zake zile ngumu za kuringa, maana yake na sisi wote tunamngoja yeye. Watumishi ni wachache hii Wizara, tunaomba sana mjitahidi kutuongezea watu. Mteule kwa nini awe mmoja na anatuhudumia wananchi 300,000?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumekuwa na muamko mkubwa kwa sababu hati inatumika benki. Kila mmoja anatamani kuwa na kiwanja, anatamani kuwa na nyumba, angalau hela yake ataishika kwenye hati na atafainyia kazi, benki zitatusaidia, lakini utoaji wa hati ni mgumu, ni mgumu. Tunaomba sana, wakati mfumo unaendelea kutengenezwa/kutekelezwa mfumo huu wa electronic, basi tunaomba sana miundombinu ipelekwe kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya watumishi wa halmashauri kwenye Idara ya Ardhi si waaminifu. Ukienda kwenye upande wa ramani mtu anaambiwa bado ramani, huwezi kupewa hati yako au kuanzishiwa kitu chako cha kiwanja hadi kuwe na ramani. Mchora ramani ni mmoja, wakati huo huo unakuta wengine wanaojitolea wanaishi kwa remote. Hawezi kufanya kazi kulingana na ambavyo yeye anataka, labda bosi wake anamtuma kazi nyingine, kwa hiyo, hiyo ramani haitachorwa miezi mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza sana Ardhi Mkoa, kwa Kamishna na Msajili, pale kuna bwana kijiji anajitahidi sana. Ikifika hati mkoani haichelewi, kama itakavyochelewa huku chini. Tunaomba, kwa nini chini ichelewe na juu kule isichelewe? Yaani huku umefanyiwa assessment, umekadiriwa, umetoa pesa zote, lakini ukifika kupata hiyo hati kupelekwa mkoani inasumbua. Ikifika mkoani hutoi chochote, hati inatoka, yaani muda mfupi sana unakuwa umepata. Ninawashukuru sana watu wa mkoani wanatuhudumia bila kujali hadhi zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hili suala la ramani. Ramani tunaomba, mimi ninashauri hapa, mkoa uandae bajeti na uhakikishe unafanya research ya ramani kila kata. Kwa sababu unafika unamwona mtu mmoja mwenye ramani anamtafuta; kule kwetu kuna mtu anaitwa Mzee Hyera; anatafutwa huyo Mzee Hyera kama fedha. Yeye ndiye anayeijua ramani ya mwaka fulani. Kwa nini wasifanye research wakajua ramani kuwa yetu ni hii? Hata kama ni mtumishi mpya, mgeni, akibonyeza computer ajue hii ramani ipo wapi, ninafanyaje ili mwananchi ahudumiwe, lakini mlolongo unakuwa mrefu. Kila mmoja kwa nafasi yake, kila mtu anaringa anavyotaka ilhali kitu hiki ni muhimu sana, mnatuumiza wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu kliniki. Kliniki ya Ardhi imekuwa tofauti kidogo kwenye mkoa wetu, sisi hatuna malalamiko sana. Tunaomba iongezewe bajeti kwa sababu kitu kinachotuumiza kwenye kliniki ya ardhi ndani ya wiki moja anatoa hati 300, lakini mtu mmoja mmoja anapata taabu miezi miwili hajapata hati. Kwa nini, ni kwa sababu siku ya kliniki inawezekana kutoa hati 300, lakini mtu mmoja mmoja hapati hiyo hati? Waongezewe bajeti, wapewe weledi, wafundishwe. Kwetu hamna kelele za kuzidi. Wizara iwape bajeti watu wa ardhi ili waende wakafanye hizo kazi. Kwa wiki hati 300 hadi 400 tutapunguza kelele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)