Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Neema Peter Majule

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi ya kuchangia kwenye Wizara hii nyeti kabisa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze kabisa kwa kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kazi njema ambazo anafanya na hata kuweza kutuletea sasa Waziri mpya kabisa Dkt. Leonard, Naibu Waziri Kaspar Mmuya pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Anthony Sanga; pia tuna Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy, mwanamke. Kwa kweli tumefurahi sana kuweza kupata watendaji hawa ambao tunaamini kabisa wanaenda kutuvusha kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja nimpongeze tena Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Niwapongeze pia Marais waliopita kwa tendo hili kubwa sana la kutokuruhusu mahusiano yoyote au labda Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi zozote kuhusika na ardhi. Ardhi ni ya Watanzania na ardhi itabaki kuwa ya Watanzania kwa vizazi vyote. Sisi hatutaki mahusiano yoyote ya ardhi na nchi nyingine. Ardhi yetu bado ni kubwa na ardhi hii inatutosha sisi na tunaendelea kuifanyia maendelezo, ikiwepo kilimo, mbuga zetu za wanyama pamoja na makazi ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niipongeze sana Wizara ya Ardhi kwa ajili ya Dodoma. Ni kweli kuwa tulikuwa na migogoro mingi sana tulipokuwa na CDA, lakini mpaka sasa hivi jiji limefanya kazi kubwa sana. Kwa kupitia kliniki ya ardhi wametatua migogoro mingi. Ni lazima tuseme ahsante na tutambue. Pia wame-document kila migogoro ipo kwenye document. Ukienda kutaja mgogoro wowote wana-reference ya kwamba mgogoro huu uliwahi kufanyiwa kazi mahali fulani, bado mahali fulani utaisha. Pia wametenga viwanja kwa ajili ya watu wanaokwenda kupata double allocation wameweza kupewa viwanja na bado wanaendelea kutoa hivyo viwanja. Nipongeze jitihada hizi za Mkuu wangu wa Mkoa Rosemary Senyamule, DC wangu Alhaj Jabir Shekimweri pamoja na Mkurugenzi wa Jiji Dkt. Fred, wanaendelea kufanya kazi nzuri ili kumaliza migogoro ya Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa nichangie mambo matatu; jambo la kwanza, umilikishaji wa ardhi kwa wanawake bado. Tumepewa takwimu hapa kwamba wamiliki wa ardhi mpaka sasa hivi walio na hati ni kama 26% tu. Kati ya hao wanawake waliomiliki ni 28% tu. Kuna ugumu gani kumilikisha wanawake ardhi? Je, ni mila zetu na desturi ndizo zinazotufunga wanawake wasimiliki ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe wito kwa Wizara yangu, huko vijijini kuna hati za kimila, wanawake wapewe usawa kwenye kumiliki. Kuna shida gani kusema heka hii moja itakuwa ya huyu mwanaume na heka hii nyingine itakuwa ya huyu mwanamke, ili wanawake nao wamiliki ardhi, waweze kukopesheka mikopo benki na taasisi za kifedha?

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu inapunguza migogoro baada ya kinapotokea kifo. Kwenye mambo ya mirathi wanawake wananyanyasika sana. Wanawake wamilikishwe ardhi ili nao wawe na haki sawa kama Watanzania wengine. Hadi sasa hiyo 28% haitoshi, jitihada za dhati zifanyike ili kumilikisha wanawake ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; Wizara hii ni ya nyumba pia na makazi. Bado kuna nyumba nyingi za tembe, bado kuna nyumba nyingi zimejengwa kwa udongo, full suit udongo mpaka kwenye kuanzia nani, kwenye ukuta hadi paa. Wizara hii kama tumeweza kupata ruzuku ya mbolea ikaweza kutusaidia kwenye kilimo, tumepata ruzuku ya nishati safi imetusaidia kutunza mazingira, kwa nini tusipate pia ruzuku ya bati na cement ili watu hawa wajenge nyumba za viwango na nyumba ambazo zitaweza kustahimili mvua zinazoendelea nchini kwetu? Ni kwa sababu gani tuna madarasa mazuri, tuna vituo vya afya vizuri, lakini nyumba za wale wanaozunguka hizo taasisi nzuri sana ni duni, kwa nini tusipate ruzuku? Mimi ninaomba tuje na mkakati huo au tuweze na sisi kupata ruzuku ya mabati ili kuboresha makazi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, mimi niiombe sana Wizara iendelee kumilikisha ardhi kwa watu wa vijijini. Hizi hati za kimila zitolewe tu bila kujali, zinasaidia angalau umiliki wa mtu ili wawekezaji wanapokuja wakute kuna mtu anamiliki hati na tusikubali kabisa kutoa ardhi yetu kwa wawekezaji, labda tuingie ubia na mwekezaji. Mwekezaji akiwekeza awe anampa na huyo mwananchi gharama au mapato yale anayopata ili mwananchi huyu asipoteze hati. Mwisho kabisa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaunga mkono hoja na ninaipongeza sana Wizara yangu ya Ardhi, ahsante sana.