Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Rashid Mohamed Mtima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai na leo ku-appear katika Bunge lako Tukufu. Nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi na nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kusimamia Serikali yetu na hasa katika Wizara hii muhimu sana ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza katika eneo moja tu ambalo ninaona kwamba tukienda anavyotaka na alivyopanga tutatatua matatizo makubwa yaliyopo kwenye Wizara hii; eneo la Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana tumeona ilivyotendewa haki na hata bajeti hii ambayo inakuja tunaona dhamira ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vyote vinapimwa baada ya miaka mitano. Jambo hili litaondoa migogoro ya ardhi kule vijijini, migogoro ya wakulima na wafugaji. Twende tukafanye ili tutekeleze maono ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa namna ninavyoona wanavyojipanga kufanya kazi. Tunawaona wanavyokimbizana kuangalia maeneo gani wanatatua matatizo au migogoro mikubwa ya ardhi katika nchi nzima. Tuendelee kuwapa nafasi na kuwa-inform katika maeneo mbalimbali. Ninaamini kwa namna nyoyo zao zilivyo na tunavyokaa nao kwenye Kamati, wanadhamira njema kabisa ya kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi inatatuliwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninataka nichangie eneo moja tu, nalo ni upangaji wa ardhi. Tumejipanga vizuri kwenye kupanga ardhi ya vijiji, lakini ninataka nisisitize kwenye kupanga ardhi ya miji. Ninasema hivi kwa nini; ni hali ya ukuaji wa miji tuliyokuwa nayo nchini. Tanzania kama nchi ipo kwenye rank ya juu kabisa ya ukuaji wa miji katika Afrika. Katika nchi sita za juu Tanzania ni ya sita. Tunatarajia inapofika mwaka 2050 nusu ya Watanzania watakaa mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Dar es Salaam ni jiji linalokua namba tano kati Afrika. Ukuaji huu ukiangalia kwa namna inavyokuwa mwaka hadi mwaka, Dar es Salaam na Tanzania unaenda kwenye nafasi ya juu kabisa ya ukuaji wa miji kutoka namba sita tulipo leo kama nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa East Africa, sisi Tanzania ndio tunaoongoza kwa kukua katika miji. Dar es Salaam katika East Africa ndilo jiji la kwanza kwa ukuaji; linakua kwa zaidi ya asilimia tano. Ukuaji huo ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba halmashauri zote ambazo zina makao makuu kwenye maeneo ambayo siyo maeneo yao ya utawala zihame.
Mheshimiwa Naibu Spika, azimio hili limekuza vijiji vyetu vingi kwenda kwenye miji. Kwa mfano tu maeneo ya Mkoa wa Mtwara, leo Halmashauri ya Newala imehamia kwenye eneo la Kitangali ambalo lilikuwa kijiji. Kwa upande wa Masasi, Wilaya ya Masasi imeenda Mbunyuni ambako kilikuwa kijiji. Sasa kwa Mkoa wa Mtwara tu vijiji vitatu vimebadilika kuwa miji kwa haraka kwa tamko hilo tu la Rais, je, nchi nzima tunavijiji vingapi? Kwa hiyo, tuombe tukapange miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme upangaji wa miji una faida kubwa kwenye nchi yetu. Unafaida kubwa, hii migogoro tunayoisema leo ya ardhi kama miji itapangwa na kupimwa, viwanja vitakuwepo, watu hawatagombania, tutaondoa migogoro...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. RASHID M. MTIMA: ... lakini ...

MWENYEKITI: Hitimisha Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. RASHID M. MTIMA: ..., tunaenda kuweka maeneo ya huduma. Tukipanga maeneo kama vile ya shule yanakuwepo. Kwa hiyo ni jambo ambalo linafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe kwa kusema sasa sisi watu wa Newala Mjini, mji wetu tunataka tuupange. Tunaomba Serikali itusaidie, itupe fedha. Tumeandika andiko tunalileta Wizarani, itupe fedha tulipange na Mbunge wao ni Afisa Mipango Miji. Kwa hiyo, tunahakika ya kuusimamia mji ule ukae vizuri na hizo fedha tutarejesha...

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. RASHID M. MTIMA: ...nilirejesha hizo fedha nikiwa nafanya Tandahimba, zitarejeshwa nikiwa Mbunge pale Newala Mjini. Tunaomba mtupe fedha za KKK ili tupime mji ule, tuusimamie vizuri ili tuweze kusimamia miji yetu nchi nzima...
MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga hoja mkono, ahsante. (Makofi)