Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Haran Nyakisa Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nishukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu wa mawazo katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitaenda kuchangia maeneo matatu; eneo la kwanza ni eneo la kliniki ya ardhi. Ni eneo ambalo limeonesha mafanikio makubwa sana katika Wizara yetu hii, hivyo tunatakiwa sisi Waheshimiwa Wabunge, tuone namna gani wanaweza wakaboresha huduma hii kwa sababu imeonesha inatatua matatizo kwa haraka na upatikanaji wa haraka wa hati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kliniki ya ardhi limefanya vizuri sana katika mikoa mingi hususani Mkoa wetu wa Dar es Salaam katika upatikanaji wa hati. Mathalani, kwa miaka mitatu mfululizo imetatua migogoro zaidi ya 4,000 na pia imetoa hati zaidi ya 100,000 kiasi kwamba miaka ya nyuma huko idadi hii ilikuwa ni ngumu sana kuweza kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliane kwamba kliniki ya ardhi inafanyika katika maeneo mengi, kwa maana ya kutoa elimu kwa wananchi, inawasaidia kutatua migogoro ya papo kwa papo na pia inasaidia kusukuma upangaji na upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa haraka kwa sababu hili linakuwa one stop centre ya watumishi wote ambao wanakuwa wanatumika au kuhusika na upatikanaji wa hati. Hivyo, mimi ninapenda kuwapongeza sana Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna faida chache ambazo ninaweza nikazitaja, kwamba Serikali inaweza kukusanya mapato kirahisi kwa sababu wananchi wote wanakuwa wanafuata huduma na pia kunakuwa na makusanyo makubwa. Mathalani Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2024/2025 wameweza kukusanya shilingi bilioni 84 kati ya shilingi bilioni 89 ambayo walikuwa wamepangiwa kama sehemu ya lengo. Kwa hiyo, unaweza kuona namna gani mpango huu unaisaidia sana Serikali kuweza kukusanya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi kubwa sana kwa Makamishina wote wa Ardhi pale Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na watumishi wenzao kwa namna wanavyojituma katika kushughulika na hizi kliniki za ardhi kwa kuzifanya mara kwa mara, kwa sababu wana utaratibu ambao wamejiwekea katika Mkoa wa Dar es Salaam kwamba kila baada ya miezi mitatu wanaenda kila halmashauri au kila manispaa. Kwa mfano Kigamboni walishafanya mwezi uliopita, mwezi wa tatu, wanaondoka pale wanaenda Temeke, Ubungo na sehemu zote. Kwa hiyo, kufanya hivi wanasaidia sana kupeleka huduma kwa wananchi, lakini pia Serikali inaweza kupata mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa ninaomba pia kupitia Kiti chako, Wizara hii inahitaji kuangaliwa sana katika hii angle ya kliniki ya ardhi kwa maana ya kuiwekea fedha ambazo ziweze kutumika. Pia Wizara ya Fedha wasichukue fedha zao kama zile ambazo zinakuwa zinapelekwa kwenye Mfuko Mkuu kwa sababu ukichukua zile fedha hawa wanaendelea kupambana kutumia own source kiasi kwamba wanakuwa wanapata shida sana kwa maana ya kuweza kuendesha hizi shughuli. Sasa ili waweze kuwa na tija waachiwe hizi fedha, waweze kuzungusha na kufanya kwa faida na kuiletea Serikali mapato makubwa kama ambavyo inavyoonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kigamboni kwangu kuna changamoto tu mbalimbali za uvamizi wa maeneo. Maeneo mengi kwa sababu Kigamboni ni jimbo ambalo limekuwa linaendelea na linakua kwa kasi, lakini pia limekuwa na migogoro mingi sana ya ardhi ambayo nimshukuru sana Mheshimiwa Kamishna Mathew ambaye amekuwa akija mara kwa mara tunakaa na wananchi na kuweza kuangalia utatuzi wa ile migogoro, kwa maana ya kuhakikisha maslahi ya wananchi yanakuwepo, lakini pia Serikali inakuwa imefanya kazi yake vizuri. Ninampongeza sana Kamishna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kuzungumzia; mwenzangu aliyetoka kuzungumza hapa alikuwa anasema kwamba Dar es Salaam ni jiji la sita kwa kukua duniani, lakini pia ni jiji la kwanza kwa kukua East Africa. Mimi niombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na timu yake ya Makatibu Wakuu na viongozi wengine, watupie jicho Dar es Salaam. Dar es Salaam sasa hivi ilivyofikia imetapika, hakuna sehemu nyingine ya kujenga. Sehemu za kujenga zinazotakiwa zijengwe zina migogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo ninataka nishauri kwamba watumie ile world class planning mode ambayo wenzetu wanatumia huko duniani kwa maana ya kwamba tubadilike, tutoke kwenye jiji, twende kwenye Dar es Salaam Metropolitan Authority. Tupanue lile jiji liwe kubwa. Mheshimiwa Waziri akilifanya hili katika wakati wake atakuwa umetengeneza legacy kubwa sana, kwa maana gani? Dar es Salaam inatakiwa sasa tuanze kuandaa miundombinu ya metropole kama zile ambazo tunaona maeneo mengine, kama vile Johannesburg na Dubai; wanatumia zile metropole na zile metropole zinaenda mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo nilikuwa ninatamani sana Wizara waje na mpango ambao utasaidia kupanua Dar es Salaam, itoke Dar es Salaam kwenda hadi Chalinze, itoke Dar es Salaam twende hadi Mkuranga, itoke Dar es Salaam iende hadi Mkuranga, itoke Dar es Salaam iende hadi Bagamoyo ili tupanue makazi ya watu. Kwa sababu Wizara ndio wenye nafasi ya kuweza kupanga na kumilikisha maeneo, tutakuwa tumeiweka ile population ya watu itakuwa imekaa vizuri, pia tumepunguza foleni ya watu Dar es Salaam. Kwa sababu mtu anakuwa anakaa Chalinze anakuwa na uhakika wa kufika Dar es Salaam kwa nusu saa kwa sababu ya kutumia metropole ....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, ahsante.

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)