Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zainab Rashid Kawawa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja na kuchangia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa maelekezo ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kuanzisha kliniki ya ardhi na hatimaye kutatua migogoro mingi ya ardhi nchini, lakini pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na timu yote ya Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia na kuanzisha mabaraza mapya yanayoshughulikia mashauri mbalimbali ya ardhi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii ya kuendelea kushughulikia migogoro ya ardhi, ninaomba nijikite kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi na nitazungumzia zaidi Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi ni rasilimali kuu ya maendeleo katika nchi yetu. Uzoefu mbalimbai unaonesha kuwa binadamu ndiye mtumiaji mkuu wa ardhi ambapo ukubwa wa ardhi hauongezeki bali matumizi ndiyo yanaongezeka. Kama ilivyo katika maeneo mbalimbali ya nchi, ardhi ya Mkoa wa Lindi ambayo sehemu kubwa ina sifa ya vijiji inatumika zaidi kwa shughuli za uzalishaji kwenye kilimo, uvuvi, utalii na madini. Vilevile ina misitu ya asili, uhifadhi wa wanyama pori na uwindaji.

Aidha, ardhi hiyo imebarikiwa kuwa na gesi ya asilia ambayo inafaa kwa kupikia na kuendeshea magari na matumizi ya umeme nchini. Ardhi yetu ina fursa nzuri ya uwekezaji wa viwanda na bado haijatumika kwa wingi.

Mhesimiwa Naibu Spika, hivi karibuni matumizi ya ardhi ya Mkoa wa Lindi yameongezeka kutokana na kuongezeka kwa kasi ya mifugo. Tunashuhudia jamii ya wafugaji inahamasika kupeleka mifugo mingi Mkoa wa Lindi. Sababu zinazoelezwa ni kuwepo kwa malisho ya uhakika kutokana na ardhi yenye rutuba, uwepo wa vyanzo vingi vya mito isiyokauka, na mazingira bora ambayo hayashambulii wala kuathiri afya ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa ya kuchochea maendeleo yanayoonekana kwa Mkoa wa Lindi. Ninaishauri sasa Wizara itekeleze Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa Mkoa wa Lindi ili kuainisha maeneo mahsusi yatakayotumika kwa mifugo kwa kutenganisha shughuli za ufugaji na shughuli za kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna athari kubwa ya uharibifu wa ardhi endapo mifugo itaendelea kufugwa kiholela bila kuwa na utaratibu na maeneo mahsusi, ikiwemo uharibifu wa mazingira, ardhi kupoteza rutuba ya asili kwa matumizi ya kilimo, lakini athari mbaya zaidi ambayo inaendelea hadi hivi sasa ni kuwepo kwa migogoro ya wananchi hivyo kukosekana kwa amani baina ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba jukumu hili lisiachiwe halmashauri za wilaya bali Wizara hii ijikite kuainisha maeneo ya matumizi ya ufugaji sambamba na maeneo yatakayofaa kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata nyama, viwanda vya ngozi na kadhalika, hii itasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi kwa jamii, kwani ajira itaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo ninaitakia utekelezaji mwema wa bajeti ya mwaka 2026/2027 nikiamini kwamba kwa umakini na umahiri wa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri ushauri huu utapokelewa kwa mikono miwili. Nawasilisha.