Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kushiriki mkutano huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbele yetu kuna hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2026/2027, hotuba hii ni nzuri na nitumie fursa hii kuipongeza Wizara kwa kuandaa hotuba yenye mwelekeo mzuri. Mheshimiwa Spika, Naomba kuchangia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2026/2027 nikiangazia mambo kadhaa, hasa namna ya uandaaji wa mipango miji, ni wajibu wa Serikali kuwa na mipango miji yenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inasema eneo la Masaki na Oysterbay ujenzi wowote utakaofanyika usizidi ghorofa nne, lakini kumekuwepo na baadhi ya watu wengine wamejenga ghorofa zaidi ya nne huku wengine wakikosa fursa hiyo, hali hii inapelekea wananchi kuona kuna double standard, aidha kwa mustakabali wa maendeleo na dunia ilipo sasa sheria hiyo ni ya kizamani ukizingatia maeneo hayo niliyoyataja ni maeneo mazuri kiuwekezaji na wawekezaji wananunua maeneo hayo kwa gharama kubwa, hivyo kumwambia mwekezaji ajenge ghorofa nne tu kunasababisha mwekezaji huyu kupata hasara kwani itamchukua muda mrefu kurejesha fedha zake alizowekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ibadilishe mfumo huu na watu wanaotaka kujenga wangepewa uhuru wajenge majengo marefu ya kisasa na kusiwe na double standard, Masaki na Oysterbay ni maeneo yanayohitaji majengo ya kisasa kiuwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tuhakikishe mipango yetu inakuwa madhubuti na ya kimkakati na kuendana na wakati wa sasa hasa kutenga maeneo maalum ya biashara na sio kuruhusu kila eneo mtu afanye anachotaka, kwa maeneo kama ya Mbweni ambayo kwa sasa ukuaji wake ni mkubwa, ni vema kuchukua tahadhari mapema kwa mamlaka husika kuzingatia mipango miji ya kisasa yenye taswira. Dar es Salaam na Dodoma ni miji miwili ya kimkakati zaidi nchini. Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na bandari, Dodoma ni makao makuu ya nchi, lakini miji yote miwili inakabiliwa na msongamano wa ardhi, makazi yasiyo rasmi na changamoto za mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka wa fedha 2026/2027, naziangazia changamoto na mapendekezo ya utekelezaji.
Kuhusu uhaba wa nyumba za gharama nafuu; Dar es Salaam ina upungufu wa nyumba zaidi ya 500,000. NHC imejenga nyumba nyingi, lakini nyingi ni za bei juu shilingi milioni 80 hadi 300. Mwalimu, askari na mhudumu wa afya hawawezi kumudu. Matokeo yake wanapanga Tandale kwa shilingi 200,000 chumba kimoja kisicho na choo cha ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Dodoma makao makuu ya nchi; tangu Serikali ihamie Dodoma bei ya kiwanja 20x20 Nzuguni, Ihumwa na Mkonze imepanda kutoka shilingi milioni mbili mwaka 2016 hadi shilingi milioni 25 kwa sasa. Wafanyabiashara wananunua viwanja vingi na kuvilaza wakiota faida. Mwalimu, daktari na polisi hawawezi kumudu kununua. Matokeo yake wanapanga mbali na maeneo ya kazi na wanachelewa kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji Kampeni ya Kitaifa ya Urasimishaji, Wizara itenge fedha kwa ajili ya kurasimisha mitaa 200 ya Dar es Salaam kwa mwaka 2026/2027. Kila mwananchi alipie shilingi 100,000 tu kupata Hati ya Hakimiliki ya Mazoea. Lengo ni kutoa hati 300,000. Hati hizi zitumike kukopa benki kuboresha nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Dodoma udhibiti wa bei ya ardhi na kufuta viwanja vilivyolala; Bunge litunge sheria ya kodi ya ardhi tupu. Mtu mwenye kiwanja zaidi ya miaka mitatu bila kukiendeleza alipe faini ya 5% ya thamani ya kiwanja kila mwaka. Hii itawafanya hao wanaomiliki viwanja hivyo ama wauze au wajenge kwa maana ya kuviendeleza. Pia Serikali ipange bei elekezi ya viwanja maeneo ya Nzuguni na Ihumwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kibaha Vijijini ni lango kuu la kibiashara na uwekezaji, mipango miji na ardhi ni sehemu muhimu kimkakati. Wizara hii ndiyo msingi wa maendeleo yote. Bila hati miliki, hakuna mkopo benki, bila mipango miji, hakuna TAMCO itakayokua, bila makazi bora, hakuna nguvu kazi yenye afya. Kibaha Vijijini ni lango la Mkoa wa Pwani na tunashuhudia kasi ya ukuaji kutokana na TAMCO, Expressway na Bandari Kavu ya Kwala, lakini kasi hiyo inaleta msongamano wa ardhi na changamoto za makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuainisha mahitaji ya msingi ya Jimbo la Kibaha Vijijini katika sekta hii ya ardhi na makazi.
(a) Upimaji na umilikishaji wa ardhi; zaidi ya 70% ya wananchi bado wanamiliki ardhi kimila bila hati. Kata za Gwata, Bokomnemela na Dutumi zina mashamba makubwa ya wakulima wadogo wa muhogo, mpunga na korosho, lakini wakulima hawawezi kukopa benki kwa sababu hawana hati za hakimiliki ya kimila. Pia wawekezaji wanaokuja TAMCO wanataka maeneo ya viwanda vya malighafi Ruvu na Kwala, lakini wanakwama kwa migogoro ya mipaka. Mahitaji ya haraka ni kupima vijiji vyote na kutoa hati za hakimiliki ya kimila zisizopungua 15,000 kwa mwaka 2026/2027.
(b) Mipango ya matumizi ya ardhi na mipango miji; Mlandizi, Ruvu na Kwala zinakua kwa kasi sana. Mlandizi sasa ni mji mdogo lakini unakua bila mpango kabambe. Viwanda vidogo vinajengwa karibu na shule, nyumba za makazi zinajengwa kwenye njia za maji, na stendi ya zamani imejaa. Tunahitaji master plan ya Mlandizi kutengwe eneo maalum la kibiashara, kujengwe jengo ambalo kutakuwa na frame za biashara na eneo hilo liwe kitovu cha biashara, watu wote wakitaka mahitaji muhimu wanakwenda hapo, hii itaondoa uholela wa kila eneo watu kufanya biashara na kupoteza taswira ya mji wetu, Ruvu Kijiji na Kwala inayobainisha maeneo ya viwanda, biashara, makazi, kilimo na hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunahitaji mpango kabambe wa maeneo ya jumla kwa vijiji vyote ili kutenganisha maeneo ya malisho, kilimo na makazi kupunguza migogoro.
(c) Nyumba za gharama nafuu kwa wafanyakazi wa TAMCO na walimu, wafanyakazi wa umma na wananchi wa kawaida; TAMCO ina ajira 853 na itaongezeka hadi 2,000 ifikapo mwaka 2027 kwa kuingia kwa Hyundai na Goodlife, lakini wafanyakazi wengi wanapanga Mlandizi kwa kodi kubwa ya shilingi 80,000 hadi shilingi 150,000 kwa chumba. Walimu wa Shule za Ruvu Sekondari na Mlandizi A nao wanakosa nyumba za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji Mradi wa Shirika la Nyumba (NHC) kujenga nyumba 500 za gharama nafuu Mlandizi na Kwala. Nyumba hizi zitapangishwa kwa shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000 kwa mwezi.
(d) Ofisi za Ardhi na huduma kusogeza karibu; wananchi wa Gwata wanalazimika kusafiri zaidi ya kilometa 45 hadi Ofisi ya Ardhi Kibaha Mjini. Mafaili kupotea, gharama za usafiri na urasimu unakithiri. Tunahitaji Ofisi ya Ardhi ya Wilaya Ndogo kufunguliwa Mlandizi. Ofisi hiyo iwe na huduma zote za upimaji, hati, uthamini na usajili.
(e) Hifadhi ya ardhi ya umma na maeneo ya wazi; kwa sababu ya kasi ya ujenzi, maeneo ya wazi, viwanja vya michezo na hifadhi za mazingira yanavamiwa, Mto Ruvu unaendelea kuvamiwa. Tunahitaji Wizara itamke wazi maeneo ya hifadhi na kuyapima ili kuyakinga na sheria kali zitumike kwa yeyote atakaekiuka ili iwe mfano kwa wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali kwenye Wizara hii hasa kuhakikisha makazi bora, pamoja na masuala mazima ya ardhi, ila sisi watu wa Kibaha Vijijini tunazo changamoto kadhaa tunazokabiliana nazo, naomba Wizara wazitafutie ufumbuzi kwa upana wake na kuja na suluhisho la haraka, changamoto hizo ni kama ifuatavyo:-
(a) Migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji; Kata za Dutumi na Bokomnemela zimeripoti migogoro mikali kati ya wakulima wa muhogo na wafugaji wanaohama Rufiji. Pia wawekezaji wanaotaka kununua ekari 500+ kwa kilimo cha kisasa wanashindwa kwa sababu mipaka ya kijiji na kijiji haijulikani. Mahakama ya Ardhi iko Kibaha Mjini na kesi zinachelewa miaka mitatu hadi mitano. Matokeo yake ni mapigano na kupoteza uzalishaji.
(b) Uvamizi wa ardhi na ujenzi holela; kwa sababu Mlandizi haina mpango kabambe, watu wanajenga kiholela. Njia za maji zimezibwa na ndio sababu Mlandizi inapata mafuriko kila mvua. Pia wawekezaji wa TAMCO wanalalamika kuwa wanapimiwa viwanja lakini majirani wanavivamia kabla ya ujenzi. Kamati za Ardhi za Vijiji hazina uwezo wa kudhibiti kwa sababu hazina ramani rasmi.
(c) Gharama kubwa za upimaji na hati; mwananchi wa kawaida anatakiwa kulipa kati ya shilingi 250,000 hadi shilingi 400,000 kupima kiwanja na kupata hati. Hii ni kubwa kwa mkulima wa kijijini. Matokeo yake wananchi nane kati ya 10 wanaamua kuendelea kumiliki kimila. Benki zinawakataa wakikopa kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha korosho.
(d) Ucheleweshaji wa fidha kwa miradi ya maendeleo; Mradi wa Expressway, Bandari Kavu ya Kwala na upanuzi wa TAMCO yote yalihitaji wananchi kupisha mradi. Baadhi ya wananchi bado hawajalipwa fidia zao tangu mwaka 2024. Hii inajenga chuki kati ya wananchi na Serikali na inachelewesha miradi. Pia tathmini ya mali inafanywa bila mwananchi kushirikishwa ipasavyo.
(e) Ukosefu wa wataalam wa sekta ya ardhi ngazi ya kijiji; kila kijiji kinatakiwa kuwa na Kamati ya Ardhi ya Kijiji na Mtaalam wa Ardhi, lakini Kibaha Vijijini tuna Maafisa Ardhi wanne tu kwa vijiji vyote ambao hawawezi kufika kila mahali. Matokeo yake, Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji yanatoa maamuzi yenye makosa na migogoro inaongezeka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri wangu wa kina kwa Serikali ifanye nini ili kuboresha sekta hii Jimbo la Kibaha Vijijini.
(a) Kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi:-
(i) Zindua Operesheni Hati Kijiji 2026; tenga shilingi bilioni 1.8 kwa mwaka 2026/2027 kupima vijiji vyote vya Kibaha Vijijini na kutoa Hati za Hakimiliki ya Kimila 20,000. Ruzuku, gharama kwa wananchi walipie shilingi 50,000 tu badala ya shilingi 300,000.
(ii) Kamilisha mipango kabambe; maliza master plan ya Mlandizi, Ruvu na Kwala kabla ya Juni, 2027. Kataza ujenzi wowote mpya bila kibali cha Mipango Miji kuanzia Januari, 2027.
(iii) Jenga Ofisi ya Ardhi Mlandizi; Wizara itenge fedha kujenga na kuanza Ofisi ya Ardhi ya Wilaya Ndogo Mlandizi. Iwe na maafisa nane, gari moja na vifaa vya kisasa vya upimaji vya GPS RTK.
(iv) Nyumba za NHC; agiza NHC ianze mradi wa nyumba 500 za gharama nafuu Mlandizi na Kwala. Serikali itoe ardhi bure na NHC ijenga. Nyumba hizi zikodishwe kwa wafanyakazi wa TAMCO na walimu na watumishi wengine wa umma pamoja na wananchi wa kawaida.
(v) Serikali imalize malipo ya fidia; hakikisha wananchi wote waliopisha miradi ya Expressway, Kwala na TAMCO wamelipwa kabla ya Desemba, 2026. Unda dawati maalum la malalamiko Mlandizi ili kusaidia usikilizwaji wa malalamiko na Wizara iweze kuyapatia ufumbuzi.
(vi) Tupunguze siasa kwenye migogoro ya ardhi; ili ardhi iendelee kuwa bora ni lazima tukubaliane kupunguza siasa na kuwaachia watendaji wafanye kazi zao.
(vii) Boresha maslahi ya watumishi; ili kuepuka vitendo vya rushwa Serikali iboreshe maslahi ya watumishi kwenye sekta hii, kwa kuwapa extra duty itasaidia sana kupunguza rushwa na kusaidia utendaji wa kazi usiotia shaka.
(b) Kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Halmashauri ya Kibaha:-
(i) Kwa kushirikiana na Wizara ajiri wataalam; ajiri Maafisa Ardhi 10, Maafisa Mipango Miji wanne, na Wapima sita ili kila kata iwe na afisa wake.
(ii) Kwa kushirikiana na Wizara, tenga maeneo ya wazi; halmashauri itamke na kupima maeneo yote ya wazi, viwanja vya michezo na hifadhi ya Mto Ruvu. Wavamizi wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho na onyo kwa wengine.
(iii) Baraza la Ardhi la Wilaya; anzisha Baraza la Ardhi la Wilaya linalokaa Mlandizi mara moja kwa mwezi kupunguza kesi zinazopelekwa Kibaha Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi ni uhai, kama hatutapanga vizuri sasa, miaka mitano ijayo Mlandizi itakuwa na msongamano usiopitika, wakulima watakuwa hawana mashamba na TAMCO itakosa ardhi ya kupanuka. Tukitekeleza ushauri huu, Kibaha Vijijini itakuwa mfano wa Tanzania ya Viwanda yenye mipango miji bora na wananchi wenye hati mikononi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.