Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Tinnar Andrew Chenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nichangie mambo machache kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. Serikali ije na mpango madhubuti wa kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kusiwe na mwingiliano wa matumizi na jambo hili lisimamiwe na ikiwezekana litungiwe sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna ujenzi holela, Serikali ije na mpango wa kutenganisha matumizi ya maeneo kwa mfano kuwe na eneo ambalo litaruhusu nyumba za kawaida (bungalows) na hapa haitaruhusiwa kujenga ghorofa, kuwe na eneo la kujenga ghorofa moja, vivyo hivyo na eneo la kujenga zaidi ya ghorofa moja. Sasa hivi maeneo ambayo yaliitwa low density kama Oysterbay yamegeuzwa kuwa maeneo ya high density kutokana na utitiri wa maghorofa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwe na housing colour code hasa kwenye majiji makubwa ili kupandisha hadhi maeneo. Aidha, kumekuwa na maombi ya kubadilisha matumizi ya ardhi na vibali vimekuwa vinatolewa. Niombe eneo hili pia liangaliwe kwa umakini maana sasa hivi katika mji wa Dar es Salaam kunajengwa petrol stations nyingi kwenye maeneo ya makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja vinavyopimwa kwa sasa vizingatie kuacha maeneo mahsusi ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia kunapotokea migogoro ya watu kuvamia eneo la mtu ambalo tayari lina hati halali, basi Serikali ichukue hatua ya kumlinda mwenye hati halali, kwani kwa sasa wamiliki halali wamejikuta wakihangaika wenyewe mahakamani huku Wizara ikiwa kimya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu Maafisa wa Ardhi ambao wanakuwa chanzo cha migogoro ya ardhi badala ya kuwahamisha toka kituo kimoja kwenda kituo kingine kwani huko ni kutoa ugonjwa eneo moja na kuuhamishia eneo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha wa Serikali huwa unaanza tarehe 01 Julai mpaka tarehe 30 Juni ya mwaka unaofuata, ninashauri hapa hata kwenye malipo ya kodi ya pango kanuni hii ifuatwe kama ambavyo walipa kodi wote wanavyolipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ije na mpango kujenga nyumba za bei nafuu kwa watu wa kawaida maana hizi zinazojengwa kwa sasa bado ni ghali sana hasa ukilinganisha na pato la watu wetu. Mpango uliopo haujawanufaisha wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itoe elimu juu ya matumizi ya nyaraka za ardhi. Mfano nini maana ya town plan (TP), je, town plan ni nyaraka inayompa mtu umiliki wa ardhi au ni nyaraka inayoelezea mpango mji maana kuna watu wanaamini town plan (TP) ni nyaraka ya umiliki wa eneo.

Pia Serikali iangalie upya Mabaraza ya Ardhi kwani kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu utendaji kazi wao na hasa yale ya kata. Aisha, Serikali iyalinde maeneo ambayo yalitengwa kwa madhumuni mahsusi mfano open space, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya huduma maalum mfano masoko. Kumekuwa na uvamizi wa maeneo haya au watumishi wa ardhi kuyamilikisha maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa mipango miji siku zijazo wanapotenga maeneo ya barabara wazingatie kuweka provision ya lane ya ambulance na magari ya Zimamoto maana tunaona jinsi ilivyo shida kwa ambulance kuwafikisha wagonjwa mahututi hospitalini au janga la moto linapotokea gari la Zimamoto kufika kwa wakati ni kipengele kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali ije na mpango wa matumizi sahihi ya ardhi kwa kutenga maeneo yatakayotumika kama makazi, shule, hospitali, masoko, nyumba za ibada, nyumba za burudani, viwanja vya michezo na kadhalika, kwani ilivyo sasa unakuta baa iko katikati ya eneo la makazi, ili makosa yaliyofanyika huko nyuma yasijirudie, tujifunze kutoka kwa jirani zetu Rwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Dar es Salaam kama inawezekana ambulance na gari za Zimamoto kwa sasa ziruhusiwe kupita kwenye lane ya mwendokasi kunapotokea dharura ili kupunguza majanga maana kwa sasa haiwezekani kujenga hizo lane kutokana na ufinyu wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yatakayotumika kama makaburi nayo yapangiliwe vizuri kwani kwa sasa maeneo hayo maziko hufanyika kiholela bila kuzingatia kuacha nafasi kuruhusu watu kupita wanapoenda mazikoni. Kuwekwe distance kati ya kaburi na kaburi ili kuruhusu watu wanapokuja kuzika waweze kupitisha majeneza kwa urahisi.