Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza siku ya leo niweze kuchangia hii Hotuba ya Wizara ya Afya ambayo ni Wizara muhimu sana kwa Taifa, na kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uzima, nimeweza kusimama hapa siku ya leo kuchangia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli anafanya kazi kubwa na nzuri kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora na siyo bora huduma. Kwa kweli tunampongeza mama na mimi binafsi naendelea kumwombea, Mwenyezi Mungu ambariki, amjalie afya njema aweze kuendelea kutupambania sisi Watanzania, na sisi tuko nyuma yake tunamsaidia katika majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Afya, kaka yangu, ndugu yangu Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu wake dada yangu Dkt. Samizi kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya kwenye Wizara bila kumsahau Katibu Mkuu kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa simtendei haki Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kitete Tabora, huyu ndiye ambaye nimekuwa nikifanya naye kazi kwa karibu sana kipindi chote, na hata ninapokuwa sipo, Ofisi yangu imekuwa ikifanya naye kazi kwa karibu mno kuhusiana na changamoto za wananchi katika Jimbo la Tabora Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka Hospitali ya Kitete ni Hospitali ya Mkoa, lakini iko kwenye Jimbo la Tabora Mjini. Kwa hiyo, ninafanya nayo kazi kwa karibu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo mimi ninaomba niseme maneno machache kuhusiana na hii Wizara ya Afya. Pamoja na pongezi nilizowapa, nilikuwa ninaomba sana pamoja na yote, mnafahamu kila siku kilio chetu kikubwa hospitali yetu imekuwa ni hospitali ya muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya kitete imeanzishwa mwaka 1906, wakati huo wale wenzetu walikuwa wakipata majeraha, au nini, wanapelekwa pale. Majengo ya hospitali ile kwa kweli siyo rafiki sana. Ningeomba sana, Serikali imesema itafanya structure mpya kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya pale katika Hospitali ya Kitete. Kila nikiangalia naona kama bado tunahitaji hospitali na tunahitaji eneo kubwa ili kuweza kujenga hospitali yenye hadhi ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtakumbuka, Tabora tuna watu zaidi ya milioni tatu ambao wengi wanategemea hospitali ile, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa huduma mbalimbali katika hospitali ile. Watu wakifika pale wengine wanaambiwa nendeni Bugando, wengine wanaambiwa nendeni Benjamini Mkapa. Kwa kweli hii hali siyo sawasawa kabisa
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji sisi kama watu wa Tabora ni kuhakikisha huduma zote zinapatikana katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, kwa sababu kuna watu wengi, na wengi wanahitaji huduma, na wananchi wanatufuata sana kutuuliza ni kwa namna gani ambavyo mtaweza kuboresha huduma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa kwa ajili ya kumalizia jengo la Mama na Mtoto. Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka hiki ni kilio changu cha muda mrefu. Ninajua watakavyokuja kutujibu hapa kutakuwa kuna majibu mazuri na sisi watu wa Tabora tupate kupumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa jengo la ICU kwa ajili ya watoto. Ninamwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri, jengo hili ujenzi wake umeshaanza, lakini fedha zipelekwe kwa wakati ili jengo hili liweze kukamilika kwa wakati kama ambavyo wametuahidi sisi watu wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Yambe kwa kazi kubwa anayoifanya, amekuwa akitumia mapato ya ndani kuhakikisha kwamba anaboresha changamoto zinazopatikana pale kwenye hospitali yetu. Ameweza kuboresha baadhi ya majengo ya wodi, lakini pia ameweza kununua vifaa tiba vya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pale katika Hospitali ya Kitete ameweza kutuwekea gym kuhakikisha kwamba yale magonjwa yasiyoambukiza yanapungua kwa watu kuweza kufanya mazoea ya kufanya mazoezi ili kuweza kuondoa ama kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie kuhusiana na suala zima la Bima ya Afya. Kwanza kabisa, ninampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake thabiti wa kuhakikisha kwamba Watanzania wote tunakuwa na Bima za Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kwamba kila mara sisi Wabunge tumekuwa tukipata changamoto za wananchi wetu kupata maradhi na mwisho wa siku kuwa hawana uwezo wa kwenda kupata huduma. Tumekuwa tukiwasaidia kwa matibabu mara kwa mara, lakini Mheshimiwa Rais ametuletea hii Bima ya Afya na sisi Wabunge tumuunge mkono kwa kuhakikisha tunashauri vizuri katika suala zima la Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu ni kwa namna gani Serikali inapambana kuhakikisha wana-finance hii Bima ya Afya. Hata hivyo, kunakuwa kuna changamoto. Niwaambie Wizara, wananchi wa Tanzania wako tayari kuchangia hii Bima ya Afya lakini ambacho wanakutana nacho ni cha upungufu wa vifaa tiba, na upungufu wa dawa kidogo, kinawachanganya. Wanaona akienda pale na bima yake hata panadol anambiwa nenda kanunue nje. Hili jambo siyo sahihi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana na ninaishauri Serikali kuhakikisha kwamba, kwa mfano kwa sasa hivi kuna vijana ambao wana mtandao wao, na jana nilikuwa nikimsikia kaka yangu hapa Mheshimiwa Kingu amezungumzia jambo hili, na mimi ninaomba niungane naye kwa dhati ya moyo wangu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana ambao wana platform yao kupitia mobile network; Wizara ingeamua kujiunga katika hii mobile network na wao wakawa na akaunti yao maalumu kuhakikisha kwamba Watanzania (wananchi) wanachangia kidogo kidogo ili kuweza kupata huduma bora za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu Serikali ina mambo mengi, ina changamoto nyingi. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba ikifanya hivi, itakusanya fedha nyingi ili kusaidia huduma bora za afya na siyo bora huduma na wananchi wengi huko kabisa watajiunga katika hii Bima ya Afya katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?
MWENYEKITI: Mheshimiwa ndiyo muda wako umekwisha.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika tano?
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha, unga mkono hoja.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)