Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi. Nilikuwa nimejiandaa kuchangia kwa dakika 10, lakini nitazingatia maelekezo ya Kiti. Mambo tunayochangia hapa ni mambo ambayo ama tumekutana nayo au tunapata kutoka kwa wananchi wetu katika maisha ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, la kwanza ningependa niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Afya amekuwa anafanya kazi nzuri, na Jimbo la Tarime Vijijini ameacha alama tangu amefanya ziara akiwa Waziri wa Maliasili. Kwa Wabunge wengi hawana wasiwasi na uwezo wake mahali popote ambapo amepelekwa amekuwa bulldozer, anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nisaidiwe, sisi Wabunge hapa tuna bima, maana unaanza kujitetea wewe mwenyewe halafu unaenda maeneo mengine. Wabunge hapa tunapata huduma ya bima kwa maana ya Mbunge, mke au mume na watoto, lakini wazazi wetu hawamo kwenye ile bima. Nimekaa hapa kipindi chote sijapata maelezo ya maana kwa nini Wabunge wazazi wetu hawatibiwi na bima hii ambayo tunapata hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Wabunge hapa vijana wengine hawajaolewa, wengine hawajaoa, wengine ni wagane na wengine ni wajane. Kuna watu ambao wana wazazi wao ambao watoto wao hao vijana waliopo humu Bungeni nikiwepo na mimi, wazazi wetu walilima kahawa, wakawinda wanyama tukasomeshwa, lakini mzazi anagua, Mbunge anahangaika na mzazi wake. Hili jambo limeleta taharuki katika familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni sababu gani imezuia Wabunge wazazi wetu wasitibiwe kwa bima zetu? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wagonjwa wakienda hospitalini wanaenda kumwona daktari, kuna kitu kinaitwa consultation fee, yaani ili Mganga amsikilize, analipia. Sasa mgonjwa huyu akishamaliza kupata maelezo ya daktari, anaenda pale dirishani anatakiwa achangie gharama ya matibabu, fedha ile ameshamaliza. Hawa watumishi madaktari wanalipwa na kodi za Watanzania hawa hawa; ni sawa na walimu, sawa na watumishi wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mgonjwa alipe fedha ndiyo aelezwe ugonjwa wake? Kwa nini isigeuzwe, mgonjwa akishaelezwa ugonjwa wake aende dukani, fedha aliyonayo achangie matibabu? Kwa hiyo, ningeomba jambo hili Mheshimiwa Waziri pia uliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Jimbo la Tarime Vijijini watumishi waliopo ni 36.9% tu, zaidi ya 60% hakuna watumishi katika maeneo yale. Tuna vituo vya afya kama Mtana miaka mitatu sasa; Bumela, Sirari, Magoma, Gibaso, Kerende hivi vituo vyote vya afya vimekamilika, ni majengo yako pale buibui ndiyo wanaishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri anisaidie namna ya kufanya kazi. Kituo cha afya kisifanye kazi ya zanati na wananchi wa Tarime Vijijini wasiendelee kuangalia majengo badala ya kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni Hospitali ya Rufaa ya Musoma, kwa Baba wa Taifa. Tunapozungumza, kuna mkataba waliingia mwaka 2024 wa shilingi 14,000,000,000, Mkandarasi amelipwa shilingi 4,000,000,000 tu. Majengo ambayo yanatakiwa kujengwa pale ni muhimu sana. Yaani kule hakuna huduma ya macho, hakuna huduma ya meno, hakuna huduma ya mionzi, hakuna wodi za wagonjwa na mkandarasi anafanya kazi hajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri atoe hadhi na heshima kubwa kwa Mkoa wa Mara. Wagonjwa wa Mkoa wa Mara wanatumia gharama kubwa kwenda Bugando siku hizi, kuja Benjamin Mkapa na kwenda Muhimbili kwa sababu ya huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule Mandarasi Prince Limited apewe fedha yake ile hospitali ikamilike. Mnavyozungumza utalii wa kimatibabu ni pamoja na Mkoa wa Mara; ukitibiwa, umepona, kabla ya kurudi ulikotoka unaenda Butiama kwa Baba wa Taifa unaangalia mandhari, halafu unarudi kwako. Kwa hiyo, ninaomba utusaidie kwenye huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ana mipango mizuri ya kuboresha Muhimbili. Sina shida na hiyo, lakini ninashauri ikiwezekana kupeleka huduma hizi, magonjwa mengine ni ya kawaida tu. Unaenda kwenye zahanati, hata ule mzani wa kupima mtoto tu uzito wake haipo. Hata mabenchi hayapo! Tuboreshe huduma kwenye zahanati, kwenye kituo cha afya, tuboreshe huduma halmashauri za wilaya, huduma za hospitali za rufaa za Mikoa, msangamano wa hospitali kubwa hizi utapungua. Tukifanya hivyo, itasaidia Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana kwa kazi. Nimeanza kusema Waziri hajawahi kushindwa kwenye Wizara yoyote. Anafanya kazi nzuri, lakini atusaidie kutoa huduma ambayo ni nzuri na Hospitali ya Muhimbili, tunaunga mkono kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshauri Mheshimiwa Waziri, pamoja na majengo ya ghorofa, tuwekeze kwenye utaalamu bobezi. Tuwekeze kwenye vifaatiba katika maeneo yetu, hata kama itakuwa chini ya mti, lakini kifaa kikifanya kazi, watu wakapata huduma ya matibabu, Mheshimiwa Waziri atakuwa ameacha alama kwa Watanzania na itamsaidia Mheshimiwa Rais kusaidia huduma za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)