Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kunipa nafasi hii ya kuchangia. Ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kuniwezesha kusimama katika Bunge lako Tukufu kuchangia Bajeti ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru Magharibi kwa kutoa kura nyingi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na pia kwa kunipa kura nyingi, leo imesababisha nisimame hapa kuongea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kuishukuru Wizara ya Afya kwa ujumla kwa kazi nzuri. Jana Mheshimiwa Nkingwa amemsema Waziri Mchengerwa, lakini Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kweli ni mzalendo, amewasilisha vizuri. Huyu ni mzalendo kweli, amenitembelea, amefanya ziara katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Alipofika, ameweza kusaidia kupatikana kwa barabara ya lami kama kilometa mbili hivi kwenda hospitali ya wilaya. Pia, ameshuhudia uwekezaji wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hospitali la wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu ni mzalendo na wananchi wanampenda kweli. Ameahidi kwamba, atapeleka ambulance katika hilo Jimbo la Arumeru Magharibi. Watumishi wale ambao wamepungua atahakikisha kwamba, wanapatikana ili waweze kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema dakika sita tu. Ninaomba ni-declare interest, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Ninaomba unipendelee dakika 10, kama jana walivyokuwa wanafanya, ili niongee kidogo tu, kama utaridhia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wengi jana wamechangia kuhusu Bajeti ya Afya. Ninawapongeza sana kwa kuchangia kuhusu Hospitali ya Muhimbili. Sina haja ya kurudia, ninawapongeza tu Waheshimiwa Wabunge, huu ni mradi mkubwa, ambao utaenda kubadilisha sura ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Muhimbili itapata ithibati ya Kimataifa. Kwa hiyo, tutaimarisha utalii, tunaita Tiba Utalii katika hospitali yetu, tutaimarisha mafunzo ya madaktari wetu, tutaimarisha tafiti katika nchi hii na tiba ya kisasa kutokana na mitambo mikubwa, ambayo imewekezwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaenda kutumika katika hospitali hii. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwamba mmeunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia na Mheshimiwa Dkt. Samizi, amekuwa kiungo kizuri sana, tulipotembelea na kufanya ziara, akiongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa. Ninashukuru kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya imefanya kazi nzuri sana kwenye kinga. Ukiangalia suala la homa ya ini na shughuli nyingine wamefanya kazi nzuri, nawapongeza, lakini ninasema hivi tuimarishe kinga, Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana amesema Mheshimiwa Mahera, tuelekeze kwenye primary health care, ambako ndiko kuna hospitali ya wilaya, kuna vituo vya afya na kuna zahanati, watu wako kule kwa wingi. Ikiwezekana kama bajeti itaruhusu, hebu tuendeleze kuimarisha vituo vya afya. Akina mama wengi sasa hivi ndiyo wanajifungulia kule, tuimarishe kwa vifaa na kwa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimeomba dakika 10 kwa sababu, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati, nimalize tu. Kwa hiyo, ninaomba hilo la kinga Mheshimiwa Waziri lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nitakuwa sijatenda haki nisipoongea kuhusu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya nini katika nchi hii? Ndiyo nikakuomba hizo dakika tatu hivi nimalizie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi katika nchi hii. Kwanza kabisa ukiangalia hospitali za Wilaya, amejenga hospitali 119, vituo vya afya 649, zahanati 2,700, ajira mpya 5,000, watumishi wa afya na madaktari bingwa na bobezi amewasomesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakuishia pale, katika vifaa vya tiba, ninaomba tusikilize tu kidogo; ukiangalia MRI, mnasikia watu wanasema, amekuta saba, amepeleka mpaka 13; CT-Scan amekuta 13, sasa hivi ziko 45; Ultrasound amekuta 476, sasa hivi ziko 970. Cath Lab ni mtambo mkubwa wa kupasua moyo kwa matundu madogo na mishipa ya damu, amekuta mbili sasa hivi ziko nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu uvumilie kidogo. Digital X-Ray, zile za kisasa kabisa, unajua mambo aliyofanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni vyema Watanzania wafahamu na tunasemea hapa. Kuna Min Lab nzuri sana ziko nne, lakini PET Scan ameleta Hospitali ya Ocean Road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nivumilie dakika moja. Ukiangalia Hospitali ya…
(Hapa, Kengele Ililia Kuashiria kwisha kwa Muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ninakushukuru sana. (Makofi)