Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara ya Afya. Awali ya yote, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Dkt. Samizi, kwa kazi nzuri wanayofanya. Mimi nakiri kwamba Mheshimiwa Waziri ni mfano bora wa uwajibikaji katika Sekta ya Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, ninaomba kipekee nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Yako mambo mengi ambayo ameyafanya ndani ya Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, Mkoa wa Songwe ulikuwa ni mpya, lakini ndani ya miaka mitano ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumepata hospitali ya mkoa, inafanya kazi; tumepata Hospitali ya Wilaya ya Songwe, imekamilika inafanya kazi; tumepata hospitali ya Mji wa Tunduma, inafanya kazi; na tumepata Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba, inafanya kazi. Vilevile tumepata jengo jipya la mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, jengo ambalo awali lilikuwa limechakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mafanikio haya makubwa ambayo Mkoa wa Songwe tumepata kupitia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yako mambo machache ambayo natamani niishauri Serikali ili iweze kuyafanyia kazi na kufikia malengo ambayo anataka wananchi wa Mkoa wa Songwe waweze kuyapata kwenye Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kwenye Hospitali yetu ya Mkoa wa Songwe. Hospitali ile pamoja na kwamba, inafanya kazi, lakini kuna changamoto ndogo, kwamba jengo la wanawake na watoto bado halijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bunge la Kumi na Mbili Wabunge wa Mkoa wa Songwe tuliomba Serikali iweze kutoa fedha ili kukamilisha jengo la mama na mtoto. Tunaishukuru sana Serikali kwa sababu, mwezi wa 10 mwaka 2025 ilituletea shilingi 3,000,000,000 ambazo kimsingi zimesaidia sana kujenga structure ya ghorofa tatu. Vilevile, zitasaidia sana kumalizia miundombinu yote ya floor ya kwanza, ambayo kimsingi tutapata pale operation room mbili kwa ajili ya wanawake, na vilevile itatusaidia kupata vyumba vitano vya wanawake kujifungulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kwenye Hospitali ya Mkoa wa Songwe. Bado shilingi 3,000,000,000 ambazo zikitolewa, zitasaidia sana kuweza kukamilisha jengo la mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Hospitali yetu ya Mji wa Tunduma, Mji wa Tunduma ni lango la SADC. Pale tunalo jengo la mama na mtoto ambalo kimsingi, bajeti yake ni shilingi bilioni 2.7, lakini mpaka sasa hivi, kwa masikitiko makubwa, tumepokea shilingi 300,000,000 tu ambazo zimetuwezesha kuanza kujenga msingi. Kwenye bajeti yetu ya mwaka huu imetengwa shilingi 100,000,000 ambayo kimsingi ni fedha ndogo, itachukua muda mrefu sana kuweza kukamilisha jengo la mama na mtoto kwenye Mji wa Tunduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Mji wa Tunduma ni lango la SADC. Tunaishukuru Serikali, ndani ya Awamu ya Tano tumepata vituo vya afya sita. Kwenye vituo hivyo, kituo kimoja cha afya cha Tunduma kinazalisha watoto 800 kwa mwezi, siyo kwa mwaka. Kituo kimoja cha Chapwa kinazalisha watoto 300 mpaka 400 kwa mwezi. Hospitali ya Mji wa Tunduma kwa mwezi inazalisha watoto 400 mpaka 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi hii ni kubwa sana kwa sababu, hospitali ile inahudumia siyo tu Watanzania, lakini pia watu kutoka kwenye Mataifa mengine. Ninaomba, changamoto kubwa ambayo inatukumba kwenye Mji wa Tunduma ni ukosefu wa watumishi. Watumishi wanaofanya kazi kwenye vituo vya afya hivi vipya vya Mji wa Tunduma wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Rais wetu kwa sababu, juzi ametoa kibali cha kuajiri watumishi 5,000. Tunashukuru kwa sababu, kwenye Wilaya ya Ileje mmetuletea watumishi, lakini bado kwenye Mji wa Tunduma hatujapata mtumishi hata mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, tunafahamu uwajibikaji wake, tunafahamu uchapakazi wake, ninaomba aangalie Mji wa Tunduma kwa jicho la tofauti. Bahati nzuri mtendaji wa Wizara hii alimewahi kuwa RAS wa Mkoa wa Songwe. Kaka yangu Shekilage ninamwomba sana, akumbuke Mkoa wa Songwe, aangalie Mji wa Tunduma kwa jicho la tofauti. Afanye atakavyofanya atuletee watumishi katika Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Hospitali ya Wilaya ya Momba, ambayo nayo imekamilika, tunashukuru. Jengo la Mama na Mtoto limekamilika na huduma pale zinaendelea, lakini bado tuna idadi ndogo sana ya watumishi. Tunahitaji vilevile kuweza kupata mtaalamu wa mionzi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka nizungumzie ni kuiunga mkono Serikali kwa jambo lake ambalo imeleta la kujenga upya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hospitali ile ni ya Taifa, siyo ya wilaya, siyo ya mkoa, siyo ya kanda, ni Hospitali ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na historia ya Hospitali ya Muhimbili ambayo muda hautoshi siwezi kuielezea, lakini kutokana na uchakavu wa miundobinu wa hospitali ile na msongamano wa watu, ninachelea kusema kwamba, sisi kama Taifa tumechelewa sana kuijenga Hospitali Mpya ya Muhimbili.

(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia namna gani ambavyo...

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, Hospitali ya Muhimbili itakamilika ndani ya miaka mitano. Tunatamani hii ndiyo iwe legacy, ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atatuachia Watanzania. Ndani ya miaka mitano tunaomba hospitali iweze kukamilika.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile waweze kutusaidia zile shilingi 3,000,000,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kumalizia Hospitali ya Mkoa wa Songwe. Tutakapopitipisha bajeti yake hapa leo, aweze kuzitoa hizo fedha na Hospitali yetu ya Mkoa wa Songwe iweze kukamika, ahsante. (Makofi)