Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JESCA Y. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali naenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuweza kufika hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkoa wa Dodoma tusiposema, tutakuwa wachoyo wa fadhila. Sisi Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametutendea haki sana. Ametutendea haki kwa majengo mazuri, kwa vituo vingi kutoka 2021 vituo 429, mpaka Aprili mwezi uliopita vituo 699. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunayo haja ya kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dodoma tunampongeza na tunamshukuru sana kwa kumwangalia mama na mtoto kwenye mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa vifo vya mama na mtoto katika Mkoa wa Dodoma, ameendelea kuwa kinara kwa kuwasaidia akina mama wa Mkoa wetu wa Dodoma. Amehakikisha mazingira mazuri ya mwanamke wakati anakwenda kujifungua kwa kutoa vifaatiba, na mazingira ambayo yanamfanya mwanamke awe comfortable.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale General Hospital sasa hivi ninaipongeza sana Wizara ya Afya, wameweza kuboresha, wameweka kitengo rasmi cha emergence, mwanamke akifika pale anaangaliwa huyu aende kwenye operesheni, au aende wapi? Kwa kweli wameboresha sana hospitali yetu ya General. Zamani ilikuwa changamoto ni kubwa, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto za watumishi, kwenye mkoa wetu, mahitaji ni makubwa sana ya watumishi wa afya. Tuna uhitaji wa watumishi wa afya 10,000 lakini sisi tuna watumishi 4,000. Unaenda kwenye hospitali za Wilaya unakuta Daktari mmoja anahudumia eneo kubwa mpaka unajiuliza, huyu Daktari anapumzika saa ngapi? Maana usiku unamkuta yeye, asubuhi unamkuta yeye. Kwa hiyo, changamoto hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana wale vijana ambao wamewapa ajira za kujitolea, basi wawapatie ajira hizi, kwa sababu wanajitolea muda mrefu kwenye idara hiyo, lakini hawapewi hizo nafasi za kwenda kuhudumu kama waajiriwa kwenye sekta hiyo ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, wapo vijana wetu kwenye Wilaya wanajitolea muda mrefu, miaka mitatu, minne wanajitolea, lakini wakija, wanaajiriwa wengine kwenye idara hiyo ya afya. Kwa hiyo, ninaomba sana kwenye idara hii ya ajira mtufikirie sana watumishi wa afya Mkoa wa Dodoma, ingawa tunashukuru, wapo, lakini tunaomba sana mtusaidie kutuongezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii sera ya matibabu bure, wenzangu wengi wamezungumza, na mimi nizungumze. Mkoa wangu wa Dodoma bado sera hii haitufikii vizuri wanawake. Unakwenda kujifungua, unaambiwa utalipia matibabu, lakini bado unaambiwa utajifungua kwa kuchangia na vifaatiba vingine. Utakuta mzigo ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke wa kijijini ukimwambia atoe shilingi 250,000 kwa operesheni ni fedha nyingi sana. Shilingi 250,000, bado atoe shilingi 250,000 hiyo, lakini bado anaambiwa alete na vifaa vingine! Tunaomba sana Wizara iangalie jambo hili. Jambo hili limekuwa likiwasumbua sana wanawake wakienda kujifungua. Jambo hili linafanya wanawake wengi wanajikuta sasa wanazalia nyumbani kitu ambacho siyo kizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko vijijini kwetu mtu anaona bora aende akazalie nyumbani. Ninaomba sana watuangalie Wizara ya Afya, hasa kwenye jambo hili la vifaatiba, kwani ni jambo ambalo mwanamke yeyote anatamani kujifungua akiwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya uhaba wa vitanda. Kuna maeneo, kwenye hospitali nyingine ukienda bado vitanda havitoshelezi kwa wanawake. Unakuta wanawake wengine bado wanajibanabana kwenye vile vitanda. Kwa hiyo, ninaomba Wizara iendelee kutufikiria katika kuboresha mazingira haya ya kumsaidia mama na mtoto, basi tuhakikishe kwamba vitanda vinatosheleza katika kumsaidia mwanamke kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)