Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaanza na neno la pongezi kwa Waziri wa Afya, babu yangu Mheshimiwa Mchengerwa. Pia ninampongeza Katibu Mkuu wake, na vilevile nisiache kumpongeza na Mganga wetu Mkuu, dada yangu. Ndugu yangu, Mheshimiwa Mchengerwa, Wizara yake imeenea na mambo yako meupe kama suti yake ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mkoa wetu wa Morogoro kwa ujumla kwa nchi hii ni Mkoa namba mbili kwa ukubwa. Kaka yangu, Mheshimiwa Mchengerwa anajua, mwaka 2023/2024 tulipokea ugeni wa Mheshimiwa Rais, alikuja, na nilisimama nikaomba kwa Mheshimiwa Rais kwamba hospitali yetu ya Mkoa wa Morogoro hali yake siyo nzuri, traffic ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna traffic kubwa, amezungumza jana kaka yangu Mheshimiwa Shabiby hapa, sawa tunapata huduma vizuri, lakini je, majengo yale mimi tangu mtoto yapo vilevile, ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa, kweli! Mimi ninamfahamu Waziri, ni mtu wa viwango, mtu wa vitendo, nikizungumza kwenye hili, ninajua nimemgusa moyo wake, ataenda kuiangalia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sisi tunaitazama SGR kama jambo kubwa sana....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Clayton Chipando, kwa mujibu wa Kanuni, hauruhusiwi kumkatisha msemaji, ninaomba urudi ulipotoka.
Mheshimiwa Hamisi Taletale, endelea. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sisi wakazi wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla tunaitazama SGR kama ndiyo jambo letu la utalii. Tunaangalia sisi wakazi wa Morogoro, hospitali tunayoitegemea, amezungumza dada yangu pale Mheshimiwa Juliana Shonza, ni Muhimbili. Muhimbili ni National Hospital, lakini siyo kila mtu anaweza akakodi ndege, siyo kila mtu anaweza akachukua ambulance kutoka Morogoro kwenda Muhimbili. Tuangalie leo hii tumeletewa SGR, kwa nini tusije na ambulance ndani ya ile SGR? Tunashindwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini Rais wetu ni msikivu, atalifanya hili kiurahisi. Tutengeneze, tufanye modern, vitu kama hivi wenzetu ng’ambo wanaweza, kwa nini tusiwe sisi? Je, lini linaweza kufanyika hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mdau mkubwa na mdau namba moja wa Hospitali ya Muhimbili. Kwa nini nasema hivyo? Mimi ni kama balozi wa ile hospitali. Nimemsikia Mheshimiwa Mchengerwa akizungumzia bajeti yake hapa; mimi sitakaa kumshikia shilingi, wala kushikia shilingi bajeti, ila ninaweza nikaomba ikiwezekana tuiongezee hata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Muhimbili ninaifahamu vizuri, wagonjwa wetu wanaotokea Morogoro vijijini wakitoka referral wanapelekwa Muhimbili. Sasa leo hii Muhimbili ina changamoto ya magari ya wagonjwa, ana ushahidi Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wagonjwa kutoka Muhimbili kwenda Mloganzila, kuna magari mawili tu. Kwa nini? Kwa nini tuna magari mawili? Labda wafanyakazi wake wanamwogopa kumwambia, aende akatembee Muhimbili, magari ya wagonjwa (ambulance) yapo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao ushahidi, juzi wakati ninahangaika na mwenzetu mmoja wa muziki, gari zipo mbili. Wagonjwa wapo wawili pale! Haiwezekani. Tuangalie nini kifanyike? Ninampongeza Mheshimiwa Mchengerwa, huko nyuma alishawahi kunipa mpaka gari la ambulance, basi nenda akaongeze ambulance Muhimbili. Hili kwetu linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, lakini siyo la umuhimu. Tunayo changamoto, amesema jana kaka yangu Mheshimiwa Shigongo hapa kuhusu homa ya ini. Hili gonjwa ni kubwa sana. Leo hii mtu akipata homa ya ini anakula RV kama vile ni chai. Sasa nani wa kututazama katika hili? Huko nyuma tulikuwa tunafanya chanjo pale Muhimbili, sijui kama mpaka leo bado ipo, lakini na ile awareness ya watu kujua kama kuna tatizo la ugonjwa wa homa ya ini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wanakufa na wengine wanakufa ghafla na stress kwa sababu akianza kutumia RV anajiona ooh! Kushnei (kwisha habari yake); lakini kama tunaweza kusimama kama Wizara ya Afya kwenda kuwaelimisha vijana, kuna shida na kuna changamoto la gonjwa la homa ya ini, hili litatusaidia na kupunguza namba ya maambukizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa huu una kinga kwa chanjo ya mara tatu. Mheshimiwa Mchengerwa sisi tunamwita Mtu Kazi. Mtu Kazi haswa, na kama nilivyosema mwanzo, suti yake nyeupe, ina kitu ndani yake. Aende akaokoe vijana, maana homa ya ini mtu akipiga chafya tu anaipata. Homa ya ini siyo mpaka watu wajamiiane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunajazana kwenye madaladala, tunajazana kwenye mwendokasi kwenye kugombea kuingia, mwisho wa siku watu tunaambukizana huu ugonjwa na watu hawafahamu kwa sababu hawana elimu. Hili jukumu linatoka wapi kama siyo kwa Wizara ya Afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchengerwa awaambie wataalam wake wasimame wainue Taifa. Taifa linaangamia kwa sababu ya kutokupata maarifa ya gonjwa la homa ya ini. Hili lipo chini ya Wizara ya Afya, tokeni simameni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa nikizungumza hili suala, na hata humu ndani kuna Wabunge hawajachanja chanjo ya homa ya ini. Basi tuletewe watu pale wachanje ili hili suala liishe. Tunaogopana hapa kwa sababu hili gonjwa lipo, na kama halipo, watu wanatakiwa wafahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya machache, ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa, hospitali yetu ya Wilaya inafanya kazi vizuri, lakini bado kuna changamoto ndogo ndogo. Niliongea vizuri na Mheshimiwa Katibu Mkuu, naomba ikipendeza waje Morogoro vijijini watutembelee. Ahsante sana.