Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mariam Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kwa dhati ya moyo wake kuweka fedha katika Hospitali ya Muhimbili. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa jambo hilo alilolifanya, ni jambo kubwa kwa afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Afya, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu, nitaanza na Hospitali ya Temeke. Hospitali hii ina idadi ya wagonjwa ambao wamepitia katika hospitali ile kwa mwaka 2005, wamefikia 605,772. Akina mama wajawazito walioenda kujifungua ni 6,190; wagonjwa wa afya ya akili na mengineyo ni 5,124 lakini bado kuna wagonjwa wengine ambao wanatoka katika hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya jimboni kwa Mheshimiwa Waziri, wagonjwa wote wa Rufiji, Mkuranga wote wanafikia kwenye Hospitali ya Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ya Temeke ni hospitali ya Mkoa ambayo waliitwaa kutoka katika Halmashauri ya Temeke. Kinachoshangaza ni kwamba, tokea wameitwaa hospitali ile hakuna mwendelezo. Wodi sasa zimekuwa kama vibanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, ameona changamoto mbalimbali zinatokea katika Hospitali ya Temeke. Mara X-Ray imezimwa, mara wananchi wanalalamika hivi, mara kuna changamoto kibao. Hayo yote nayo yanatokana na kwamba pale Temeke bado, kumekuwa kama hospitali ya Kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali imejenga Hospitali ya Zakhem, lakini ikapime Hospitali ya Zakhem, ni kituo cha afya tuseme, na ile hospitali ya pale Ilala inafanana na hospitali ya Mkoa wa Temeke! Haifanani. Hospitali ya Mkoa ni hospitali kubwa, inatakiwa iwe ina mambo mengi, iwe ina majengo mazuri, iwe na wataalamu, iwe na watumishi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona waliyoyafanya, wameingia pale Hospitali ya Temeke, wameunda Tume, Tume imefanya kazi; wamebadilisha uongozi, lakini pamoja na kubadilisha uongozi ili tumsaidie Dkt. Mfaume, waboreshewe na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wanadai hizo service call zao za kufanya kazi. Wanafanya kazi za ziada, lakini hawana mapato, hawalipwi. Service calls zao hazipatikani. Kwa hiyo, madaktari wa Temeke wapo, wanakwambia, mama sisi hapa Temeke shilingi 5,000 kwetu, kwenda cafe kula, daktari anaona yaani hawezi. Haiwezekani, Temeke ni mjini. Temeke ina wakazi 570,00 kwa mujibu wa sensa. Kwa hiyo, bado tunahitaji maboresho pale Temeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotaka kulijua jambo lako liko bovu kiasi gani, nenda Amana, nenda Mwananyamala; kule mambo ni mazuri. Hapa Temeke kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa waziri kwa moyo wake mzima kabisa aisaidie Temeke. Temeke bado inahitaji msaada, inahitaji maboresho makubwa sana. Nimwombe, na ninamtambua, na Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri, kwamba wote wao ni Wanatemeke. Basi sina mashaka kabisa kwamba wataitendea haki Hospitali ya Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye Hospitali yetu ya Muhimbili. Hospitali ya Muhimbili jamani leo kuja kuletwa hapa, kwamba inataka kujengwa upya, ni jambo kubwa. Ndugu zangu ni jambo kubwa. Hospitali ya Muhimbili ipo pale tangu mwaka 1905, wakati wa Vita ya Maji Maji hadi leo hii, hivi kwelli ni stahiki yake! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kwa dhati. Wapo watu wanaelezea eneo la Hospitali ya Muhimbili ni square meter 176,000 lakini maboresho yanakwenda kufanyiwa katika square meter 46 tu. Majengo ya ghorofa yapande juu, yaende sambamba na hospitali zile za kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua, simama pale Muhimbili, angalia dakika tano hiyo inakuja Ambulance ya Halmashauri ya Handeni; dakika tano hiyo inakuja ambulance sijui ya halmashauri gani, zinaingia pale kwa sababu wagonjwa wale wanatoka rufaa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na kutaka mambo mengi, tuna mambo ya AFCON na nini, lakini je, Tanzania ina hospitali ya Kitaifa? Hapana, hospitali ya Kitaifa ijengwe. Pamoja na kuwa nami ni mwana-heritage nimeona kwamba yale majengo ya Mwaisela, Kibasila, Sewa Haji yatabakia kama majengo ya kihistoria. Kwenye by laws ya culture heritage na historical inasema hivi, nayo yanaweza kukarabatiwa ilimradi yasibadilishwe muundo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba, pamoja na kujenga hospitali mpya, na zile wodi za Mwaisela, Sewa Haji ziingie katika ukarabati mkubwa, ilimradi wasibadilishe ule muundo wake. Mimi ninaomba tuienzi hospitali yetu. Kila mmoja amepitia, kama sio wewe, ndugu yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muhimbili kuna changamoto; mtu anatolewa OPD pale jirani na wazazi, anabebwa kwenye baiskeli. Tusione kuwa sisi tuna magari; kwa kutumia baiskeli anapelekwa nginjangija hadi Mwaisela. Hivi ni kweli kuwa Hospitali ya Taifa inatakiwa iwe hivyo! Hapana, ni lazima ijengwe, na niseme kwamba tumechelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kwa dhati ya moyo wake. Mama huyu ni wa huruma, wa upendo, nimwambie mama yangu chapa kazi, chapa kazi, Watanzania watakukumbuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walisema SGR, leo SGR hiyo inatubeba wote. Bwawa la Mwalimu Nyerere…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako, muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM N. KISANGI: … leo hiyo changamoto ya umeme imeondoka. Kwa upande wa bandari; mimi natoka bandari TMK, makontena…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa

MHE. MARIAM N. KISANGI: … yamejaa, bado nusu, jimbo langu lote mwisho litapotea. Haya tuyaulize kule nyuma…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Kisangi muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM N. KISANGI: …alikuwa wapi kama siyo DP World? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Kisangi, muda wako umekwisha.

MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)