Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ghati Zephania Chomete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa, kazi nzuri anayoifanya katika sekta hii ya afya. Pia ninampongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa; tunapenda kumwita Mtu Kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akiwa kwenye Wizara, ni kweli anaisimamia vilivyo. Tumemwona akiwa katika Wizara tofauti tofauti, anafanya vizuri na Wizara inachangamka. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. Ni yeye pamoja na Naibu Waziri, dada yetu Florence na wafanyakazi wote wa Wizara ya Afya, tunawapongeza kwa namna wanavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia wote wanaofanya kazi katika sekta ya afya kwa Mkoa wangu wa Mara. Tumeona kwa namna wanavyowahudumia wananchi wa Mkoa wa Mara katika sekta hii ya afya. Nimesema ninampongeza Rais kwa namna anavyotuletea fedha za miradi ya sekta hii ya afya katika Mkoa wetu wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa muda mrefu Hospitali ya Mwalimu Nyerere ilikuwa haifanyi kazi, lakini kwa huruma za Mheshimiwa Rais, ameleta fedha nyingi, na sasa hospitali ile inaendelea kufanya kazi kwa kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, bado kuna changamoto. Tunashukuru tumepokea miradi tofauti tofauti. Tumepokea mradi wa Kituo cha Damu Salama kwa shilingi 1,000,000,000, tumepokea mradi wa umeme kwa shilingi 4,000,000,000, pia tumepokea mradi wa wodi ya watoto wenye changamoto ya uzito kwa shilingi 1,000,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado tuna changamoto. Fedha ambazo nimezisema hapo hazijaletwa. Bado tunaomba shilingi 14,000,000,000 kwa ajili ya kumalizia Hospitali ya Mwalimu Nyerere, bado fedha hizo hazijaletwa. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, yeye ni kijana wa Mwalimu Nyerere, tumemsikia mara nyingi kwenye nukuu zake akinukuu nukuu za Mwalimu Nyerere, na hospitali ile ni jina la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba shilingi 18,000,000,000 ambazo zinahitajika kwenda kumaliza miradi kwenye ile hospitali, azipeleke ili Wanamara waendelee kupata neema. Siyo Mara tu, hospitali ile inahudumia wananchi kutoka Kenya, Simiyu, na maeneo mengine yaliyouzunguka Mkoa wa Mara. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa unyenyekevu mkubwa akaitazame hospitali ile ili kusudi fedha ziende, miradi ile iweze kukamilika (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuna daktari pale wa saratani ambaye yupo pale, lakini hatuna maabara ya saratani. Wagonjwa wengi wa Mkoa wa Mara ambao ni mama zangu, wana saratani ya matiti, saratani ya damu, na saratani ya utumbo. Hatuna maabara. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri alitazame hilo. Sambamba na hilo sisi Wanamara tunamtegemea sana Mheshimiwa Waziri katika huduma hizi ambazo anatarajia kuzifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuisemea huduma ya bima ya afya ambayo ni kielelezo kikubwa cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Anatamani kila Mtanzania aweze kupata huduma hiyo ya bima ya afya. Tunaomba elimu kubwa itolewe kwa watu wa chini, ili waweze kuelewa maana ya huduma hiyo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, pale wanapoenda kupata huduma, wapate huduma ya vifaatiba, viwepo kwenye vituo, na huduma ya dawa iwepo kwenye vituo. Siyo kwamba mtu awe na bima ya afya halafu anapofika kwenye kituo, anakosa huduma hiyo, siyo jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kumsifia na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi unaotarajiwa kufanyika wa Muhimbili mpya. Ni jambo ambalo kila Mtanzania anatamani Muhimbili mpya ijengwe; na hii Mheshimiwa Rais ametamani kuwaletea Watanzania na kuwaacha na tabasamu. Itakapojengwa Muhimbili mpya, ataleta tabasamu na kuwaachia Watanzania tabasamu kubwa katika Muhimbili mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)