Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nitaanza alipoishia Mheshimiwa Ghati. Tunapozungumzia suala la Muhimbili mpya, hili jambo kama itakumbukwa, tangu mwaka 2020 lilishaanza kusemwa. Kwa hiyo, ninampongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi yake dhidi ya afya ya Watanzania kwa kuamua kuendelea na mradi huu wa Muhimbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati umefika sasa tuipate Muhimbili mpya, kwani majengo yake ni ya muda mrefu sana, yamechakaa. Pia majengo haya ya Muhimbili yamechoka, yana umri takribani wa miaka 100. Yaani ukiuchukua umri wa mzee wetu Kabudi humu ndani na yale majengo ya Muhimbili, Muhimbili ni kubwa kuliko umri wa Mzee Kabudi. Kwa hiyo, tunahitaji kama Watanzania Muhimbili mpya. Rais wetu ana mapenzi na afya ya watu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, atupe maelezo ya kina, mchanganuo wake umekaaje? Kiasi gani kinaenda kwenye ujenzi; na kiasi gani kinaenda kwenye vifaa? Tuseme sisi kama Watanzania tuna kiu kubwa sana ya mradi huu, kwa sababu siyo jambo jipya, ni jambo ambalo limeshakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nina imani kubwa naye, anafanya kazi kubwa na nzuri. Watu wa Rufiji ni mashahidi katika hilo, na ndiyo maana wakampa jina la Mchengerwa (Mtu Kazi). Pia anaye Naibu Waziri mzuri ambaye anafikika, Naibu Waziri ambaye anachukua matatizo ya Watanzania, ni hodari kupokea simu. Mheshimiwa Dkt. Samizi ni mwepesi kwenye simu, hata saa saba usiku amekuwa akipokea simu na akitusaidia changamoto za afya za wananchi wetu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kumsaidia Waziri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka sasa kuzungumzia NCDs, yaani magonjwa yasiyoambukiza. Tishio la magonjwa yasiyoambukiza limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa nchini; na bajeti kubwa ya Wizara hii ya Afya imekuwa inaenda kutibu magonjwa haya yasiyoambukiza, hali ambayo inasababishia mzigo mkubwa kwa Mfuko wetu wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Kwa mwaka 2025/2026 51% ya malipo yameenda kulipia magonjwa haya yasiyoambukiza. Sasa, inabidi hatua za haraka zichukuliwe, vinginevyo tutaufanya Mfuko wetu wa Bima ya Afya kujiendesha kwa nakisi. Nasi tunatamani mfuko huu ufike mahali, ujiendeshe kwa ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana DG wa mfuko huu wa NHIF, dada yangu Irene Isaka, anafanya kazi nzuri sana yeye na watendaji wake, hususan wale watendaji waliopo hapa ndani ya Bunge, Flora pamoja na mwenzie Neema, wanafanya kazi nzuri sana kwa kushirikiana na Wabunge wanapokuwa na changamoto za wananchi wao au wanapopata changamoto za bima ya afya kwenye hospitali mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko umekuwa ukiendelea kuendeshwa kwa nakisi kwa mfululizo wa miaka mitatu, lakini mpaka nusu ya mwaka huu tuliokuwanao mfuko umeanza kufanya vizuri kwa kutengeneza ziada. Ndiyo maana ninamwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la magonjwa yasiyoambukiza inabidi kazi ya ziada ifanyike. Nitaiomba Wizara itoe elimu kwa Watanzania juu ya masuala ya kuwasaidia Watanzania kujua visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili kwenye suala hili, ili tupunguze magonjwa yasiyoambukiza, kwa sababu bajeti kubwa inaenda kutibia huko, ni pamoja na ile kampeni waliyoianzisha ya jua namna yako. Ile kampeni ni nzuri sana. Ninachokiomba itembee kwenye mikoa yote na kwenye wilaya zote. Watanzania tunatakiwa tuwe makini na lishe, kwa sababu tusipokuwa na lishe iliyokamilika ndiyo mwanzo unaotupelekea kuwa na uzito mkubwa, presha, na sukari. Matokeo yake Wizara inabeba mzigo mkubwa wa kwenda kutibia magonjwa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, vingine nitavileta kwa maandishi. Ahsante sana kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja. (Makofi)