Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza tunawapongeza watendaji wa wizara hii, tukianzia na Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa anajiita Castron. Mtendaji mzuri sana huyu, tulikuwanaye tangu zamani, tunamjua, anafanya kazi vizuri. Msaidizi wake Naibu, anafanya kazi, wamemtaja watu wengi sana. Mimi sikumjua huyu mama, kumbe kuna watu wengine humu ndani wamejificha ni wazuri sana. Mama ni mzuri kupita kiasi, anapokea simu usiku na mchana, anamsaidia sana Waziri kwa kweli, anafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu, anafanya kazi vizuri, Mganga Mkuu wa Wizara anafanya kazi vizuri, na watendaji wote wa Wizara tunawapongeza. Tunawapongeza watendaji wote na waganga wote wa Benyamini Mkapa, wanafanya kazi vizuri sana, kwa sababu wao ndio wanaotupokea hapa na wanatutibu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye hoja. Huwa ninajiuliza mambo mengi kwamba, tuna bei elekezi ya pamba, tuna bei elekezi ya mafuta. Ni nini hakitokei tukawa na bei elekezi ya dawa? Sielewi hapa. Yaani hapo sielewi. Kwa sababu leo Asprin sijui Panadol, huyu anauza mia tano, huyu mia mbili. Kuna gharama kubwa za dawa bila sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatutengenezi project; au hata kitengo cha kuangalia ubora wa dawa zetu, lakini kiweke bei elekezi? Tuna kosa gani kuweka bei elekezi ya dawa? Kwa sababu sasa watu wengine wanauza dawa wanavyotaka. Leo ukienda kwenye duka, kuna maduka wanakwambia tunakuuzia dozi, kuna mwingine anakwambia tunakupa kidonge kimoja. Yaani vidonge navyo vinauzwa kama pipi. Kwa nini hatutengenezi mfumo ambao watu wetu wanaweza kutibiwa vizuri? Kwa hiyo, ninafikiri kwamba hili nalo walichukue wakaliweke vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la ujenzi wa Muhimbili mimi hata ningeambiwa usiku wa leo, kwamba jamani eeh hela imepatikana ya kujenga Muhimbili nipo tayari ku-support kwa asilimia mia moja. Wakati fulani huwa tunawaza sana juu ya ujenzi wa hela. Wanasema vitu vitamu na vitu vizuri vinaenda na noti. Leo nenda India Apollo zipo mia ngapi? Niliuliza juzi India, moja inajengwa pale Apollo, dola sijui milioni ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye nchi za watu tunarudi hapa, nchi fulani imeendelea, nchi fulani imeendelea, Tanzania hatuendelei. Tukitaka kujenga, ooh bei kubwa, bei ndogo. Hakuna hiyo, ajenge; tumekubaliana ajenge. Wala mimi siulizi gharama, ajenge, tunaitaka Muhimbili. Tena hiyo Muhimbilii iandikwe Samia Muhimbili mpya, kwa sababu ndiyo Zawadi ambayo mama ndiyo atakuwa ametuachia. Zawadi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unasema maneno hapa, kesho ukiwa Muhimbili, wakikuhudumia utatoka unaangalia majengo, unapiga makofi kwamba, na mimi nilikuwa Mbunge, niliruhusu hapa. Kwa hiyo, tuombe, katika vitu ambavyo ni vya maana, tuweke hilo jengo ili lijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna uwezo wa Mheshimiwa Mchengerwa kukopa fedha tukajenga Muhimbili sasa, ajitahidi apate uwezo wa kukopa fedha kama zile zile, tujenge zahanati zote za vijiji, na tujenge vituo vya afya vyote vya kata. Aombe hizo fedha, tunazitaka kujenga Muhimbili. Tumekubali ajenge, lakini aende akaombe fedha nyingine, kama ni huko huko aombe. Tunataka sera ya Serikali itekelezeke, vijiji vyote viwe na zahanati na kata zote ziwe na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mchengerwa suala moja hapa lingine. Ninawashukuru sana, sana sana Wizara ya Afya, Hospitali yetu ya kongwe ilikuwa na shida kubwa ya X-Ray. Jengo tu la X-Ray lilikuwa limeshindikana, hata jana kabla sijaja hapa nimeuliza kule, wanasema mafundi wako pale wanatengeneza X-Ray kwa speed ya 4G. Ninawashukuru sana kwa hilo, ninamshukuru mama kwa kutupatia hiyo X-Ray na kujenga jengo hilo kongwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la kumalizia. Ninamwomba Mheshimiwa Mchengerwa, hizi habari za bei kuona mganga kijijini shilingi 5,000; kumwona mganga sijui mkoa shilingi 10,000; sijui kumwona nani elfu ngapi, kwa nini? Hivi kweli vijijini kuna waganga jamani? Yaani hata tukimwona nurse tu shilingi 5,000? Shilingi 5,000 kijijini unaitoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hili suala la kumwona mganga liangaliwe mara mbili mbili. Kama mnahitaji waganga wa vijijini wapate hela, tuwawekee kwenye mishahara yao, tuwaache wananchi wapate msaada. Leo mtu anakwenda hana shilingi 5,000 anatoa wapi shilingi 5,000 ya kuweka hapo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Benjamin Mkapa, juzi nimeuliza wanasema Jumatatu mpaka Ijumaa wanatoza shilingi 25,000 kumwona mgonjwa, Jumapili na Jumamosi shilingi 70,000; hospitali ile ile ya Serikali. Hapo hatutaki, twendeni kama ni shilingi 25,000 ya Muhimbili, iwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)