Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama pia sitampongeza Naibu Waziri wetu na wafanyakazi wote wa Wizara hii ya Afya. Kiukweli wanafanya kazi nzuri na sisi tunayaona hayo wanayoyafanya. Pia ninaendelea kupongeza zaidi mageuzi makubwa katika hii Wizara ya Afya ambayo yanakwenda kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesimama, kwanza kabisa ninaunga mkono hoja, hicho ndicho cha kwanza. Ninalo jambo langu ambalo ninalichukulia kwa ubinafsi na linaniumiza sana kwamba, Serengeti nimepokea jumla ya watumishi 25, ninashukuru sana kwa hilo, lakini mpaka ninavyosimama hapa mbele yako jumla ya watumishi 21 wamehama bila kubadilishana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo ikumbukwe Serengeti kama jimbo linahudumia wananchi, lakini pia nina watalii. Sambamba na hayo, Mheshimiwa Rais alivyoandaa Filamu ya The Royal Tour, ameweza kutambulisha utalii na kuweza kuongeza idadi ya wakazi na watu ambao wanazidi kufika Serengeti. Sasa angalia hali ya afya ambayo mimi kama Mbunge wa Jimbo la Serengeti na wananchi wa Serengeti tunapata wakati mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jambo moja, kwamba wakati wanapangwa watumishi wapya, basi sisi tunaopatikana pembezoni tuongezewe idadi, kama unanipatia watumishi 25, au 21 wanaondoka, haya ni mambo ambayo kiukweli yanahuzunisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, mimi pia niungane na Mheshimiwa Ghati Chomete, dada yangu kuhusiana na suala la Hospitali inayobeba hadhi na jina ya Baba yetu wa Taifa. Tunaomba sana, hospitali hiyo iangaliwe kwa upekee mkubwa sana, kwa sababu ukiangalia, sambamba na kwamba Serengeti tunapokea watalii, Hospitali ile ingekuwa imeimarishwa, baadhi ya watalii wangekuwa hawaendi kutibiwa nje ya nchi, wangekuwa wanaishia hapa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia tayari Mheshimiwa Rais amekuja na maono ya kutengeneza uwanja wa Kimataifa wa Serengeti ambao pia unakwenda kuongeza idadi ya watalii, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kaka yangu mtu kazi tafadhali azingatie sana jambo hili na atusaidie watu wa Serengeti na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo sina mengi ya kusema, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, na hongera kwa mageuzi makubwa. (Makofi)