Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Cornel Lucas Magembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia ninaomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Afya. Kwanza nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upendo wake mkubwa kwa Watanzania kwa kuendelea kusimamia afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato alitupatia heshima kubwa katika kipindi chake hiki cha kukamilisha ujenzi wa Hospitali kubwa ya Rufaa pale Chato. Tunamshukuru sana wananchi wa Chato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza kwa kazi nzuri Mheshimiwa Waziri wa Afya pamoja na Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoendelea kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Rais anaomba kura alipokuwa anapita kwetu kule alikuwa anasema katika siku 100 anakwenda kutoa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuanzia makundi maalum. Sasa nilipokuwa nasikiliza hotuba zake nikaanza kujiuliza kwamba ni kweli anakwenda kufanya! Ni nani anakwenda kupewa Wizara ile kwenda kusimamia? Bahati nzuri alipokuwa anataja Baraza la Mawaziri, alipomtaja Mheshimiwa Mchengerwa kwamba ndio anakwenda kuwa Waziri wa Wizara hiyo, nikasema hapa ameweza, ameshika penyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamfahamu Waziri kwa sababu kwenye mambo ya msingi huwa anasimama. Ndiyo maana katika siku 100 haya mambo yamekwenda kutekelezwa. Akiwa TAMISEMI pale na mimi nikiwa DC kwa kweli tulinyooka, tukaenda tukafanya kazi vizuri na ninajua hata alipopelekwa kwenye afya watu wa afya watanyooka. Hongera sana Mheshimiwa Waziri, endelea kupiga kazi na mambo yatakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, tumeona kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Wizara imeomba fedha za maendeleo, na moja ya fedha ambazo zimeombwa ni pamoja na ujenzi na upanuzi wa hospitali yetu kubwa ya Muhimbili. Niungane na wenzangu wengine ambao wamesema kwa kweli ninaunga mkono jambo hili kwa asilimia mia moja kwa sababu linakwenda kurejesha afya zetu sisi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Wizara pamoja na kwenda kuendeleza hospitali yetu kubwa ya Muhimbili, mimi nilikuwa na ushauri ufuatao: Jambo la kwanza ni kutekeleza ile sera ambayo imewekwa na nchi yetu ya kuhakikisha tumepata zahanati kwa kila kijiji, na kuhakikisha tunapata vituo vya afya kwa kila kata na hospitali za wilaya kwa kila wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tukienda kwenye Halmashauri yangu ya Chato na Wilaya ya Chato, tuna kata 23 kwenye Wilaya nzima ya Chato. Vituo vya afya ambavyo viko, vinafanya kazi mpaka sasa hivi vilivyokamilika viko vituo vya afya vitano tu katika kata 23. Sasa ukiona tofauti ya kata 23 kuwa na vituo vya afya vitano vinavyofanya kazi vizuri, maana yake hii ni hatari kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokifahamu, wananchi walio wengi 74% mpaka 80% wanakaa kule kwenye vijiji na kwenye kata. Sasa tukishindwa kuboresha vituo vyetu vya afya ambavyo ndiyo vinakwenda kusaidia watu wengi wanaoishi huko kwenye kata na kwenye vijiji, ninadhani tunakuwa tunafanya kazi ambayo siyo sahihi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara ijikite kwenda kuhakikisha inakamilisha vituo vya afya kwenye kata zetu. Kwa mfano, mimi nina vituo vya afya vinne kwenye jimbo langu lenye kata 14, ambavyo vituo hivi vya afya vilianzishwa, lakini mpaka sasa hivi havijakamilika na kuanza kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho Kituo cha Afya cha Katende ambacho hakitoi huduma yoyote kwa sababu miundombinu na vifaatiba havijakamilika. Tuna Kituo cha Afya cha Nyabilezi - Bukome nacho kimeanza kufanya kazi, lakini siyo kwa weledi ule ambao unatakiwa. Tuna Kituo cha Afya cha Ilemela, Kituo cha Afya cha Bwina, Kituo cha Afya cha Butarama Kata ya Kigongo, vyote vile vilianzishwa, lakini miundombinu yake haijakamilika na vifaa tiba havijafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kwenye mpango wake wa maendeleo wa kupeleka fedha kwenye ukamilishaji wa vituo vya afya, vituo vyangu vya Butarama, Bwina, Ilemela pamoja na Katende vizingatiwe na kingine cha Ilyamchele ambavyo vyote havijapata fedha ya kuweza kwenda kukamilika ili wananchi wa maeneo yale waweze kuwa wanapata huduma zinazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba Wizara hii ndiyo inasimamia sera, lakini iko Wizara ya TAMISEMI ambayo yenyewe inakwenda kutekeleza. Pia kuna ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI, na fedha nyingine nyingi zinapitia kwenye Wizara ya Afya. Zitoke fedha kutoka Wizara ya Afya zipelekwe kwenye TAMISEMI ili vituo hivi viende kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)