Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Grace Elias Mkoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. GRACE E. MKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Bajeti hii ya Wizara ya Afya. Kwanza, ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema nami kusimama mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru au kuwapongeza Waziri wa Wizara ya Afya, lakini Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwa kazi nyingi ambazo wanazifanya katika Wizara hii na tuliona mchango wao mkubwa sana katika Wizara hii wanaoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwa fedha nyingi ambazo amezileta katika Mkoa wetu wa Singida, takribani shilingi bilioni 5,140, ili kutekeleza miradi ya Wizara ya Afya katika Mkoa wetu wa Singida. Fedha hizo zimetumika kuboresha miundobinu katika Mkoa wetu wa Singida; kujenga zahanati katika Mkoa wetu wa Singida, ambapo zahanati hizo zilikuwa hazijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kupongeza sana watumishi wetu wa Mkoa wa Singida ambao baada ya fedha hizi kuletwa, wao walizisimamia na kuhakikisha zahanati na vituo vya afya vikakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na fedha hizo kuletwa katika Mkoa wetu wa Singida, lakini bado tuna changamoto nyingi sana. Katika Mkoa wetu bado tuna changamoto za watumishi, takribani 58%. Watumishi hao ni madaktari wa usingizi, waganga na manesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku nilitembelea zahanati mojawapo katika Mkoa wetu wa Singida, zahanati hiyo ya Bomani, nilikutana na nesi mmoja, anatoa chanjo, lakini pia anawasaidia wanawake wajawazito hasa pale ambapo wanapata uchungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Singida changamoto ya watumishi ni kubwa sana. Ninaomba Serikali, kupitia Waziri wetu wa Wizara ya Afya, alichukue hili na akajaribu kuitatua changamoto hii hasa kwa Mkoa wetu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wetu wa Singida bado kuna ukosefu wa magari ya kusambazia chanjo. Mfano, katika Wilaya ya Ikungi bado kuna changamoto kubwa sana, Wilaya hiyo haina kabisa gari la kusambazia chanjo. Pia, Mkalama nako kuna changamoto kubwa sana, hakuna gari kabisa la kusambazia chanjo. Nina imani kubwa sana na Waziri wetu wa Wizara ya Afya, ninaomba alione hili, ili sasa hawa wananchi na wenyewe wakapate gari la kusambazia chanjo, katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkoa wetu wa Singida bado kuna changamoto kubwa sana, na changamoto hiyo bado kuna kata takribani 78, hazijapata vituo vya afya. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara hii ya Afya, alichukue hili na alione kwa uzito sana. Ukiangalia Mkoa wetu wa Singida na wilaya zake zote, uko scattered sana. Wananchi wa Mkoa wa Singida wanaishi scattered sana, na wanapata changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri alichukue hili na aliangalie kwa uzito, sasa na wananchi wa Mkoa wa Singida wakajengewe hospitali ili tuweze kutatua changamoto ya watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza sana Wizara hii kwa kazi nyingi inayoendelea kufanya, lakini kuna ujenzi wa Hospitali ya Muhimbili. Ninaunga mkono hoja kwa huu ujenzi mkubwa wa Hospitali ya Muhimbili, kwa sababu Hospitali hii ya Muhimbili inaenda kulitangaza Taifa la Tanzania kwa upya. Pia inaenda kutatua changamoto nyingi ambayo sasa wananchi wengi walikuwa wanatoka kwenye mikoa yetu ya Tanzania, wanaenda kulundikana katika Hospitali ya Muhimbili. Mlundikano unakuwa ni mkubwa, lakini hospitali hii ikienda kujengwa wananchi wengi wataenda kufaidika na hii hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, nami ninaunga mkono hoja. (Makofi)