Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanakwerekwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais, ambayo mimi ninasema sasa hivi washafikia 100%, kwa kwenda kuijenga ile Muhimbili mpya. Tayari 100% zimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze tu kwa kuipongeza Serikali, ilikuwa ina dhamira nzuri, njema, yenye tija katika Taifa letu ya kuondoa chakula kukipeleka TBS. Bado tunaona kuna shida nyingine ambayo sasa hivi imejitokeza. Watu ambao wanafanya biashara ya chakula, udhibiti wao umekuwa mdogo, yaani udhibiti wao umekuwa hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, na tunaiomba Serikali, hii dhamana ya kudhibiti chakula irudi tena kwa TMDA. Taasisi hii ilipata ithibati kubwa sana, na uaminifu duniani kote, kwa sababu tu ya udhibiti mzuri ambao tulikuwa tunaenda nao Tanzania. Sasa hivi tunaomba tena warejeshewe majukumu haya, waendelee nayo wao, ili tuendelee kuwa na hadhi ile ile kama dunia ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zina FDA, kwa maana ya kwamba, wao ndio wadhibiti wa chakula na dawa. Naomba sana Serikali yetu sikivu hii, irejeshe mambo haya katika TMDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa biashara ya supplement imehamia kwenye mitandao. Ukifungua mtandao wa Mheshimiwa Waziri hapo, dawa zote, supplement zote zinauzwa kwenye mitandao. Mbali ya hilo, tayari wale ambao wanauza, wao wanajiita madaktari. Dozi zinatolewa kwenye mitandao, supplement hizo zinauzwa kwenye mitandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wazuri tu sasa hivi, sasa hawa wanaouza hizi supplement kwenye mitandao, na wao waweze kwenda kuchangia huu Mfuko wa Bima ya Afya. Tuna vijana wazuri ambao wametengeneza njia nzuri za makusanyo, basi nao walisaidie Taifa hili katika kupeleka fedha hizo, makusanyo hayo kusaidia wenzetu ambao watakuwa wanaenda katika kuisaidia Bima ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na jambo lingine. Tuna hospitali nyingi sana ambazo tayari tumeshatengeneza, bado tunahitaji marekebisho na vifaa. Katika bajeti hii, ninamwomba sana Waziri aende akasaidie hospitali hizi. Wenzetu Wabunge hapa wamesimama wakasema, wakatoa na mifano katika maeneo yao. Bajeti hii iende ikatatue changamoto hizo, tukiamini kwamba Waziri ni mtu kazi, atakwenda kuboresha hospitali hizi, walau zifikie malengo ambayo Wabunge hawa na wananchi wale wanatarajia kufikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimalizie suala langu dogo tu kuhusu DMO, na RMO, wengi wao ni wanaume. Mheshimiwa Waziri, akikaa na Wizara ya TAMISEMI, waende wakaongeze idadi ya wanawake kuwa ma-DMO na ma-RMO. Tunataka kuondoa vifo vya mama wajawazito na watoto. Tukiwawekea hawa ma-RMO na ma-DMO ambao watakwenda kuongeza nguvu katika kinga ya mama na mtoto, basi tutakwenda kufikia malengo kabisa ya kuondoa vifo kabisa, kuwe hakuna. Tukatimize hili, idadi yao tumeitazama, ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali hizo hizo, tuna hospitali ambazo Mheshimiwa Waziri amesema makusanyo yao yako chini. Tuna hawa ma-DMO, ma-RMO ambao wamekaa katika wilaya katika mikoa, kwa kipindi kikubwa. Tayari chochoro zote za wizi, chochoro zote za kuingiza vitu ambavyo havihitajiki, wameshazizoea. Waende wakafanye mabadiliko, watu ambao tayari wamekaa kwa miaka miwili, miaka mitano, miaka 10 katika maeneo hayo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Waziri amezunguka katika Wizara nyingi, ndani ya miaka mitano, siyo chini ya Wizara tatu. Basi nao wafanyiwe mabadiliko, kuona angalau tunaenda kuleta tija, lakini angalau tunaweza kwenda kukusanya maduhuli ambayo yatakuwa yanasaidia Wizara katika makusanyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninaiomba sana Serikali, tuna ujenzi mkubwa ambao unakwenda kuijenga Muhimbili mpya. Muhimbili mpya ndiyo taswira ya afya katika Taifa letu. Wizara iongeze nguvu, Waziri amesema baada ya miaka mitano, kama kuna uwezekano, Mheshimiwa Rais amesema anataka kuacha furaha kwa Watanzania hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kama kuna uwezekano, ishuke chini baada ya miaka mitano hata iwe miaka mitatu. Mheshimiwa Rais na yeye atimize majukumu haya, aone furaha hii akiwa bado yupo katika madaraka yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nami ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)