Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Muhimbili ni kioo cha Tanzania kwenye matibabu. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira ya makusudi kuijenga Muhimbili mpya. Ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri wake, na madaktari, wauguzi, watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo kila mmoja wetu anaiona, kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Mchengerwa kwa usimamizi mzuri wa huduma za afya, ambazo zinaendelea kupatikana ndani ya nchi, katika kutoa huduma hizi kupitia madaktari bingwa na wabobezi, ambao wanatoa huduma za afya ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanikiwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya, kutoka vituo 10,153 mwaka 2021/2022 mpaka kufikia vituo 13,683 mwezi Machi, 2026. Ni hatua kubwa kwa Serikali, tunaomba kuwapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha anaimarisha Bima ya Afya, na Serikali imetoa shilingi bilioni 48.8 kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata Bima ya Afya, na tayari kaya zaidi ya 200,000, zimeweza kufikiwa katika kupewa Bima ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze zaidi katika huduma ya afya, kwa madaktari bingwa na madaktari bingwa mabobezi, hasa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande huu ninaomba nichangie katika utoaji huduma. Tumeiona JKCI inavyopeleka huduma katika mikoa mingi Tanzania. Wanatoa huduma za kliniki ambazo zinawasaidia wananchi wa Tanzania katika kutatua changamoto za magonjwa wa moyo zinazowakumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa, nami ninaomba JKCI kupitia Serikali yetu ya Tanzania na msimamizi wake mkuu Mheshimiwa Mchengerwa, kwenye upande wa afya, iwe na dhamira ya makusudi ya kupeleka huduma za afya kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuanzisha Kituo cha Moyo katika Serikali ya Zanzibar. Huduma hii, ninaamini itakwenda kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nimeiomba kwa sababu itawarahisishia wananchi, kuwauguza wagonjwa. Wanaposafiri kufika Muhimbili kwenye kituo cha JKCI, itawapunguzia gharama, pia kituo hiki kitakapokuwa kimeanzishwa Zanzibar. Kwa hiyo, ninaomba hili lichukuliwe, kwa ajili ya kuanzisha branch kule Zanzibar cha JKCI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua suala hili Wizara ya Afya iko Bara, lakini ninaomba ishirikiane na SMZ, yaani zinatofautiana kati ya Bara na Zanzibar. Ninaomba zishirikiane na SMZ kuanzisha kituo cha afya kwa ajili ya magonjwa ya moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia Serikali yangu sikivu na ninaamini itashughulikia suala hili kwenye upande wa magonjwa ya saratani. Magonjwa ya saratani yana maumivu makubwa na ni makali sana, yanawaumiza sana Watanzania, lakini gharama zake nazo ni kubwa. Mgonjwa anapofika hatua ya kuanzishwa chemotherapy, gharama ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali yangu sikivu ipunguze gharama za matibabu haya ya saratani kwa sababu maumivu ya saratani ni makali, lakini gharama nazo zikiwa kubwa mgonjwa anazidi kupata maumivu makali. Ninaiomba Serikali iliangalie suala hili ili kupunguza gharama hizo kwenye upande wa saratani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kufikia 106 mpaka ikamfikia kupata tuzo ya Rais bora katika utoaji wa huduma za afya ya akina mama na watoto kwa kupunguza za vifo barani Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)