Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Janeth Peter Pinda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JANETH P. PINDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waziri wa Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara, pia watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya kazi za afya na katika kuboresha shughuli zote za afya na kuwafanya Watanzania waendelee kupata huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi sana ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa kinara katika kuwafanya akina mama wajawazito pamoja na watoto kuendelea kupata afya bora. Hili kwa kweli sisi tutakuwa ni wachoyo wa fadhila tusipomshukuru sana mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, sasa niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Ninaomba nishukuru sana katika kipindi hiki tumepokea shilingi bilioni 2.3. Yote hii ni kwa ajili ya kuviwezesha vituo vya kutolea huduma kuweza kutoa huduma za dharura pamoja na upasuaji na kwa ajili ya akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa niende moja kwa moja kwenye suala la ujenzi wa viwanda. Ninaenda kwenye ujenzi wa viwanda kwa sababu tumejengewa vituo vingi sana vya afya, tumejengewa hospitali, sasa kazi itakuja kwenye uhaba wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe tukijengewa hiki kiwanda cha dawa kitaweza kutuondolea sisi adha ya uhaba wa dawa. Kwa sababu gani? Tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote. Tunapoenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote, watu wengi watakwenda kuwa na bima, na wengi watahitaji dawa, na wengi zaidi ni wale ambao wanaweza wakawa na magonjwa yale yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kukiwa kuna changamoto ya dawa, itakuwa ni shida katika hivi vituo ambavyo tumeweka, watu watakaokwenda kupata huduma watakosa huduma hizi. Kwa hiyo, ninaomba sana katika suala la viwanda tulipe kipaumbele katika bajeti hii ambayo tunakwenda kuitekeleza kwa mwaka wa fedha huu unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Bima ya Afya kwa Wote. Ninawapongeza sana Wizara kwa namna ambavyo wamelichukua na kulipa kipaumbele kama vile Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alivyoahidi katika siku zake 100 za utendaji wake wa kazi, aweze kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tumeona limetekelezeka kwa wale watu ambao ni wa kima cha chini au watu wasiokuwa na uwezo. Kwa kweli niwapongeze sana watu wa bima ya afya ambao wamelitekeleza hadi kufikia leo ni kwa 62% ya malengo ambayo yalikuwa yamewekwa katika usajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Wizara katika mwaka wa fedha unaokuja tuone namna tutaweza kufikia na watu wengine ili waweze na wenyewe kupata bima ya afya. Kikubwa tuendelee kutoa elimu ili kuwafikia wananchi wengi waweze kuelewa bima ya afya ni kitu gani, ili tutakapokuja kwenda katika makundi mengine kusiwe na shida kwa sababu watu wengi watakuwa tayari wameshaelewa hiyo bima ya afya ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote haya, ninaomba sana katika Dira ya 2050 inasisitiza Taifa la watu au wananchi wenye afya njema. Wananchi wakiwa na afya njema, wataweza kuwa wabunifu, lakini watazalisha zaidi na kufanya ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za maendeleo waweze kujiamini kwa sababu watakuwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika sekta ya afya siyo tu uwekezaji wa kawaida, ni uwekezaji wa kimkakati ambao utaweza kusaidia Watanzania kuwa na afya bora. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri katika utekelezaji wa bajeti hii, ni muhimu kufungamanisha maono ya Dira ya Taifa pamoja na maono ya Mheshimiwa Rais, kwa sababu hayo yote yeye anachokitaka ni Watanzania kuwa na afya bora. Kwa hiyo, tukizifungamanisha tutaweza kutekeleza Dira 2050 ili wananchi waweze kuwa na afya bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inapaswa kuwa chombo kikuu cha utekelezaji wa Dira ya Taifa kwa maana ya kwamba kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya ya msingi za vijijini na mijini na pia kuwekeza katika afya ya mama na mtoto hasa mama mjamzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wangu wa Katavi, ninashukuru kumekuwa na ule utaratibu wa Thamini Uhai wa Mjamzito na Mtoto. Kwa kweli tunatekeleza katika wilaya zile zote tano na tunayaona mafanikio makubwa sana, akina mama wananufaika sana na huu mradi. Ninaomba hata katika vile vituo vya afya tuweze pia na vyenyewe kuweka utaratibu wa kuweza kwenda kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sitakuwa na mambo mengi, zaidi sana niende kwenye ujenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Ninaweza nikaungana na wenzangu kuona kwamba hii hospitali ni muhimu tukaijenga kwa sababu tumejengewa hospitali mikoani, lakini tumepata vituo vya afya. Ikijengwa hii itaboresha zaidi huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru ninaunga mkono hoja. (Makofi)