Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu na wananchi wa Urambo kwa jinsi wanavyonipa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba yao ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ametutendea haki kwa upande wa huduma za afya. Ametujengea vituo vya afya na zahanati. Sina mengi ya kusema, zaidi ya kusema Mheshimiwa Rais ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee pia nimshukuru sana Mheshimiwa Mchengerwa, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayofanya. Kwa kweli Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa huduma nyingi alizotupa Urambo, tunaomba ambulance, kwa sababu sasa kukimbiza wagonjwa Kitete Hospitali ya Mkoa na kwingineko, kwa kweli ni shida. Tunaomba sana ambulance. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa upande wa Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Tabora tuna Hospitali ya Mkoa inayojulikana kwa jina la Kitete, lakini kwa upande wa maradhi yasiyoambukizwa, tuna shida sana ya kupata huduma. Malaria na mengine yote, sawa, lakini yasiyoambukizwa ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huduma kubwa ambazo tunazitegemea, 17 katika hospitali ya mkoa sisi tunazo sita tu. Kwa hiyo sasa hivi hata tukipiga simu, utakuta wagonjwa wetu wengi wapo hapa; wapo Benjamin Mkapa, wapo Bugando, wapo Nkinga, kwa sababu huduma za kibingwa kwa kweli zinazotolewa Kitete ni sita tu kati ya 17. Kwa heshima ninamwomba Waziri ambaye ninamjua ni mchapakazi, nimefanya naye kazi sana, atusaidie huduma za kibingwa ziongezwe Hospitali ya Kitete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo nimshukuru kwamba katika hiyo Hospitali ya Kitete wanajenga wodi ya watoto hasa ICU na imeendelea vizuri isipokuwa kwa upande wa wodi ya akina mama, (ya wazazi) haiendelei sana. Kwa hiyo, tunaomba tusaidiwe, inasuasua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa Mkoa wa Tabora, tuna shida kubwa sana na hospitali ya kanda. Kwa muda mrefu Serikali ilitupa matumaini kwamba Mkoa wa Tabora utakuwa na hospitali ya kanda mpaka tukatafuta eneo kubwa Buigiri mpaka sasa hivi bado tunaota. Je, Serikali bado inatufikiria? Tunaiomba Serikali isitusahau, ndoto ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu Mkoa wa Tabora kuwa na hospitali ya kanda iendelezwe kwa sababu ni matumaini yetu kwamba ikiwa hospitali ya kanda huduma itakuwa kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaomba hiyo hospitali isibadilishwe kwa kuwa wazo lilikuwapo la kupeleka Buigiri hospitali ya kanda iendelee. Pia, tuliahidiwa kwamba kutakuwa na Hospitali ya Utengamao ambayo itajengwa Nzega na tayari wameshatafuta eneo. Kwa hiyo, tunaomba Hospitali ya Utengamao ijengwe nzega kama Serikali ilivyotuahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TMDA, kwa muda mrefu TFDA ilikuwa inapima vyakula, baada ya kuwa TMDA tunaomba irudishwe iwe TFDA iendelee na kazi iliyokuwa ikifanya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, ninashukuru sana kwa nafasi hii, ninamwombea Mungu Rais wetu aendelee, Mawaziri wetu wa Afya waendelee ili tupate afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)