Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Revocatus Chipando Clayton

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara ya Afya. Kwa sababu dakika ni chache, ninaomba nikimbizane, nilikuwa na vitu vingi sana vya kuongea katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nichukue muda huu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Tanzania. Ninataka niwaambieni na hii ibakie kwenye kumbukumbu ya Bunge hili. Kazi aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Wizara hii ya Afya itabakia kwenye kumbukumbu za Watanzania milele na milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetembea mikoa kwa mikoa nikiwa na kampeni yangu inaitwa “Mama hana deni.” Moja kati ya vitu ambavyo nimeshuhudia kwa macho yangu ni majengo mapya ya kisasa yanayojengwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimekwenda kushuhudia vifaa vya kisasa na mitambo ambayo watu wote wa mikoani walikuwa wanalazimika kwenda Muhimbili ikiwa inapatikana katika mikoa yetu huko Kigoma, Mwanza na sehemu nyingine tofauti tofauti. Kazi iliyofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itabakia kwenye kumbukumbu. Kwa wale ambao kazi yao ni kupingapinga, hii inaitwa “Shikeni Adabu, Mama kafanya kazi.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimpongeze Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu wake dada yangu Mheshimiwa Dkt. Florence. Ninataka niwaambieni Waheshimiwa Wabunge, hii combination ni ya hatari. Tuwe macho kushuhudia kazi inayoenda kufanywa na hawa majemedari wa kazi. Ukisikia Mheshimiwa Mchengerwa anaitwa Mtu Kazi, tunamjua kutokea Wizara nyingine alizotokea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Mchengerwa katika Wizara nyingine inatupa imani kubwa kwamba bajeti hii tumwachie aende nayo ili tuweze kuona matokeo katika Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambieni Waheshimiwa Wabunge, moja kati ya vitu ambavyo vitabakia katika kumbukumbu ya maisha yangu, ni jambo la kutengewa shilingi 8,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kanda Kigoma Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma tuko karibu na Burundi, tuko karibu na Zambia, tuko karibu na Congo. Hizi fedha tunazokopa tunafanyaje? Zinatakiwa zirudi. Ili zirudi, ni lazima tuchukue fedha za Congo, na za Burundi, za Zambia. Lazima Kigoma iwe ndiyo sehemu kama hub ya nchi hii kukusanya fedha kupitia Wizara ya Afya. Mwaka 2025 zilitengwa, haikujengwa? Ninaomba mwaka huu tuanze ujenzi, shilingi 8,000,000,000 zianze kufanya kazi katika Jimbo la Kigoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka ninaomba sana Wizara ya Afya iweke kitengo cha kutoa elimu mtandaoni. Washauri wa mitandaoni wamekuwa ni wengi, watatumaliza. Unaweza ukalala, ukaamka asubuhi ukakuta umekatazwa kula kila kitu. Kuna mtu anakataza usile ugali. Jamani, mimi nimekula ugali miaka 35. Leo hii ndiyo ukila ugali unaambiwa sasa ndiyo umejimaliza kweli! Hivi watu wa vijijini unaweza ukawapa hiyo idea kweli eti mtu asile ugali! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali sana tunawaomba Wizara itenge kitengo maalumu cha kutoa elimu mtandaoni. Hawa wanaongea ovyo ovyo wakamateni. Elimu wanazotoa hizi za ovyo ovyo zinatupotosha. Huyu anakwambia kula maembe, huyu anasema maembe yana sukari. Sukari ni ule utamu, kwa hiyo, hata ukila maembe, yana sukari. Wanatuchanganya, tunaomba mtengeneze kitengo maalumu kwa ajili ya mitandaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nigusie bima ya afya. Watu wengi wamezungumzia Bima ya Afya kwa Wote, na sisi tunaunga mkono Bima ya Afya kwa Wote kwa sababu tunaamini...

MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Clayton Chipando kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kassimu.

MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpa taarifa Mheshimiwa Baba Levo kwamba China imepitisha sheria na utaratibu kuwa mwenye mamlaka pekee ya kuongelea masuala ya huduma mbalimbali za afya na ushauri wa kitaalamu wa kiafya kwenye mitandao ya kijamii ni mtu aliyethibitishwa na mamlaka husika na mwenye vigezo husika. Hiyo taarifa ninampa, na aichukue. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Clayton Chipando unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea mama na unilindie kamuda kangu. Unajua kengele haitachukua taarifa. Ninaipokea na ninadhani anaunga mkono suala letu la kuhakikisha tunadhibiti waongeaji wa kwenye mitandao ambao wamepitiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwenye bima ya afya. Kwanza ninaunga mkono Bima ya Afya kwa Wote. Wabunge wenzangu watakuwa mashahidi hapa, tunaopata shida zaidi ni sisi Wabunge ambao tuko kwenye majimbo yetu. Mwananchi akiugua, hana hela atakuja kwako, lakini kama tukifanikiwa Bima ya Afya kwa watu Wote, tafsiri yake ni kwamba suala la kuanza kutibiana na wananchi litapungua katika miji yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bima hii ya afya tunaomba iunganishwe na ambulance kwa sababu mtu anatibiwa bure kutokana na bima aliolipia, lakini akipewa rufaa inabidi achangie mafuta ya ambulance. Kwa mfano, Kigoma, na ninashukuru sana niwapongeze uongozi wa Hospitali ya Maweni. Ilikuwa kusafiri kutoka Kigoma mpaka kwenda Dar es Salaam ambulance ulikuwa unalipia karibia shilingi milioni mbili na kitu, shilingi 1,600,000 sijui, ambapo kwa ndege go and return shilingi 700,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ina maana mgonjwa bora amlipie dokta kwenye ndege inakuwa ni shilingi milioni 1.4 wanaenda wanarudi kwa ndege, wanaachana na ambulance. Kwa hiyo, tunaomba kwenye bima iingizwe na ambulance ili mgonjwa huyo anayetibiwa kwa bima akipata rufaa ambulance imbebe asidaiwe fedha nyingine, kwa sababu tunawajua watu wetu, hali zetu ni ngumu huko mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kuhusu ujenzi wa Muhimbili, ninashangaa mtu ambaye anapinga ujenzi wa Muhimbili. Mimi nimetembea katika nchi za wenzetu, unaingia hospitali ni kama unaingia katika hoteli ya five star.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaingia kwenye hospitali unaweza ukajua unaingia airport. Safi (clean), za kisasa, mitambo ya kisasa iko mle ndani. Namwomba Mheshimiwa Mzee Mchengerwa, hawa wanaopingapinga atuachie sisi, yeye aende kufanya kazi. Aende akafanye kazi. Sisi tunatoa baraka zote, Mungu amjalie apewe hizo fedha, aende akafanye kazi ili watu waje wajifunze katika Hospitali yetu ya Muhimbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaomba sana hili mlichukue kwa ukubwa. Kumekuwa na tatizo, watu wanasema madokta wengine wanakimbia kufanya kazi vijijini. Ninaomba sana Mheshimiwa Mzee Mchengerwa aje na mbinu mbadala, waongezee hela madokta wanaofanya kazi vijijini. Mimi ninakuambia kuna watu wanalima dhahabu maporini huko, watu wanatafuta hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwaambia kama ukiwa mjini ni shilingi 2,000,000, ukiwa kijijini ni shilingi 4,000,000, utaona wote wa mjini watahamia vijijini kwa sababu watu wanataka hela. Tengeneza mazingira mazuri. Hakuna mtu ambaye hataki kwenda kufanya kazi sehemu ambayo atapata hela nyingi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, leo nimemaliza kwa wakati. Kwa kusema hayo machache kwenye Jimbo la Kigoma Mjini tuna ombi maalumu la uwezeshaji wa OPD pale, fedha zimepelekwa, ukarabati unaendelea. Tunaomba wale wakandarasi wamalizane kabisa ili tubaki tunawadai kazi na wasibaki wanatudai chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Mwenyezi Mungu awasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)