Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jamila Mahmoud Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JAMILA MAHMOUD JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi kwa nafasi uliyonipatia ya kuweza kuwa mchangiaji wa kwanza kwa session hii ya jioni. Pia, nisiwe mkosefu wa shukrani, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutuwezesha kuwa hai mpaka muda huu na kuweza kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninachukua nafasi hii pia, kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama wa Watanzania, mama wa ukweli, mama mchapakazi. Bila ya yeye hapa sasa hivi tusingekuwa na furaha ya kuchangia Hotuba ya Wizara ya Afya kwa jinsi ya namna alivyowawezesha na kuthamini afya ya Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninachukua nafasi hii kumshukuru au kumpongeza Waziri wa Afya kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba jamii ya Watanzania inapata huduma ya afya sahihi na kwa wakati. Sio yeye peke yake anayefanya hii kazi, anasaidiana na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi, naye pia, anastahili hizi pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zisingeweza kusimama au kutangazika kama Watendaji wa Taasisi na Wizara ya Afya wasingekuwa wanatoa ushirikiano wa karibu kwa Mheshimiwa Waziri na msaidizi wake. Kwa hiyo, ninachukua nafasi hii pia kuwapongeza watendaji wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Seif na watendaji wengine wote kupitia vitengo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itaangazia maeneo mawili makuu, lakini muda ukiruhusu tutaweza kuangalia na vitu vingine. Jambo la kwanza ambalo nitalizungumzia ni suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Muhimbili na pia, nitazungumzia suala zima la Hospitali ya MOI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba, kupitia kiongozi wetu Jemadari, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa bajeti au fedha za kutosha kuhakikisha kwamba ujenzi wa Hospitali ya Muhimbili Mpya unafanikiwa. Naweza kusema kwamba, uazishwaji au ujenzi wa Hospitali ya Muhimbili Mpya lengo lake kubwa ni kutoa huduma za kisasa kwa wagonjwa ambao wapo Tanzania na nje ya Tanzania, lakini pia, ujenzi huu au kupatikana kwa hospitali hii kutapunguza suala zima la rufaa, ambapo mara nyingi tumeona wagonjwa wengi wanatoka Tanzania na kukimbilia matibabu kwenye nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imetoa fursa kwa Watanzania kuweza kupata huduma sahihi na kwa wakati sahihi. Pia, inatoa fursa ya kuongeza kipato au kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kwa sababu ya kupitia au kutopitia huduma ya tibautalii. Uwekezaji wa Hospitali ya Muhimbili, pamoja na kwamba, tumeona kutakuwa na majengo ya kisasa na huduma za kisasa, lakini huduma bora hazipatikani kupitia majengo tu, bali kutokana na huduma inayotolewa ya utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuwa tunajenga hospitali yetu, muhimu ni tunatakiwa tuzingatie rasilimali watu na rasilimali vifaa. Tunahitaji kuwa na madaktari wabobezi na wahudumu ambao wanafanya kazi katika mazingira mazuri, lakini pia, kuwa na vifaa ambavyo vitaweza kuendana na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na programu za kuwa na ubunifu na kufanya tafiti mbalimbali. Hivyo basi, ninashauri wakati tunaendelea na ujenzi, basi twende sambamba na utayarishaji wa rasilimali watu kwa kuwapatia mafunzo na pia, kutafuta na kutayarisha vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mafunzo, tunamaanisha, kwa upande wa madaktari na watendaji wake, lakini pia, kwa sababu tunakwenda katika masuala ya teknolojia, tunahitaji kuwa na watendaji ambao wamepata elimu ya kutosha katika masuala ya teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kidogo kwamba, hivi karibuni kulikuwa kuna suala la mifumo. Kuharibika kwa mifumo ambayo ilisababisha baadhi ya wanafunzi wa internship pale Muhimbili kurejea mitihani yao kwa sababu tu kulikuwa na tatizo hilo, mwanafunzi huyu anaweza kupata report-result ame-pass, akiamka inakuja result ame-fail na kutakiwa akafanye mafunzo. Sasa hii mifumo kama haitakuwa na wasimamizi imara, basi inaweza ikaleta hitilafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Hospitali ya MOI tunashukuru kwamba, imefanya vizuri. Imeweza kuongeza upatikanaji wa huduma. Tumetoka kwenye kuhudumia wagonjwa 8000 mpaka wagonjwa 18,000. Ninaomba tu, kupitia hapa, pamoja na kwamba tunatoa huduma, lakini tunahitaji Hospitali ya MOI kuongeza wigo, kuenea katika maeneo mengine ya Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa sababu, kule Zanzibar tumekuwa na wagonjwa wengi ambao wanapata matatizo ya kuhitaji huduma za upasuaji, lakini wanashindwa kuzifikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Wizara iangalie hiyo, kufungua kitengo chake pale Zanzibar. Aidha, kufungua kimoja kwa ushirikiano na hospitali zilizo Zanzibar ili kuweza kuwahudumia Wazanzibari, kwani nao pia ni Watanzania na wana haki ya kupata fursa na manufaa ambayo yanatoka katika Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)