Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zeyana Abdallah Hamid

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZEYANA ABDALLAH HAMID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha leo kukutana tena kwa siku ya pili kuchangia Bajeti ya Afya. Ninawashukuru sana wachangiaji wengi, hasa wa Kamati ya Afya ambao tumekaa pamoja na Wizara, tunaenda kuandaa mipango mipya ya 2026/2027 itakayohakikisha matumaini, maelekezo, maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunayatendea haki ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuamini kwenye azma yake hii, na hawa ni wananchi wake wapendwa. Analilea Taifa hili na kipaumbele chake cha mwanzo ni afya. Ninaomba nitoe shukrani pia kwa taasisi mbalimbali ambazo wametu-host kipindi cha ziara. Tumeona kwa macho yetu, na ninapenda kutumia sauti hii kuwaambia wananchi kwamba investment iliyofanyika Tanzania ni kubwa mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna matokeo ambayo tutatolea kama mifano ili sote kama Taifa tufunge mikanda kwamba, safari bado inaendelea chini ya uongozi wake jemedari wetu, mtu kazi. Leo tumesikia jina ambalo wengine hatukulizoea, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na msaidizi wake mahiri sana, Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi. Ukiangalia Wizara ya Afya kwa kweli, ina wataalamu waliobobea. Mimi wenyewe najisikia fahari kuongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Seif Shekalaghe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumetembelea taasisi tofauti na Wakurugenzi wamekuwa wakituonesha kazi halisi inayofanywa kutoka haya ambayo yanapangwa kwenda kwenye yale ambayo yanatekelezwa. Ninamshukuru sana na ninampongeza sana Dkt. Grace Magembe, Daktari Mkuu; pia, kuna vinara wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa Muhimbili, ninampongeza sana Dkt. Delilah na Wakurugenzi wengine wa taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zimewezeshwa kwa wataalamu na vifaa. Kinachohitajika sasa hivi ni tuunganishe nguvu kusindikiza bajeti ipewe vipaumbele vya finances. Tusindikize wafanyakazi, tuwape moyo wafanyakazi, tuangalie changamoto zilizobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu mikubwa ni miwili leo na ninapenda nianzie moja kwa moja kwenye kile ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametung’arisha nacho ulimwenguni, upungufu wa vifo vya mama wajawazito. Tulioshiriki mikutano ya Kimataifa ukiwaambia tu unatoka Tanzania wanakuambia, Tanzania ile yenye champion wa maternal death reduction? Unawaambia, ndiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linalofuata na ambalo ninawasihi Wabunge wenzangu ni kila mmoja wetu kuanzia sasa ajitayarishie kujibu. Tulifanyaje? Kwa sababu, hilo suala tunaulizwa na wananchi wa kawaida, pia wanataka kujua kwani tumefanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni investment iliyofanyiwa kazi kimkakati. Ninaomba niende kidogo kwenye takwimu na nitakuwa very brief. Katika kila vizazi 100,000 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametushusha kutoka kwenye vifo 556 mpaka 504. Hili ni punguzo la 80%, ni kubwa, ni la kihistoria na linaendelea kushangaza ulimwengu. Sisi Watanzania tunasema tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunajipongeza na hili, kuna takwimu ambayo ni pacha ya takwimu hii, ninapenda pia, nizungumzie watoto wanaozaliwa katika hivi vizazi 100,000 wanaofariki, tunawapoteza kwa masikitiko, bado ni 2,400. Sasa tukilinganisha hii 104 ambayo work was done na tukitazama hii 2,400 katika 100,000 ile ile, tunajiambia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi bado iendelee. Huu ni mchango ambao tumekuja kukaa kama kamati na tumeona kuna siri ambayo leo ninaomba Wabunge wenzangu tuipate na nina hakika Wizara nayo inaangalia kwa umakini. Taarifa zimeonesha kwamba, tunajipanga hivyo, lakini vizazi vya watoto vinaweza kupunguzwa sana kwa kuweka huu mwambata wa mama na wachangiaji wenzangu wengi wamezungumza kwamba, pamoja na uchache wa wafanyakazi tulionao, hatuna sababu ya kumpoteza mtoto huyu mchanga, ikiwa mwambata atakuwa ni sehemu ya uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwambata huyu sisi hatuna uwezo wa kumgharimia. Hatumlipi wala hatumsomeshi, lakini kuna taasisi ambayo imefanya utafiti na ninaomba niitaje. “Thamini Uhai”, ambayo imeshirikiana na NMR. Kuna taarifa za uhakika kwamba, mwambata ana sehemu kubwa ya kum-save mtoto mchanga huyu tusimpoteze, baada ya kuwa tumem-save mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michoro iliyoandaliwa ni kazi ambayo watu walikaa wakatafakari na wakathamini kumbe kila chumba kinagharimu shilingi 2,000,000, 3,000,000, nyingi ni 4,000,000. Hii siyo gharama kubwa ya kukaa mimi leo nikaizungumza siku muhimu kama leo ya bajeti, lakini kwa vile kuna namna ambayo sote tukikubaliana, tutaweza kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na ninawasihi Wizara ya Afya na TAMISEMI tuiangalie hii investment ndogo, tukaishushe ile 2,400 ya watoto wachanga, ili tupate zawadi nyingine. Mheshimiwa Rais atambulike kushusha kama alivyoshusha vifo vya mama na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona ninavyoiangalia hii ni kazi ambayo hata Halmashauri jamani inaweza kuibeba! Kama ni michoro, ipo; kama ni miongozo, ipo; kama ni sheria, ipo; kama ni azma, ipo; na tunajua Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatutegemea tukawa-save hawa watoto wachanga, basi ninaamini tukishikamana, hili linawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mchango wangu wa pili, nao ninakwenda kwenye mifumo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Malizia, kengele imelia, malizia.

MHE. ZEYANA ABDALLAH HAMID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Wizara ya Afya nawa-salute kwa kutuletea mwarobaini wa mifumo kusomana. Pamoja na kwamba, michango mingi ilikuwa inazungumza kama kushauri, ninaomba niwakilishe Wabunge wenzangu, ushauri wote ambao tumeutoa leo, kama utaisoma ile bajeti vizuri kwa kutulia, wamepita kila kwenye mpango unaohitajika, ninauita mwarobaini na ninathubutu kusema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkufunzi wa mifumo ya afya katika ngazi ya Masters na Ph.D na kila tunachokisomesha kwa mifano chungu nzima ya Marekani na Uingereza, Wizara ya Afya imetuwekea. Ninachowasihi wafanyakazi wa sekta ya afya ni kwamba twendeni tukabadilike. Haya ni mabadiliko ya kiutendaji. Tunaweza tukaona ni makubwa, yanaongeza mzigo kwenye mazungumzo yetu ya kazi, lakini hapana, yanakwenda kutufanyia kazi yetu kuwa nyepesi, kuwa ya uhakika, tuka-save maisha ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda ku-save gharama kubwa sana. Tathmini zinaonesha katika kila Dola moja inayokuwa invested una-save Dola mbili hadi tatu na hizi ni data zilizofanyiwa research. Tunaweza kuona ni fedha nyingi tunawekeza, lakini tutakuja kuona gharama ambazo tumeziweka, within one year tutakuja kukutana hapa tunapongezana kwa kazi nzuri ambayo Wizara imetufanyia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu-support hii kazi, tusomeshe vijana wetu digital health transformation, ndiyo mpango mzima. Ninawapongeza sana Wizara. Ahsante kamati kwa ushirikiano, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)