Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AMINA IDDI MABROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ametujalia jioni hii kuwepo hapa, lakini pia, amenijaalia niweze kusimama kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninaomba kuchukua nafasi hii kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake na mageuzi makubwa ndani ya sekta hii ya afya. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chake ameweza kujenga na kuboresha hospitali katika kila Wilaya. Kaweka vifaa tiba, na pia, ameweza kuweka mashine za kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninavyokwambia imesababisha huduma bora na nzuri kwa wananchi wote wa Tanzania. Kwa mfano, mwaka 2021 kulikuwa kuna MRI saba, sasa hivi ninavyokwambia, mwaka huu 2026, kuna MRI 13. CT-Scan Mwaka 2021 zilikuwa 13, sasa hivi kuna CT-Scan 45. Ultrasound machine mwaka 2021 zilikuwa 476, hapa ninavyozungumza zimeongezeka kufikia 970. Kulikuwa na Digital X-Ray 147, sasa hivi ninapozungumza kuna Digital X-Ray 491.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni baadhi tu ya vifaa ambavyo nimevitaja, kwa kweli kama nitavitaja vifaa vyote hapa, ninaweza muda wangu wote nikaumaliza. Pamoja na mazuri haya ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya na anaendelea kuyafanya, tumpe maua yake, tumpe heshima yake kwa kumtambua yeye ni Mama wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, sasa ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Mheshimiwa Waziri huyu amefanya mambo makubwa toka kipindi chake. Ninampongeza sana yeye pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wake na Watendaji wake. Ninaamini kwamba bila ushirikiano wa pamoja, wasingeweza kufanya maendeleo haya makubwa. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aendelee kuchapa kazi, sisi tuko pamoja naye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwamba umuhimu wa kujenga hospitali mpya nchini, lakini bado Hospitali ya Taifa Muhimbili ina nafasi kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi. Kwa umuhimu huo, ninaomba kusema kwamba bado Watanzania tunahitaji sana ujenzi mpya wa hospitali ya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuungana na wenzangu waliotangulia na ninaamini kwamba wananchi wote na Watanzania wote wanatuangalia tunasemaje kuhusu ujenzi huu wa Muhimbili mpya. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuidhinishe bajeti hii ambayo imetengwa siyo zaidi ya shilingi trilioni 1.2 ili tumpe nafasi Waziri ya kwenda kujenga hospitali ya Muhimbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, ninampongeza tena Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika siku zake 100 za ahadi tangu kuingia madarakani…
(Hapa Kengele Ililia kuashiria kuisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MHE. AMINA IDDI MABROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha pili cha awamu ya Sita, ameweza kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura 161 ambapo utekelezaji wake ulianzia Januari 26, 2026. Ninawapongeza sana Wizara, tunatambua kwamba tayari wameanza awamu hii kwa kutekeleza kuwasajili wananchi siyo zaidi ya milioni moja. Hii ni hatua kubwa sana, hatua ambayo tunastahili kuwapongeza Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawaomba sana Wizara ya Afya wajitahidi sana kuendelea kuwatambua wale wananchi ambao hawana uwezo ili waweze kufikia lengo ambalo limekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza sana Waziri pamoja na timu yake kwa utekelezaji wa Sheria hii ya Bima ya Afya kwa Wote katika kufanya mifumo kusomeka, kwa kuunganisha mifumo ya vituo vya kutolea huduma za afya na mifumo ya Kitaifa ya Bima ya Afya. Tayari sasa hivi hospitali 28 za rufaa, za Mikoa, Kanda Maalumu na Taifa zimeanza kusomana. Hii haijapata kutokea. Haya ni maendeleo makubwa kwa Taifa letu, haya ni maendeleo ambayo tutaweka historia ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ililia, nilikuwa ninangojea umalizie tu.
MHE. AMINA IDDI MABROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaomba kumalizia kwa kusema ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuiunge mkono bajeti hii ya Waziri. Ninakushukuru sana. (Makofi)