Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Ninaomba kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, kutupa uhai sisi sote ambao tuko humu ndani, kutupa afya njema, kwa kweli yeye ni mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumshukuru Mheshimiwa Rais. Nisipomshukuru Mheshimiwa Rais sijui ninaweza kujisikia vipi maana ninaweza nisimalize kuchangia. Ninamshukuru kwa mengi sana ambayo ameyafanya katika nchi hii, na mimi ninaamini katika watu ambao wanaamini kabisa katika Rais ambaye atakuja kukumbukwa akimaliza muda wake, ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo ambayo anayafanya, kwa mambo ambayo ameyafanya na kwa mambo ambayo anaenda kuyafanya. Atatengeneza historia ya kuwa mwanamke shupavu, shujaa, jasiri, mvumilivu, mwenye huruma, na mchapakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Mheshimiwa Rais kwa muda wa siku zake 200 ameweza kuajiri watu 5,000 kuwa watumishi wa kitengo cha afya peke yake. Siyo hayo tu, Mheshimiwa Rais ameweza kupunguza vifo kutoka vifo 550 mpaka vifo 104 katika rate ya idadi ya vifo 100,000. Hili siyo jambo dogo, ni jambo kubwa sana, lazima tumpongeze. Kwa kuwa yeye ni mama, anafahamu machungu ya mzazi, machungu ya mtoto kukosa mzazi, kwa hiyo lazima nimpongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitashukuru Bima ya Afya kwa Wote. Bima ya Afya kwa Wote imeanza tarehe 22 Machi na sasa hivi inaenda kutengeneza mkakati wa kusaidia special groups, yaani wanawake, makundi maalum, wale wasiojiweza pamoja na watu wenye ulemavu. Kwa nini nisiendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais? Nitakuwa mchoyo wa fadhila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, ninaomba kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuleta mashine au kipimo kikubwa cha saratani ambacho ni cha pili katika Sub-Sahara Africa. Unaweza ukaona namna gani Mheshimiwa Rais ameweza kutuheshimisha Tanzania. Siyo hivyo tu, kwa ajili ya kutaka kulinda afya za watu wake ambao wamemchagua, Mheshimiwa Rais, kipenzi chetu ameweza kuandaa mkakati mzuri wa kusaidia magonjwa yasiyoambukiza. Haya magonjwa yote yanaenda kutibiwa bure. Nani kama Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Mheshimiwa Rais ametuletea mashine zile za kuondoa saratani ya awali kwa watu wenye ualbino, ni nani kama Mheshimiwa Rais? Mashine hizi zipo katika hospitali kadhaa kama CCBRT, KCMC, Bugando na Ocean Road ambayo huduma hii inatolewa bure. Yote hii anaenda kutuongezea life span ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi au mtu mwenye ualbino. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na yote ambayo nimeyazungumza hapa, Mheshimiwa Waziri, ni msikivu na watu wote wanaamini ni mtu kazi, ninaomba mashine hizi zisambae Tanzania nzima. Maisha yetu yanategemea hizi mashine kwa sababu unapoona kidogo una kipele, unaweza kwenda kukitoa kipele hiki kabla hakijaleta ugonjwa mkubwa wa ngozi wa saratani. Hii inaenda kutusaidia sisi maisha yetu, nikisema sisi ninamaanisha mimi ni mmojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu uwezo wa Mheshimiwa Waziri, nafahamu uchapakazi wake na ninaamini hili anaenda kulibeba na kupeleka Tanzania nzima, na hamna kinachoshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ninaliomba, kila siku naulizwa na Waheshimiwa Wabunge hapa tunapataje yale mafuta? Ninaomba utengenezwe utaratibu mzuri kupata mafuta ya sunscreen kwa ajili ya kulinda afya za watu wenye ualbino. Kwa sababu gani? Bila haya mafuta, sisi hatutembei; bila haya mafuta, hatu-participate kwenye majukwaa yetu; bila haya mafuta, hatuwezi kushirikiana na wenzetu. Kwa hiyo, maisha yetu yanategemea mafuta haya. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, ninaomba kupongeza juhudi hizi ambazo zinaenda kufanyika, katika kuandaa mkakati wa kutengeneza viwanda kwa ajili ya madawa. Mwenyezi Mungu awabariki sana. Hii inaenda kuondoa tatizo kubwa la kupatikana kwa dawa katika Tanzania yetu. Ni jambo kubwa sana, hatutaweza kwenda kutegemea tena huko nje kama watatuletea au kama tutanunua huko nje, zitakuwa ni kwa kiwango kidogo sana, lakini tutaweza kutengeneza dawa zetu wenyewe na kutibu wananchi wetu kwa sababu tunafahamu umuhimu wa afya ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache, ninawashukuru, ninaunga mkono hoja. (Makofi)