Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, ninapenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, mwanangu sana huyu tulikuwa naye Kamati ya Katiba na Sheria na Mheshimiwa Dkt. Florence mwanangu pia tulikuwa Kamati ya Maliasili na Utalii, kwa kazi nzuri. Sina wasiwasi nao, ninajua watatenda kazi nzuri na Wizara ya Afya itasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kutumia nafasi hii kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri alizozifanya kwenye sekta ya afya kwa Watanzania. Baada ya pongezi hizo, pia ninapenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mganga Mkuu wa hospitali yetu ya Mkoa wa Katavi Dkt. Banuba. Ninawapongeza pia wafanyakazi wote nchini Tanzania, Madaktari na Wauguzi. Kazi ya udaktari na uuguzi ni ya wito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende kwenye mchango kwenye Wizara ya Afya. Pamoja na pongezi hizi, kuna upungufu kwenye mkoa wangu wa Katavi. Kwanza kabisa ninapenda Mheshimiwa Waziri wa Afya afahamu kwamba mkoa wetu wa Katavi hospitali ya rufaa haijakamilika. Hospitali hiyo mwaka 2025 kwenda 2026 kwenye bajeti yake iliomba shilingi 5,000,000,000. Katika hizo shilingi 5,000,000,000, Serikali imeleta shilingi 269,000,000 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizo Mheshimiwa Waziri hazitoshi kumalizia jengo la mama na mtoto ambalo ndiyo kuna wodi ya akina mama, kuna wodi ya watoto, kuna kuna vyumba vya upasuaji na kuna vyumba vya laundry kwa ajili ya kufua mashuka ya hospitali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Mchengerwa mtu kazi, mwanangu, anipatie shilingi 5,000,000,000 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ili iweze kukamilika. Nikiwa nimesimama hapa, wananchi wa Mkoa wa Katavi wamenituma nimwambie Waziri kwamba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi haina mochwari, wagonjwa wanapofariki kwenye hospitali hiyo, wanatakiwa kusafirishwa kupelekwa kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo iko mbali takribani kilometa saba mpaka 12 ambako ndiyo kuna mochwari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inconvenience inayoleta shida kwa wafiwa. Kwanza wanakodi gari la kubeba huo mwili kuupeleka kwenye hospitali, lakini zaidi ya hapo kwenye hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi hakuna hata chumba hicho cha kuhifadhi hiyo miili. Kuna kijikorido fulani tu kimewekewa pazia, miili hiyo ndiyo huwa inawekwa. Mheshimiwa Waziri, niko chini ya miguu yako, ninaomba hizo shilingi 5,000,000,000 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mochwari ni muhimu. Jengo lililoisha pale kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Waziri najua kuna siku atafika, ni OPD tu ndiyo iliyokamilika ambako kwenye hiyo OPD kuna vyumba viwili vya ICU ndiyo vinatumika kuwalaza wagonjwa. Mheshimiwa Waziri ninakuja kwako, ninakulilia, ninakuheshimu, wote ninyi wawili ninaomba fedha shilingi 5,000,000,000 kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilinganisha pia sisi Katavi tuko mbali kufika kwenye hospitali za rufaa. Tunatembea kilomita zaidi ya 700 kuifikia Hospitali ya Rufaa ya Mbeya au hapa Benjamini Dodoma. Plan yetu ya mwanzo ilikuwa ni kujenga hospitali ya Kanda. Kwa bahati mbaya Serikali imeona hospitali ya Kanda ijengwe Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hospitali ya Kanda imejengwa Kigoma, ninawaomba chonde chonde mtukamilishie hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa kutupatia shilingi 5,000,000,000 ili tuweze kukamilisha hilo jengo. Umebaki mwezi mmoja bajeti pesa hizo ziweze kufika huko. Ninaomba sana, tutakapomaliza bajeti yako leo Mheshimiwa Waziri uweze kunifanyia jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumza hapa, pia ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kwenda kufungua utaratibu wa kujenga viwanda vya madawa nchini Tanzania. Hilo ni jambo jema. Tulikuwa na viwanda vya madawa zamani, lakini vile viwanda vilikufa. Bila viwanda vya madawa, hatuwezi kufika popote. Ninashukuru sana na ninapongeza sana kwa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo na wengine wameweza kulizungumza hapa, ni suala la kuboresha hospitali ya Muhimbili, kuwa Muhimbili mpya. Tunaunga mkono hii hoja kwa mikono miwili. Ombi letu ni zile hospitali za rufaa za mikoa zikamilike basi na hiyo Muhimbili mpya ikijengwa tutakuwa tumekwenda sambamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Bima ya Afya. Kwenye Bima ya Afya ninaipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu kuhusu Bima ya Afya, lakini kwenye Bima hii ya Afya ninaomba kutoa angalizo. Mara nyingi watu wamekuwa na Bima ya Afya, wanakwenda hospitali wanaishia kuandikiwa dawa, lakini zile dawa ambazo zina bei, zenye magonjwa makubwa huwa wanaambiwa wakanunue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa bima hii mpya ambayo inakwenda kuanzishwa nchini kwetu Tanzania, ninaomba iangalie hili suala isije watu wakakata hiyo bima mpya, wanapofika pale wanaandikiwa dawa, wanaambiwa wakanunue. Wanaambiwa kwamba hizi dawa hazipo, siyo package ambayo ipo kwenye bima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba kusemea gonjwa moja baya ambalo Watanzania wengi wanakufa, ambalo saa nyingine tunakuwa hatufahamu. Kwenye bima hii ya afya, kuna magonjwa ambayo ni ya gharama. Magonjwa kama ya figo ambayo gharama ya kusafisha kuingia kwenye session moja kusafishwa figo pale Muhimbili ni shilingi 180,000; kule Katavi ni shilingi 200,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujua, hii bima ya afya mpya itakuwa pia inawezesha wagonjwa wa figo, wagonjwa wa kansa wanaokwenda kupata matibabu wataweza kutumia hii bima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja ya Wizara ya Afya. Ombi langu ni lile lile mwanangu Mheshimiwa Mchengerwa, nimepiga magoti kwako ninaomba shilingi 5,000,000,000. (Makofi)