Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kuweza kunipa nafasi hii ili na mimi vilevile niweze kuwa mchangiaji katika Wizara hii ambayo ni muhimu sana kwa maisha ya Watanzania. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia uzima na afya na hatimaye kuweza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nianze kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa na kazi kubwa anayoifanya kuona kwamba anajenga ustawi wa sisi Watanzania. Kwa kweli katika jambo hilo, tunamshukuru sana. Amefanya mambo mengi sana, lakini sasa amekuja kugusa kwenye wizara hii ambayo ni muhimu kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze sana hasa katika kuanzisha afya ya jamii kwa wote. Kwa kweli katika jambo hili tunamshukuru sana kwa sababu hii sasa ndiyo suluhu ya afya kwa Watanzania. Tunasema, mama ahsante sana kwa jambo hili ambalo umetuletea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa kweli sasa leo nimekubali kwamba zigo zito mpe Mheshimiwa Mchengerwa. Mheshimiwa Mchengerwa ame-prove kwamba yeye mambo mazito ndiyo saizi yake. Amefanya mambo mazito kule TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bado tunaona katika hii Wizara ya Afya bado anaendelea kutenda mambo ambayo ni mema. Amelivaa jambo hili la Bima ya Afya kwa Wote, amelibeba kwa nguvu zake zote. Watu huko wana mashaka kwamba sasa Watanzania wote wanakwenda kuingia kwenye bima ya afya. Je, dawa zitapatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ameliona, Mheshimiwa Rais amemwagiza naye amelibeba, akasema sasa anaagiza wawekezaji waweze kuweka viwanda hapa. Tuna imani kubwa sana kwamba sasa Bima ya Afya kwa Wote itawezekana chini ya Mchengerwa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninamshukuru sana Naibu Waziri. Nimewashukuru sana watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tunaamini watatuvusha. Hatuwezi tukaenda kwenye Taifa la uchumi wa kati tukiwa na Watanzania goigoi. Tunataka twende kwenye uchumi wa kati tukiwa na afya njema, tukiwa wenye afya ndipo hapo tutakapoweza kufanya kazi na kwenda kwenye uchumi wa kati. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, Bima ya Afya kwa Wote imeanza, ni jambo jema sana. Ninachoomba sasa, ianze kwa wote. Wameshaanza kweli kwa hizi kaya za TASAF, tunawashukuru. Sasa, waanze na kwa watu wengine wote. Wajue kwamba zaidi ya 70% ya Watanzania ni wakulima, na sisi wakulima, na mimi ni mmojawapo wa wakulima, tunategemea mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo wakati wa mazao sasa, tunaenda kuuza; tukichelewa tutapishana na gari la mshahara. Hii ni kwa sababu fedha zile tutazitumia kwenye mambo mengine, na hiyo shilingi 150,000 itakuwa ni changamoto. Kwa hiyo, niwaombe sana kwamba sasa hii hebu ianze mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, bado kuna changamoto ambazo zipo, na hususan tunaotoka kwenye hizi wilaya hizi mbali. Mimi natoka kule Sikonge, tuna changamoto sana ya watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Jimbo langu la Sikonge, Wilaya ya Sikonge tuna upungufu wa watumishi 191. Nitawaletea hiyo orodha yote ya mahitaji hayo ya wafanyakazi. Nitamletea yeye, nitapeleka TAMISEMI, na vilevile na kule Utumishi, walifanyie kazi. Kama tunataka kuboresha kweli sekta ya afya ni vizuri tukawa na hawa watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, niishukuru sana Serikali kuhusiana na hospitali yetu ya Mkoa ya Kitete. Ni kweli kwamba kuna uwekezaji mkubwa sana ambao Serikali imeufanya katika hospitali yetu ile, lakini ninaomba, bado kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyika katika hospitali yetu ya Kitete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza yale majengo ni ya muda mrefu. Mwenzangu amesema hapa, yana zaidi ya miaka 100, yamechakaa sana. Tunaishukuru Serikali wametusaidia kutengeneza master plan, tumeipata. Sasa tunaomba fedha zipatikane ili kusudi ile hospitali iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zile huduma za kibingwa, mama yangu, Mheshimiwa Mama Sitta amesema pale, tunazo chache. Kati ya 17 tunazo sita tu. Sasa tunaomba zile nyingine zipatikane. Zikishapatikana, nina imani kwamba Wanatabora tutakuwa tumefanyiwa jambo jema. Ni imani yangu kwamba kila kitu kinaenda hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakokwenda kule mbeleni yawezekana hiyo hospitali sasa ikawa ndiyo hospitali yetu ya kanda, lakini kwa kuanzia, tunaomba kwanza tuimarishe hiyo hospitali iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, ninamshukuru sana Naibu Waziri, nimeongea dakika tano. Kwa hiyo, mchango wangu wote is almost ameumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)