Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kassimu Amari Mbaraka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia siku ya leo, kuwemo tena katika Bunge hili Tukufu tukiendelea kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, nami ninachangia katika hii bajeti ya Wizara ya Afya hoja kadhaa ambazo zitakuwa na faida kubwa kwa maslahi mapana ya Taifa, halikadhalika Jimbo la Tanga. Kwani ikizingatiwa Mkoa wa Tanga na Jimbo la Tanga Mjini, tunayo Hospitali pale ya Rufaa ya Mkoa maarufu, inaitwa Bombo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa muhtasari, ninataka nipitishe kidogo kwenye historia. Mwaka 1895 Dkt. Fredrick Plan, mtaalamu wa tropical medicine au tropical disease alijaribu kuangalia na kuona vifo vingi sana ndani ya Mji wa Tanga. Takribani 70% ya vifo vinatokea; akafanya utafiti wake na akabaini kuwa vinasababishwa na Malaria; Cerebral Malaria pamoja na Black Water Fever, hatimaye akawasiliana na Mganga Mkuu wa wakati huo ambaye ni Dkt. Alexander Baker.

Mheshimiwa Spika, alivyowasiliana naye, ikabidi wafikie maamuzi kujenga hospitali ya kwanza Tanganyika ambayo inaitwa Bombo Hospital Cliff. Kitaalamu kwenye maandiko ya historia tunasema first modern hospital ikajengwa Tanga ndani ya Taifa hili la Tanganyika. Hiyo ni historia adhimu ninaomba ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimeileta hoja hii ya kihistoria mezani? Ni kwa sababu baadhi ya mambo yasipoeleweka, historia yake huchukuliwa sana kawaida. Hospitali hii ilihudumu kutibu majeruhi wa Vita vya Kwanza vya Dunia, watalamu na wafanyakazi mbalimbali waliokuwa wakipata majeraha kwenye reli, sasa nini kipo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jengo hili la Cliff lipo ndani ya Hospitali ya Bombo. Watu wa TBA na watu mambo ya kale wamekuja kulikagua na kuliangalia kama ni salama na linaweza kutumika. Lina umri takribani miaka 131, kwa hiyo linafaa kutumika. Sasa niiombe Serikali ilikarabati jengo ili liweze kutumika kwa ajili ya matumizi ya wodi ya mama na mtoto. Wakati tukisubiri kujenga wodi ya mama na mtoto tutumie jengo hili tukilikarabati ili liweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Venice Chatter ya mwaka 1966 na Burra Chatter ya mwaka 1979, zote hizi international document kuhusiana na cultural heritage and monument zinaruhusu kukarabati majengo ya kale, kuyaweka vizuri, na yakiwa ni salama yatumike kwa maslahi mapana ya jamii, lakini huku yakiwa yana-preserve ile historia ya eneo husika. Kwa hiyo, Cliff inaangukia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata ukija kwenye by laws za UNESCO na cultural heritage inazungumzia masuala haya. Pia inaruhusu jengo hilo likarabatiwe. Tumeona Tanga tulikuwa na shule inaitwa Old Tanga, leo hii imekarabatiwa na inatumika. Vilevile tunaona Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi anakarabati majengo mbalimbali ya kale na yanaendelea kukaa katika ubora wake. Ile structure haipotei, lakini kwa sababu ni salama yatumike. Kwa heshima na taadhima ninaomba Serikali ilikarabati Jengo la Cliff na lianze kutumika rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo, nukta nyingine ya msingi kabisa ni kuhusiana na hospitali yetu ya Bombo. Tuna Wodi za Galanosi, Sokoine, na Mwapachu. Kwenye Wodi za Sokoine na Mwapachu mifumo ya maji na majitaka yote inatakiwa yarekebishwe, pamoja na mifumo ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tunaomba hii Wodi ya Galanosi Serikali itazame kwa umakini zaidi, kwamba sasa hii wodi iweze kujengwa upya kulingana na mahitaji. Hii ni kwa sababu ndiyo wodi inayohudumia magonjwa ya internal medicine. Inachukua takribani 63% ya idadi ya wagonjwa wote wanaokuja katika Hospitali ya Bombo. Hili liangaliwe kwa mapana sana na liangaliwe vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyazungumza hayo, sasa niishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi mkubwa wa Jengo la Damu Salama (Benki ya Damu Salama) ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ambalo linaenda kumaliza changamoto inayotusumbua ndani ya Mkoa wa Tanga inahusiana na Benki ya Damu Salama. Vifaa tayari vimekwishafika, vitendea kazi vipo, kinachohitajika ni jengo hili sasa kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Wizara ya Afya na Mheshimiwa Waziri Mohamed Mchengerwa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Florence Samizi kwa kuhakikisha kwamba ndani ya Mkoa wa Tanga Hospitali yetu ya Bombo takribani shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati na kumalizia jengo hili la mradi huu wa Damu Salama. Haya ni mambo makubwa na ni mambo ya kihistoria.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jambo hili kubwa na tukufu. Hapo awali hatukuwa na Benki ya Damu Salama. Tukihitaji mahitaji ya damu, lazima twende Kilimanjaro ili damu iweze kusafishwa, kuchakatwa, kisha baadaye ndipo irudishwe Tanga kwa ajili ya mahitaji, lakini sasa tunaenda kupata damu salama.

Mheshimiwa Spika, shukrani sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)