Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Patrick Adkin Mwalunenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia machache kwenye hii Wizara yetu muhimu kabisa kwa maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake kwa uwekezaji mkubwa sana kwenye Wizara hii. Pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na mabadiliko makubwa ambayo ameanza kuyafanya, tunayaona. Kweli yeye ni mtu kazi.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji uliowekezwa kwenye hospitali nchi nzima, na kwenye Jimbo langu la Mbeya Mjini ni mkubwa sana. Pale Mbeya Mjini ninayo Hospitali ya Kanda ya Rufaa, tuna mashine zote. Tuna CT-Scan tuna MRI, na vilevile inajengwa hospitali kubwa ya kansa pale Mbeya Mjini kwa ajili ya kuhudumia watu wote wa kanda hiyo. Maana yake ni kwamba, wagonjwa wanaotoka mikoa ya Katavi, Sumbawanga, na Songwe watatibiwa Mbeya. Vilevile, hata wagonjwa wakitoka nchi za jirani za Malawi na Zambia watatibiwa Mbeya. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri na pia ninampongeza sana Mheshimiwa Rais uwekezaji huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni maboresho ya Hospitali ya Muhimbili. Nchi za wenzetu, hasa hizi za jirani hospitali nyingi zinamilikiwa na watu binafsi, na ndiyo maana matibabu ni ghali sana, ukienda za wenzetu, hata ukienda huko India. Hapa kwetu Serikali imethubutu, inawekeza yenyewe na kuzimiliki hospitali hizo. Maana yake ni kwamba, gharama za matibabu zinapungua na kuwa na unafuu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niipongeze bima ya afya imeanza vizuri kwa zile kaya masikini. Hata hivyo, ninataka twende mbali zaidi, tutumie Wizara nyingine zitoe ushirikiano. Hapa ninaenda kwenye Wizara ya Kilimo. Mwenzangu amechangia kidogo, Wizara ya Kilimo inaweza kutoa majawabu, kwa maana yenyewe ndiyo inayoshughulika na wakulima. 75% ya watu wetu ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakati sasa umefika Wizara ya Kilimo kuwasajili wakulima wote kwenye ushirika. Kupitia mazao yao, wanaweza wakakatiwa Bima za Afya na Serikali haiwezi kubeba mzigo wowote. Wakatwe makato kidogo, na kila mtu atapata bima, tena akapata Bima Premium na akatibiwa bila shida ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Wizara hizo. Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, TAMISEMI, kwa maana wale vijana wa boda boda, bajaji wasajiliwe kwenye mfumo rasmi, na wanaweza wakakatiwa Bima za Afya hizi kupitia biashara yao yenyewe badala ya Serikali kubeba mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu uwekezaji wa viwanda. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri. Hili alisimamie kweli kweli. Atapata vikwazo. Mheshimiwa Shabiby aliongea kwamba biashara hii imebebwa na mataikuni, ni sawa sawa na biashara ya madawa ya kulevya. Atapata vikwazo vingi sana, lakini asimame imara. Hiyo pekee itapunguza gharama kubwa sana za matibabu kwa wananchi wetu na nchi yetu kwa ujumla. Kwa hiyo, hilo alisimamie na aishike sana private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa niende mbali zaidi. NHIF, Mfuko wa Bima ya Afya ninadhani hao ndio wawe wa kwanza kuwekeza kwenye viwanda kwa sababu wana fedha, hivyo wanaweza wakawekeza kwenye kutengeneza viwanda vya kutengeneza dawa, wakatengeneza viwanda vya kutengeneza dripu za maji na zile huduma zikapungua sana gharama ndogo sana kwa wananchi wetu. Hii ni kwa sababu yeye ndiye hatimaye anayekwenda kukusanya ile fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa ninaomba sana NHIF aanze kuwekeza kwenye viwanda vya dawa. Kwanza atatengeneza ajira na pili, atatumia malighafi inavyotokana na wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa dawa za vikohozi atapata tangawazi, zinalimwa kwenye shamba letu, atapata vitunguu saumu, vinalimwa kwenye mashamba yetu sisi, atapata malighali mbalimbali, hata asali inapatikana hapa nchini. Kwa hiyo ni dawa nyepesi ambazo zitaongeza ajira kwa watu wetu, na pia zitauzwa kwa gharama nafuu kwa sababu itakuwa ni dawa ambayo inatengenezwa kutokana na malighafi za kwetu hapa.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kuhusu uadilifu wa watumishi wa afya. Ni kweli kwamba Serikali imeajiri. Tunampongeza Mheshimiwa Rais ameajiri watumishi 5,000, lakini wengi wanaenda kusomea zile kazi ili apate ajira ili ndani ya mioyo yao hawana ile spirit ya kwenda kuhudumia watu.

Mheshimiwa Spika, baadhi yao wanakuwa na lugha mbovu, wananyanyasa wazee, wananyanyasa akina mama wanaokwenda kujifungua. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba sana, atakapokuja ku-wind up, atufafanulie na utueleze kwamba ni hatua gani atakayoichukua? Kabla ya watu kwenda kuajiriwa, wanapelekwa kwenye mafunzo ya aina gani ili kuwajengea uadilifu na kwenda kuipenda kazi yao?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi ya kuhudumia wagonjwa ni kama ibada ni kama mtu anaenda Msikitini au Kanisani kwa hiyo inahitaji uadilifu wa hali juu sana. Sio wote, lakini kuna baadhi ya madaktari na manesi hawana uadilifu, na mwisho wa siku wanatuchonganisha sisi Serikali na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ya kwangu ni hayo. Ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)